Thursday, December 28, 2006

UNAFIKI WA WAANDISHI KTK KUPONGEZA MWAKA MMOJA WA KIKWETE MADARAKANI


Naaam, rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania JMK ametimiza mwaka mmoja tangu watanzania wamuamini katika kuwaongoza.
Mwaka mmoja si kipindi kizuri cha kuamua na kutoa tathmini ya kilichofanya na mtu tunayetegemea atuongoze kwa miaka mitano.
Waandishi wengi sana wamejitokeza kutoa na kuelezea mafaniko ya rais ndani ya mwaka huu mmoja, kila mmoja amemsifu na hii ni haki yake.
Tunajua kabisa rais amekuwa ni kipenzi cha waandishi wengi tangu enzi za mchakato wa uchaguzi na mpaka anakuwa rais, kwa hali hii si rahisi kwa watu waliokuwa wakimtukuza kama mtu mwajibikaji kuanza kumtenga na kueleza uhalisia.

Kwa upande wangu mimi sioni mafanikio yoyote kama baadhi ya waandishi wanavyotaka kutuaminisha na vyombo vyao, tazama hali ya usafiri kwa wakazi wa Kigamboni jirani kabisa na ikulu, siwezi kuyaona mafanikio ya kodi tunazoambiwa zinakusanywa kwa mabilioni wakati hakuna pantoni la uhakika, au hawa waandishi wanataka tufe baharini na waandike habari za kiongozi kuja kuwatembela ndugu zetu.

Hizi sifa anazopea JMK ziangaliwe tena kwani hakuna mabadiliko yoyote
HERI YA MWAKA MPYA

Wapendwa wasomaji wa blog hii, ninapenda kuwatakia baraka na mafanikio katika mwaka mpya wa 2007

Machweo inaahidi kutochoka kuwapa kile ambacho kinafaa kwa macho na akili zako, na kwa mwaka huu 07 tegemea makubwa zaidi

Saturday, December 23, 2006

HE!!! INAWEZEKANA.......

Juzi tumekuwa na kikao na mshauri wa wanafunzi (mwaka wa pili) kikao kilikuwa na mabo mengi yaliyoongelewa kikubwa ikiwa ni masuala mbalimbali ambayo wanachuo tunaona hayaeleki kwa kuwa hayajawekwa wazi na uongozi, kwa mfano suala la ada pamoja na utafiti , inakuwaje tunatoa pesa nyingi kila mwaka wakati utafiti tunaufanya kwa mwaka mmoja tu, pia tunalipa kodi kubwa ya pango (21000/=)kila mwezi ilhali huduma katika hosteli ni mbovu hususani ubovu wa makabati na upungufu wa matundu ya vyoo, hebuchukulia mfanowa hosteli ya Kizota juu ambayo inawakaazi karibu 70 lakini wote hawa wanategemea matundu mawili ya vyoo pamoja na milango minne ya mabafu!
Huduma ya chakula inatolewa na mtu mmoja tu, kwanini, ina maana hakuna watu wengine wa kutoa huduma kwa wanafunzi hasa ukizingatia kuwa mtoa huduma huyu hatoi huduma zinazoendana na namba ya wanachuo! Nani katika menejimenti anamlinda,kwanini serikaliya wanafunzi inasema kuhusu tatizo hili na blahblah toka kwa utawala ndo zinatawala!

Usiogope! haya yalijibiwa na mshauri ambaye kwa kweli alijitahidi sana kupunguza jazba za washikadau!
Hii ndo hali halisi iliyopo hapa chuoni na labda tutegemee mabadiliko kwani ukarabati uliochukua muda mrefu kuliko ujenzi ndo kwanza upo katika hatua za mwisho huku sisi wanachuo tukikosa maktaba na hivyo kufanya masomo yetu kuwa magumu hasa ukizingatia kuwa kutegemea maktaba za nje ni ghali kwa mabo ya kivuko ambacho kinachukua muda mrefu kuvusha watu huku ratiba ikiwa inatukaba kwa sana. Hii yote tisa ni hili lililotokea mkutanoni lilianza hivi...

baada ya dean kutoa nafasi kwa wanachuo kuuliza maswali na kutoa yote yanayowakereketa, akasimama mwanadada wa kozi ya Gender anaitwa dada Agnes, huyu ni mlemavu wa macho, haoni na kwa hapa chuoni yupo peke yake.

Aliposimama kuongea kila mtu ukumbini alinyamaza ili kusikiliza nini anasema, akiongea kwa sauti inayosikika masikioni kwa uzuri kabisa aliyatoa yake mengi na hasa lile ambalo yeye analiona kwamba kuwepo kwake hapa chuoni kumekuwa ni mzigo na inawezekana kwa kuwa chuo kimemuona ni mzigo kimeshindwa kuwapa nafasi walemavu kama yeye walioomba nafasi za masomo chuoni.

Yeye anakabiliwa na matatizo mengi katika kujisomea kwani gharama zote zinamwangukia yeye na chuo kinashindwa kumsaidia japo kwa kumtafutia karatasi za kuandikia. Alijaribu kuwapatia management anuani za mashirika ambayo yanawasaidia watu wenye matatizo kama yake lakini anashangaa hakuna chochote kilichoendelea, hajapata msaada.

Wote tulinyamaza na sikia jibu hili toka kwa Dean "si kweli kwamba chuo kinakuona wewe kama mzigo, kinajivunia kuwa nawe hapa na hata huwa naona wageni wanapotutembelea hapa huelezwa kuwepo kwako hapa". Naam, tulishukuru kwamba mshauri mwenyewe aliahidi kumsaidia dada huyu ili aweze kufanikisha kile kilichomleta hapa na kumwelewesha kwamba chuo hakina noma na kuwepo kwake hasa ukizingatia vyuo vyenyewe ndo hivi tu.

Kikao hakijaisha, nitakuwa nikikutaarifu kadri siku zinavyokuja kwani kuna fukuto ambalo linahitaji majibu na kwa hulka ya 'wakubwa' labda wanasubiri kitendo kitokee ndipo waseme wanavyoona ni sahihi kwa wanachuo kufanya

Miaka 45 ya uhuru: viongozi huru wenye suti za kikoloni

Naam, sherehe za kuadhimisha miaka 45 ya uhuru wa Tanzania (ipi ilipata uhuru, Tanganyika au Tanzania!) zimemalizika na kamati imevunjwa huku waziri mkuu akijipanga tena kuongea na wafanyabiashara ili wasaidie katika maandalizi ya sherehe zijazo.

Sherehe hizi zimefanyika kama kumbukumbu kuadhimisha uhuru wan chi yetu toka kwa wakoloni, waingereza ambao walipewa jukumu la kuwa waangalizi (Tanganyika became the british protectorate) wan chi yetu kwani Un haikuwa watawala na mnamo tarehe 9desemba 1961 bendera ya malkia ikashushwa na bendera yenye rangi nne kumaanisha Tanzania ikapandishwa.

Miaka 45 si mingi sanakwa miaka uhai wa taifa japo si haba kujivunia miaka hii tukiwa huru, na kwa kufikisha miaka hii hakuna haja ya kuacha kusheherekea kwa mbwembwe na majivuno mengi kuonesha ni nini maana ya kuwa huru.

Kusheherekea uhuru ni jambo muhimu sana yaani ni kama mtu wa kawaida anaadhimisha ‘birtday’ yake. Uhuru unamaanisha hali na uwezo wa kujiamulia mabo yako bila kuingiliwa na nchi au taifa jingine (sovereignity).

Sherehe za mwaka huu zimekuwa tofauti kidogo na zile zilizokuwa zikifanywa na wamu zilizopita. Hizi zilikuwa ni za ari mpya, nguvu mpya na ari mpya.

Zimekuwa ni tofauti kwa maana ya kwamba hizi zimeendana na mkesha wa nguvu uliooneshwa moja kwa moja na luninga ya taifa (TVT). Hii iliwapa nafasi watanzania wote kushuhudia sherhe hizi zilizoambatana na tatizo la kukatika katika kwa umeme..

Suala la kukatika kwa umeme siyo ishu iliyonishawishi na kunivuta kuandika kuhusu maadhimisho haya. Na wala sitaongelea suala la waziri mkuu kuwaomba wafanyabiashara wakubwa wajitokeze kuchangia na kufanikisha sherehe hizi zinazokadiliwa kugharimu bilioni moja na ushee pesa za kitanzania.

Wengi wameongelea kuhusu sherhe hizi, wapo waliohoji kuhusu suala la ni nchi gani iliyopata uhuru, mwandishi nizar visram yeye anashangazwa na tukio la waziri mkuu kukutana na wafanyabiashara ili wafanikishe sherehe hizi, kwake hili ni kama kuibinafsisha siku muhimu kwa watanzania wote.

Wanasosolojia nao hawakuwa kimya katika kuadhimisha shehere hizi zilizoshuhudia kwa mara ya kwanza madege yetu ya kivita yakipita kwa mbwembwe kusherehekea siku hii muhimu, wao wamehoji kuhusu ni nani hasa anayesheherekea siku hii kwa watanzania. Kwao matabaka yanayojitokeza nchini yanawafanya wahoji je ni kweli sherehe hizi ni za wote au ni kwa baadhi ya watanzania? Haya yameongelewa na si vibaya kuyajadili katika nchi hii inayoadhimisha miaka 45 ya uhuruhuju pengo kati ya maskini likiwa linaonekana wazi, maendeleo ya mijini na vijijini yakiwa na tofauti kubwa na huku mipango ya maendeleo vijijini ikijadiliwa na watu wa mjini.

Sasa turudi kwenye mada kwani isije nikaonekana nataka tu kujaza kurasa, lakini hata hayo niliyoyagusa ni muhimu yakajadiliwa na pia yatatuongoza katika kutambua mada ya leo.

Mavazi ni kitambulisho kikubwa cha uataifa wa mtu kama zilivyo pesa, wimbo wa taifa pamoja na ramani ya nchi. Leo hii ukiangalia nchi huru nyingine za kiafrika utaweza kuwatambua raia wan chi hizi kwa kuyaangalia mavazi wanayovaa, hebu chukua mfano wan chi za Nigeria, Ghana na afrika kusini. Tanzania na uhuru wetu bado hatuna vazi letu la taifa.
Katika mkesha wa kukaribisha saa sita,pale mnazi mmoja, wote tutakuwa mashahidi kwa namna viongozi wetu walivyokuwa wamependeza katika mavazi mazuri ya gharama toka magharibi. Kwa kifupi mavazi hasa yaliyokuwa yamevaliwa na viongozi yalikuwa ni kama tunaadhimisha uhuru wa nchi moja ya kimagharibi.


Tumeshuhudia umati wa watanzania waliohudhuria mkesha huu wakiwa na mavazi ya aina tofauti, huku wengi wasio jukwaani wakiwa ndani ya mavazi yaliyo kwenye ‘chati’ kwa sasa miongoni mwa watu wa chini ‘mitumba’.

Huku mkesha ukiambatana na ulipuaji wa baruti, tumeshuhudia viongozi wetu waliokuwa wakishuka toka katika magari makubwa nay a gharama wakiwa ndani ya suti nzito na za gharama. Tumeshudia viongozi wanaume wakiwa ndani ya suti nzito toka kwa wabunifu wa kimagharibi, mavazi ambayo yanaonesha kabisa kwamba inawezekana tukawa tunajitawala kwa kufikiri na kuvaa kimagharibi! Angalau mavazi yaliyokuwa yamevaliwa na wanawake viongozi yalijaribu kuonesha utamaduni wa kiafrika kwa kuuvaa Unaijeria na Ughana.

Kwa maisha ya leo yawezekana kabisa baadhi ya watu wakaona suala la mavazi ni ishu ndogo sana kiasi cha kujadiliwa katika kuadhimisha miaka 45 ya uhuru wan chi yetu. Kwangu hili ni suala la kujadili kwani kujitawala ni pamoja na kuonesha waliotutawala kwamba sasa sisi tuko huru yaani tunaweza hata kuwa na maamuzi katika mavazi ya kuvaa.

Uhuru una maana nyingi sana ikiwa ni pamoja na kuonesha hali ya kuwa na maamuzi katika utamaduni wako unaoongoza maisha yako ya kila siku. Mavazi ni sehemu ya utamaduni.
Utamaduni ni zaidi ya ngoma tunazozishudia zikialikwa kutumbuiza katika sherehe hizi. Ngoma kwa sasa kwa baadhi ya watu zimekuwa zikionesha ukale, kinachotamba sasa ni utamaduni wa ‘bongo fleva’. Tumeshuhudia kila mara vikundi vya ngoma vilipokuwa jukwaani havikupata mapokezi mazuri toka kwa hadhira lakini pale walipopanda ‘wanaume tmk’ wakiwa wamevaa mavazi ya kisasa kelele za kushangilia zililipuka. Huu ndio utamaduni tunaoushabikia sasa na miaka 45 ya uhuru.


Mwandishi mahiri katika suala la utamaduni wa mwafrika, mwanazuoni Kihumbi Thairu (the African Civilization) anawashangaa wale wote wanaodharau mavazi yetu na kukumbatia mavazi ya kigeni yasyojali hali ya hewa na mazingira ya nchi zetu za kiafrika. Mavazi haya ya kigeni tunayoyavaa sit u kwamba yanashindwa kututambulisha sisi ni kina nani bali yanatufanya tukose sababu ya kusheherekea uhuru wan chi yetu.

Kwa jinsi kila kitu kilivyokuwa kikifanyika pale mnazi mmoja huku kila mmoja akiwa katika vazi lake ni uthibitisho tosha kwamba kwa sasa tuko huru kweli kweli na mwingereza hana chake tena..

Jukwaa zima lilikuwa limetawaliwa na mavazi ambayo hayakuonesha maana ya kusheherekea uhuru wetu. Miaka 45 ya kujitawala ni mingi sana kuweza kujiamulia ni nini tunapenda kuvaa, baadhi yetutumechagua kuuvaa umagharibi ndani ya umaskini wa uhuru.
Natambua juhudi zilizofanywa na baadhi ya watu waliokuwa na mapenzi ya kutupatia watanzania kitambulisho kwa kubuni vazi la taifa. Hii ilikuwa nikipindi cha miaka ya 2000 na ninakumbuka kwamba baadhi ya wabunifu walifika mpaka kule Dodoma nyumbani kwa bunge la watanzania.


Kama ilivyo kawaida ya waswahili ‘watu wa ahadi’ suala hili sasa hakuna anayeliongelea na hata vazi lililoshinda nadhani sasa litakuwa limepambwa makumbusho kwa ajili ya kuvionesha vizazi vjavyo kwamba hili ni vazi la kitanzania ambalo halikuwavaliwa kwani wazazi wao walikuwa wakivaa mavazi mengine kwa kuwa tu walikuwa huru, wenye uwezo wa kujiamlia mabo yao wenyewe bila kuongozwa na mtu mwingine.

Kwangu mimi tofauti niliyoiona katika upande wa mavazi ina maanisha vitu vingi sana ikiwemo suala la kuibuka kwa matabaka katika jamii yetu. Matabaka ambayo yanashindwa kuelewa maana ya uhuru wa nchi yetu.

Mika hii 45 ya uhuru na mavazi yaliyovaliwa na wakati wa sherehe hizi na hasa yale ya viongozi wetu yanaonesha kabisa kuwa sasa uhuru wetu umekuwa ni kwa ajili ya kuchangisha pesa toka kwa wafanyabiashara wakubwa ili kufanikisha sherehe hizi ambapo mtanzania wa kawaida anaishia kukesha akiwa amevaa mavazi yasiyoeleka hasa mitumba huku viongozi wakijichana wakiwa ndani ya suti nzito zilizobuniwa na wabunifu toka kwa wale tuliokuwatukiwaita wakoloni na mabeberu.

Kwa kuona kwamba katika sherehe hizi hakuna aliyekuwa uchi, basi sula la vazi la taifa si muhimu hasa ukizingatia kuwa nchi yetu na utawala huu una mambo mengi ya kuonesha sasa tuko huru. Kila mmoja amevaa nguo anayoitaka na kumudu kununua kutokana na ruhusa ya kipato chake. Kwa kuwa na mambo mengi ya kuleta maisha bora kwa kila mtanzania suala la mavazi si la kujadili kwa sasa
SIKUKUU NJEMA WASOMAJI!!!


Ni kipindi kingine tena msomaji wa blog hii ambapo wakristo wote wanaungana na wenzao wengi duniani katika kusheherekea sherehe 'birthday' ya mkombozi wa maisha yao Bwana yesu Kristo. Hii ni siku kubwa na inatukumbusha juu ya nafasi yetu tuliyonayo katika kutekeleza lile lililotuleta duniani na tunahitajika tufanye nini ili tuingie mbinguni(kwa wanaoamini katika hili tu-wakristo)
Machweo inapenda kuwatakia watu wote msimu mzuri wa sikukuuza 2006 pamoja na Heri ya mwaka mpya 2007

Monday, December 18, 2006


CHUO KIKUU BILA MAKTABA!
Huu ni ukweli! Unashangaa chuo kimoja hapa mjini tena cha serikali kinatoa elimu ya juu bila kuwa na maktaba ambayo jengo lipo ila linakarabatiwa. Tunaunda wasomi wa vitini na madesa. Hii ndo bongo kila kitu usanii, fikiria mkandarasi wa kujenga jengo la wizara ya maendeleo ya jamii amemaliza jengo la ghorofa saba na kumshinda mkandarasi wa hapa chuoni ambaye alikuwa na kazi ya kukarabati milango na kupaka rangi, hii tenda ina walakini kwani wanaoumia ni wanaolipia huduma hii ya elimu na wanaofaidika na ukosefu wa maktaba ni wale waliosaini mkataba wa kuruhusu ukarabati.

Ukarabati umechukua miezi minne na sehemu na mpaka sasa hakuna kilichokabidhiwa kwa chuo ila jengo linang'aa kwa rangi nyeupe
LONGOLONGO ZA RICHMOND! KUNA 'WAKUBWA' HAPO

Mmeyasikia wenyewe, hakuna haja ya kuyarudia kuyaandika malumbano yanyoendelea kati ya shirika la ugavi la tanesco na 'wasanii' wanaojiita richmond. Hawa waliingia mkataba wa kuzalisha megawati 100 za umeme kwa kutumia majenereta yao waliyotoa marikani na kuiuzia tanesko. mitambo iliwasili na baada ya mbwembe nyingi sana za kuahidi kuzalisha kwanza megawati 20 kabla ya tarehe 1desemba2006 huku wakisaidiwa na waziri wa nishati, hakuna umeme uliozalishwa.
Sasa wamekuja na longolongo ya kusema kwamba eti tanesco imewapatia gesi chafu yenye kokoto! ukiniambia gesi kuwa na kokoto kwangu mimi nitakushangaa, hivi kumbe gesi ina kokoto kama zile za kujengea zege!
bado ninalia na wale wote waliofunga mkataba na kampuni hili linalodai lina makazi yake marekani huku mwakilishi wake hapa akiwa na mkoba tu, huu ni usanii

Hivi JK anasubiri nini kuwawajibisha wanasiasa waliosani mkataba huu, wakati mwingine ninajiuliza kama waziri mkuu alikuwa na sababu ya kulijibu shairi la bwana Marwa akijitapa kuwaonesha viongozi waadilifu waliojaa tele hapa nchini, yaani wamejaa tele halafu wafunge mikataba mibovu kama hii na bado waendelee kuwa wasafi na waliojaa tele.

Jeshi la polisi lipewe kazi ya kuwasaka wote 'waliojaa tele' na kusaini mkataba huu ili wafikishwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake! (unakumbuka enzi za kufilisiwa)

majambazi yakikamatwa basi tv zitarusha sana ama kibaka akiwa mikononi mwa wanachi wenye hasira, kila mmoja hunyanyua mkono ili amwadhibu kibaka lakini majambazi ya peni hapa kwetu yana heshimika sana na wanaonekana mahujaa, naamini kabisa richmond wamekula na 'waliojaa tele' na wanaendelea kutanua katika magari yenye viyoyozi kwani tarehe za pcb ni nyingi kurekebisha na kuua so.
Kaeni kimya mkisubiri uongo mwingine toka kwa wasanii wa Richmond

Monday, December 04, 2006

WASOMI WETU NA MIKATABA FEKI


Usiogope. Nadhani unakumbuka enzi za akina chifu Mangungo wa msovero na lile jasusi la kijerumani Karl Peters, enzi hizo watawala wetu walilazimishwa na kulazimika kusaini mikataba feki iliyowafanya wapoteze tawala zao katika nchi walizokuwa wanazitawala.

Kuna sababu nyingi zilizowanya wasaini mikataba hii, moja kubwa ikiwa ni ile hali ya kujua kusoma na kuandika lugha za kigeni. pamoja na kusaini mikataba hii feki watawala hawa wa kiafrika walikuwa wakichukua muda kuijadili na kuifikiri mikiataba hii.

Tofauti na sasa ambapo watu tuliowaamini katika kuongoza nchi yetu tajiri yenye watu wapole na wakarimu, ndio wanaotuumiza na kutufanya tukae gizani kwa kuingia mikataba ya kutunyanyasa huku wao wakifaidi 'aksante' waliyopewa na mambazi haya.

Fikiria mikataba yote ambayo serikali yetu imesaini, fikiria ile ya madini, IPTL na sasa huu mpya wa sijui inaitwa Richmond, hivi mikataba hii inamsaidia nini mtanzania wa kawaida. Ninasema wa kawaida kwa sababu sasa watanzania tunatofautiana, tuna matabaka yaani ni kama nchi za kibepali.

Mikataba hii walioisaini wapo, tunawajua na wanaendelea kula kuku tu na huku wakituimbia nyimbo za kutukaririsha ya kuwa uchumi wetu unakua! unakua au unakuwa!

Mimi si mchumi lakini siamini ukuaji wa uchumi huku nchi ikiwa haina umeme wa uhakika, ni mgao tu kwa kwenda mbele huku wale tuliowaamini kutuwakilisha bungeni wanakaa kimya na kujadili mambo hata yenye jibu tayari, wanajadili eti kuhusu vazi la spika, inamaana spika yuko uchi au wanadhani wakimnunulia spika vazi jipya ndipo watajadili hoja tunazotaka wazijadiliili.

Kwanza hilojoho akilifua atalinyoosha na nini? OOOps nilisahau kumbe wao ni tofauti na mimi, wao kila siku ni full kipupwe, full kiyoyozii
WASOMI WETU NA MIKATABA FEKI


Usiogope. Nadhani unakumbuka enzi za akina chifu Mangungo wa msovero na lile jasusi la kijerumani Karl Peters, enzi hizo watawala wetu walilazimishwa na kulazimika kusaini mikataba feki iliyowafanya wapoteze tawala zao katika nchi walizokuwa wanazitawala.

Kuna sababu nyingi zilizowanya wasaini mikataba hii, moja kubwa ikiwa ni ile hali ya kujua kusoma na kuandika lugha za kigeni. pamoja na kusaini mikataba hii feki watawala hawa wa kiafrika walikuwa wakichukua muda kuijadili na kuifikiri mikiataba hii.

Tofauti na sasa ambapo watu tuliowaamini katika kuongoza nchi yetu tajiri yenye watu wapole na wakarimu, ndio wanaotuumiza na kutufanya tukae gizani kwa kuingia mikataba ya kutunyanyasa huku wao wakifaidi 'aksante' waliyopewa na mambazi haya.

Fikiria mikataba yote ambayo serikali yetu imesaini, fikiria ile ya madini, IPTL na sasa huu mpya wa sijui inaitwa Richmond, hivi mikataba hii inamsaidia nini mtanzania wa kawaida. Ninasema wa kawaida kwa sababu sasa watanzania tunatofautiana, tuna matabaka yaani ni kama nchi za kibepali.

Mikataba hii walioisaini wapo, tunawajua na wanaendelea kula kuku tu na huku wakituimbia nyimbo za kutukaririsha ya kuwa uchumi wetu unakua! unakua au unakuwa!

Mimi si mchumi lakini siamini ukuaji wa uchumi huku nchi ikiwa haina umeme wa uhakika, ni mgao tu kwa kwenda mbele huku wale tuliowaamini kutuwakilisha bungeni wanakaa kimya na kujadili mambo hata yenye jibu tayari, wanajadili eti kuhusu vazi la spika, inamaana spika yuko uchi au wanadhani wakimnunulia spika vazi jipya ndipo watajadili hoja tunazotaka wazijadiliili.

Kwanza hilojoho akilifua atalinyoosha na nini? OOOps nilisahau kumbe wao ni tofauti na mimi, wao kila siku ni full kipupwe, full kiyoyozii

Monday, November 20, 2006

Kutodhibiti fedha hizi, kauli ya Kikwete itakuwa ndoto

MIONGONI mwa falsafa ambazo zinanigusa mno nafsi yangu ni msimamo wa Rais Jakaya Kikwete kuhusu suala zima la ukuaji wa uchumi.

Rais Kikwete amekuwa akisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unaoelezwa kwa wananchi na ama wataalamu wa uchumi au viongozi wa siasa, kwamba uchumi umekua huku hali za wananchi zikiwa duni haiwezi kuwasaidia.

Kiongozi huyo wa nchi ambaye nyota yake ya kukubalika inazidi kung’ara kwa rika zote na kwa watu wa kada mbalimbali, ana maana kuwa takwimu zilizoko katika karatasi zikionyesha kukua kwa uchumi ni ‘hesabu’ ambazo hazieleweki kamwe kwa mwenye njaa.

Idadi kubwa ya Watanzania ni watu masikini ambao hawawezi hata kuhimili idadi ya kawaida ya mlo wao kwa siku moja.

Ukweli ni kwamba Watanzania wengi hawana njia za kuwahakikishia wanapata chakula cha kutosha na chenye ukamili wake kwa ajili ya mahitaji ya mwili. Mwili huhitaji vyakula vya kujenga, kulinda na ‘kuunakshi’ ili uvutie.

Kutokuwepo kwa ‘msosi’ wao wa uhakika kunasababishwa na mambo mengi, makubwa yakiwa ni rushwa, kutotendewa haki, ubadhirifu wa baadhi ya watendaji wa umma na hujuma za kila aina zinazofanywa ili kuwanufaisha wachache katika jamii.

Juhudi za Rais Kikwete kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anafaidi keki ya rasilimali zetu na uhuru uliopatikana kwa ‘mbinde’ zinaonekana na dhamira yake iko wazi.

Ni dhamira hiyo inayowapa moyo zaidi wa kuwepo kwa neema kwa kila mmoja wetu, ingawa bado ipo kazi ambayo inahitaji pia ushirikishwaji wa wananchi wenyewe katika kuupiga vita umasikini, ambao ulionekana kuwa chanda na pete miaka mingi iliyopita baada ya 1986.

Hata hivyo, upo mwanya ambao hakuna anauyeuzungumzia kuwa ni kikwazo katika kuwakomboa Watanzania na ‘njaa’ inayowakabili.

Njaa ninayoizungumzia hapa ni pamoja ukosefu wa makazi bora, kuzungukwa na magonjwa kibao ya kuambukiza na zaidi sana njaa ya tumbo, ambayo kimsingi ndiyo ufunguo unaozungumzwa na Rais Kikwete.

Mwanya huo ni kuwepo kwa ‘njia nyeupe’ kwa baadhi ya wafanyabiashara kupeleka fedha za kigeni nje ya mipaka ya nchi yetu bila kuulizwa na yeyote.

Hivi sasa kila mfanyabiashara wa fedha; awe Mtanzania wa kuzaliwa, kuomba au hata kudanganya, anao uwezo wa kusafirisha kiasi chochote cha fedha bila kupitia Benki Kuu au katika taasisi zinazoshughulika na masuala ya uchumi.

Haihitaji kuwa na karatasi kutoka chuo chochote kutambua kuwepo hilo na kuthibitishwa na jinsi dola ya Marekani, paundi ya Uingereza inavyopanda kila uchao dhidi ya fedha yetu, ambayo baadhi ya watu wasiokuwa na utaifa wanaziita za madafu. Sina uhakika wanayaangua wapi hayo madafu!

Kuondoka kwa kiasi kikubwa cha fedha ndiko kunasababisha mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa huku wahusika wakifaidi na ‘walalahoi’ ambao ndiyo wanunuzi wakubwa wakikamuliwa hadi tone la mwisho.

Hivi sasa dola moja ya Marekani ni sawa na sh. 1,335 na kwamba kesho au Jumamosi kiasi hicho kitakuwa kimeongezeka kwa asilimia 10 au zaidi. Inatisha sana hali hii.

Nguvu ya soko la dunia mara zote imekuwa ikipimwa kwa kuzingatia fedha ya Marekani, hivyo shilingi yetu zinapokuwa nyingi zaidi kwa dola moja, uchumi wetu unashuka kwa njia moja hata kama itaelezwa kinyume chake.

Zipo nchi ambapo kupata dola moja ya Marekani lazima muhusika atembee kweli kweli kutoka Benki Kuu hadi taasisi zinazohusika, ambako atapatiwa karatasi lukuki kumuhalalisha kuwa anapaswa kupata na kutumia fedha hizo.

Lakini hapa kwetu kila kitu ni bwerere…na ruksa. Ukitaka dola za Marekani nenda tu mtaa wowote, hata kama ni dampo kule Tabata, utapata tu. Hakuna haja ya kuuliza benki ziko wapi. Kwa nini ujisumbue bwana! Ya nini! Ndivyo tulivyo.

Inaweza kabisa kuelezwa kwamba KONA YANGU inahitaji kuwepo kwa urasimu uliokuwepo miaka mingi iliyopita. Hapana hiyo siyo nia yangu.

Lakini ieleweke kuwa bila udhibiti wa fedha hizo za kigeni tutakuwa tukitwanga maji kwenye kinu, na kwamba kauli za viongozi wetu zinaweza kuwa zile zile zilizozoeleka masikioni mwetu.

Hakuna maendeleo bila udhibiti wa mambo kadha wa kadha ikiwemo rushwa na dhambi nyingine, ambazo nimekuwa nikizipigia kelele kila ninapopata nafasi ndogo katika ukurasa huu kueleza.

Ni vyema sasa serikali yetu ikabuni mbinu za kudhibiti usafirishwaji wa fedha za kigeni zinazopatikana hapa nchini, ili kulinda nguvu ya shilingi yetu, hivyo kuimarisha uchumi ambao utatuhakikishia maisha bora kwa kila Mtanzania.

Inawezekana.

Monday, November 06, 2006

WANAOMILIKI SILAHA WAKO TIMAMU!!!

Imetokea majuzi kwa mkuu wa mkoa wa tabora, mtoto wa mjini Dito amemuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala kwa kuwa tu jamaa aligonga gari la mhe. huyu lililokuwa likiendeshwa upande wa watembea kwa miguu. Hii ya kutembea kwenye service road si ishu yangu bali ninauliza hivi kweli kuna uhalali wa kiongozi wa serikali kama Dito kutumia bastola yake kumtaka dereva ashuke garini! na polisi wanatuambia eti ililipuka kwa bahati mbaya!

Naogopa sheria isije ikafumba macho. Tusubiri

Monday, October 30, 2006

MASO SASA MTANDAONI

Kwa muda mrefu sasa wanachuo wa MNMA wamekuwa wakikosa ni wapi wanaweza kusemea na maoni yao kueleka kwa wengine.

MASO serikali ya wanafunzi imeanza kazi ya kuwaunganisha wanafunzi waliosoma katika chuo hiki na wale wanaosoma sasa kwa e mail ifuatayo;

masomnma@yahoo.com

Ukiwa kama mdau wa serikali ya wanafunzi hapa MNMA unaombwa kuchangia kwa kushiriki kuandika mambo mbalimbali kwa kutumia anuani hiyo. Kumbuka uwanja mpana unakuja hivi karibuni

Sunday, October 29, 2006

MASO-MNMA NA TEKNOLOJIA YA BLOG

Msomaji wa machweo, usitishike kusoma kchwa hapo juu kwani nahisi ni kigeni sana kwako.
MASO-MNMA ni kifupi cha jina la serikali ya wanafunzi wa chuo cha kumbukumbu ya mwl. Nyerere.

Kwa mwaka huu wa masomo2006/07 maso iko chini ya rais Hasaan Masudi, na moja ya malengo makubwa ya serikali hii ni kuwaunganisha wanafunzi wote si wa memorial tu bali wa dunia nzima kwa kuingia katika dunia ya blog.

Kwa sasa tegemea makubwa toka katika blog hii itakayokupa mengi toka kwa wanzuoni wa MNMA. Blog hii itakuwa chini ya wizara ya habari inayoongozwa na Obe Mashauri
MRAMBA, BILA MWALIMU, NYERERE NI MTU MWINGINE


Hivi karibuni waziri Mramba aliutangazia umma wa watanzania kuhusu madiliko katika kiwanja cha kimataifa cha dar es salaam. mabadiliko hayo ni katika sehemu moja muhimu sana nayo ni ya utambulisho wa mgeni kujua hapa ni wapi na mwenyeji kujivuna kwa kuwa na utambulisho huo.

Mramba na timu yake wanasema kwamba kutokana na sababu za taratibu za kimawasiliano, kiwanja cha ndege cha dar maarufu kama Mwalimu Nyerere international airport sasa kitakuwa kinaitwa Nyerere IA.

mmmh! hii kweli ndo kasi mpya inayohubri mabadiliko makubwa kwa watanzania na mabadiliko haya ndiyo tunayoyaona sasa, yaani watu kwa utashi wao tu wanaamua kubadili jina la kiwanja hiki kwa kuwa tu wazungu hawawezi kutamka jina mwalimu!

Huu ni ulimbukeni na kama anavyosema msanii wa parapanda Mputo katika ghani zake 'salamu zangu' kuwa msikihubiri kiswahili kwa kukitukuza kingereza, kwani kwa miaka yote jina la nyerere shurti lianze na mwalimu na hapo kila mtu duniani hatohoji kwamba huyu mwalimu ni nani. Alijulikana dunia nzima na harakati zake zinazofundishwa kila kona ya dunia hii.

Kuondoa jina mwalimu kisa tu kuna wachache wanapata shida kutamka ni sawa na kusema JFK IA libadilishwe na kuwa unavyotaka wewe. Mbona kuna majina ya viwanja vya ndege si Africa tu bali na sehemu mbalimbali duniani ni magumu si kutamka tu bali hata kuandikwa lakini ndiyo yanayobeba viwanja hivyo.

wanamachweo wanategemea waziri na wizara yake itafanya kama watanzania wanavyohitaji bila kuhoji kwa nini!

na kwa kumalizia kwa watu wenye mawazo kama ya Mramba ni kwamba huwezi kusema nyerere ukimaanisha mwl Nyerere tunayemfahamu sisi watanzania na watu wote duniani, labda kama mnataka kutueleza kuwa jina hilo halina maana sasa.

Monday, October 09, 2006

CHUO KIMEPATWA MSIBA!!!!!

Ni asubuhi ya tarehe 09/10/2006 kilamwanachuoamekwisha jiandaa tayari kwakwenda darasani,mara rais wa serikali ya wanafunzi wa chuocha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ndugu Hassan J. Masoud anaitisha kikao na wanafunzi wote katika ukumbi wa mikutano.

Hili si jambo la kawaida kwani inaashiria kuna kitu kikubwa wanachuo wanapaswa wahabarishwe, naam, maskio ya kila mmoja yanasubiri nini kitasemwa pale ukumbini na kila mtu yupo kimya. Rais anaanza kuongea ni tangazo la msiba, Msiba mzito wa kaimu naibu mkuu wa chuo ndugu O. K. Temwende

Ni majonzi chuoni na kila mtu haamini kwamba mtu waliyekuwa naye siku moja kabla ametutoka. Kila mmoja anasema analojua na aliloona, wengi tuliongea naye siku ya ijumaa kuhusu tatizo la ada, wengine wakawa naye katika bar ya chuo.

Najua wapo wengi wanaoweza kusema mengi juu ya mwanataaluma huyu, nami pia kwa muda wa kama mwaka mzima tangu nijuane naye chuoni nina mengi yakukumbuka na kujiuliza na kama si kukilaum kifo kwa ukatili uliofanya juu ya mwanazuoni huyu na kada mwaminifu wa chama cha mapinduzi.

Temwende alisoma shule ya Ndanda sekondari zamani sana ikiwa chini ya wabenediktini wa Ndanda shule ambayo miaka ya 90 ilichukuliwa na serikali ambapo nami nilipata elimu ya juu ya sekondari miaka ya 2000. Alipata elimu ya juu katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi na ninachoweza kukumbuka ni pale alipokwendakuchukua masomo ya juu katika moja ya nchi zakisosharist akiwa na A. Mrema kada mwingine wa CCM enzi hizo ambaye sasa ni Rais wa TLP

Darasani marehemu Temwende atakumbukwa kwa kuwa muwazi na siku zote alisistiza umakini na kushirikiana katika shughuli za kimasomo, alisikiliza tatizo la kila mmoja na hakusita kutoa ushauri kwa yeyote aliyeuhitaji.

Marehemu Temwende aliyezaliwa mkoa wa Mttwara alikuwa ni mwandishi mzuri wa makala na kwa wasomaji wa magazeti na hususani wasomaji wa magazeti ya propaganda ya CCM watakumbuka makala zake nzito zilizokuwa zikitolewa wakati Tanzania ilikuwa katika kipindi cha kusaka maoni uwepo wa vyama vingi katika nchi hii.

Temwende alikuwa na dhamana kubwa hapa chuoni na jinalake litabaki katika kumbukumbu za chuo kwani ni yeye aliyeongoza jopo la wahadhiri wa MNMA katika mchakato wa kukifanya chuo kuwa chuo kikuu na hivyo kutoa shahada. Alifanikiwa na matunda yake hakuna anayeyatilia shaka kwani yanaonekana. Alikuwa ni mtu wa vitendo kuliko porojo na propaganda zisizozalisha.

Kuna mengi ya kuandika juu ya marehemu Temwende aliyefariki wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali baada ya kuugua ghafla na kukosa pumzi akiwa nyumbani kwake maeneo ya kigamboni jirani tu na ofisi zake za kazi.

Imetangazwa tuna mapumziko ya msiba lakini mambo aliyoyanya marehemu juu ya chuo na kwa kila mmoja aliyemzunguka hayatafutika na hata wengine kujilamu kwamba kwanini amekubali kufa kama padri Karugendo alivyomlaum profesa S. Chachage kwa kufa ilhali kazi waliyokuwa wameipanga kuifanya haijakamilika na kwa kuwa maisha yanaendelea, kila mtu baadaye atakuwa na furaha na pale Temwende alipokomea basi ndipo tutakapoanzia.

Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa

Pumzika kwa Amani mpendwa wetu Omar K. Temwende

Saturday, September 30, 2006

KUMBE WATANZANIA TUNATUMIKISHA WATOTO!!!

Baada ya Sauper kutuonyesha jinsi tunavyokula samaki mabaki, rais alipiga sana kelele na kuungwa mkono na kila mtu ambaye kwake Darwin9tmare ilikuwa ni uongo kwa kuwa tu kasema raia namba moja.

Sasa kuna hii filam ya IRIN inayoitwa GEM SLAVES Tanzania's Child Labour yaani kwa kiswahili rahisi "utumikishwaji wa watoto katika migodi" filam hii imechukuliwa huko Mirerani wakionyeshwa wanaapollo na 'nyoka' wakifanya kazi ngumu za kutafuta tanzanite wasiyofaidika nayo.

Tumezoea kuandamana na sasa tuusubiri wakazi wa A-town waende barabarani kuilaani filam hii. na cha mno tusubiri rais atakapoenda kuongea na wazee wa arusha atasema nini, kwa kuwa atakachosema kitakuwa ni sahihi kwa watu wanaofikiri kwamba atakalosema ndilo sahii basi tujiandae kuunga mkono hata kama hatujaiona filam yenyewe kama ilivyokuwa kwa wale 'wazalendo' wa mwanza walioandamana kumpinga Sauper bila kuiona hata 'mapanki' yenyewe
NIKO LIKIZO


Nadhani ni kipindi kimepita tangu niweke kitu kipya gazetini. Wengi pia mmekuwa mkiniuliza kwa sms tatizo nini mbona sionekani tena gazetini au ndo kuchoka kwa kazi ngumu ya kuandika. NO. Niko likizo na maeneo niliyopo mtandao ni tatizo na hata ukipata nafasi katika intanet gharama wanazotoza ni kubwa ukizingatia mtoa huduma yupo peke yake 'monopoly'. kwa sasa nimepata nafasi hii kwani niko jijini kwa shughuli maalum.

Wasomaji wangu kaeni mkitambua kuwa nipo na blog hii haiwezi kuwaacha peke yenu

Monday, August 07, 2006

KIKWETE KAPOTOSHWA KUHUSU 'MAPANKI'

Watu wanayala sana na hao sato anaowasema wanaliwa na watu wenye uwezo kama wale waliompotosha kwa kusema kuwa wakazi wa mwanza hawali mapanki, wasaidizi wake wamemwingiza mkenge kwa nia tu ya kulinda vibarua vyao.

Mapanki ndo kitoweo cha wengi hasa waliovijijini.

Hii ndo hulka ya viongozi wengi, wanafikiri wao wanapokula vizuri na kusaza nasi twala na kutabasamu.

Sauper hajakosea hata kidogo kila alichokionyesha ni sahihi kwa sisi tunaoijua mwanza na vijiji vyake

Saturday, August 05, 2006

MAKAHABA TUWAFUKUZE, AU TUWAPE MITAJI WASITEGEMEE MIILI YAO?

Swali hili linatokana na hatua aliyoichukua mkuu mpya wa mkoa wa Dar es salaam bwana Kandoro.
Mkuu huyu baada ya kupewa rungu la ukuu wa mkoa muhimu wa kibiashara nchini tanzania alikimbilia maeneo ya manzese uwanja wa fisi na kuwatimua mabinti wadogo wanaofanya biashara ya kuuza miili (yeye anaiita ukahaba).

Siungani na watu wanaoshabikia kuwepo kwa mabinti hawa maeneo haya kwani licha ya kuwa umalaya/ukahaba si kitu kizuri kwa dunia ya sasa yenye gonjwa la ukimwi lakini wengi wa mabinti hawa ni wasichana wadogo kiumri(wengi wako chini ya miaka 18 miaka ambayo ni ya mtoto kuwa shule akitafuta elimu).

Sasa wamefukuzwa maeneo haya na wengine wamefikishwa mahakamani ambako mahakama imewaachia kwa kuwaona kuwa hawana hatia (ushahidi ni mgumu zaidi ya kumfungulia mtu mashtaka ya uzururaji). Kwa maana hiyo mabinti hawa wamefukuzwa toka maeneo yao na kutakiwa waondoke kwenda haieleweki wapi na wakafanye nini kwani sasa hawatakiwikujihusisha na umalaya/ukahaba tena.

Sielewi kama mkuu wa mkoa alikuwa anatafuta jina katika kurasa za mbele za magazeti yetu ama ni kasi mpya na nguvu mpya!

Unaweza kujadili suala hili, je kuwafukuza hapo ndilo suruhisha au suluhisho ni kuwaandalia mbiu nyingine za maisha kama KIWOHEDE wanavyofanya pale Buguruni. Pia ni lazima jamii ijue kuwa si Uwanja wa Fisi tu kunakofanyika uchafu huu, ni sehemu nyingi sana hapa dar na katikamiji mikubwa mingine kama Mwanza, Mbeya na Arusha
KANDORO NA WAKAZI WA MABONDENI NANI ZAIDI

Wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya za jiji la dar aliwataka kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa katiba. Huu kila mmoja anauelewa ili alinde kitumbua chake

Lakini amewakasirisha wakazi wa mabondeni ambao wamekuwa ni sugu na mara zote wameishinda serikali mahakamani kuhusu suala la kutoka katika maeneo haya hatari hususani maeneo ya jangwani.

Kilichonifanya niandike jambo hili ni ile kauli ya wakazi wa jangwani kwanza kumhusu Kandoro kama yeye na yeye kama mkuu wa mkoa, jiji la dar

Wengi walimweleza kama mgeni ambaye hata mjini hajakaa halafu anaanza kuwaletea longolongo wakati wao wamekuwa pale kwa miongo na watoto wao wanasoma muhimbili primary huku wakipata huduma ya uhakika ya matibabu toka hospitali ya taifa Muhimbili halafu leo Kandoro apange kuwaondoa!

Mgosi (Makamba) kashindwa atakuja yeye! tusubiri tuone kwani kasi aliyokuja nayo ya kuwatimua mabinti pale uwanja wa fisi inaweza kuwa juu ya wakazi wa mabondeni

Tuesday, July 25, 2006

KILA MTU NI MPIGADEBE!

Hata wewe ni mpigadebe
Haya kaandika mwandishi makini wa makala katika gazeti la kila wiki RAI, huyu ni faza Priva Karugendo, nisipoteze kusema alichosema hebu soma mwenyewe na uone alivyoandika na kwa kauli yake hatakomea hapokwani ataandika mengi kuhusu hili(wakati anaandika alikuwa anawahi ndege toka mwanza kuja dar, huyu ni mwanaharakati wa mambo ya kijamii, na mwanafalsafa wa kileo,ukisoma makala yake anayomlaumu Chachage kwa kufa utaelewa ninachokisema) na hivyo usiache kusoma suala hili katika blog hii

Ndugu yangu, Asante sana kuandika. Leo hii nitakuwa Dar. NitaondokaMwanza, na ndege ya saa mbili usiku.Ukipata nafasi uniite kwenye simu. Lakini Juma lote nitakuwa ninakimbia huku na kule. Unajua, Watanzania wote ni wapigadebe! Maana yake ni kwamba: Hatufanyi uzalishaji. Mtu ananunua shati Kampala, analileta Magu, Mwingine ananunua shati lilele na kulipeleka Mwanza, wa Mwanza, analipeleka Moshi, Arusha hadi Dar. Yote hayo ni sawa na kupiga Debe. Mpigadebe, anapata pesa kwa kumleta mtu kwenye gari, ambalo hata kipofu anaweza kujua kwamba linaelekea Mwanza! Anapata pesa bila kuzalisha chochote. Mwisho wa mwezi anakuwa na pesa kuwazidi watu walioajiriwa ofisini!

Umeyaona haya, mengi yaja
WAPIGADEBE

Nimeamua nichokoze mawazo yako wewe mwananchi kuhusu suala la wapigadebe katika vituo vya mabasi ya ndani ya miji (daladala kwa dar na express kwa mwanza)na nje ya miji (yale yaendayo mikoani)

Hawa ni vijana wenye umri wa kati kuanzia miaka 15 hadi45 yaani ni kama marehemu profesa Chachage alivyopenda kuwaita vijana wa kizazi cha dot.com. Aliwaita hivi kwa sababu moja kubwa bayo ni kwamba wengi wa vijana wamezaliwa baada ya tz kupata uhuru yaani baada ya 1961 na wamekulia katika kipindi ambacho nchi imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni,

Tukirudi kwenye mjadala kuhusu kundi hili ambalo sasa linakua kwa kasi mpya na nguvu ya jumbo, hivi ni sababu zipi zinasababisha hali hii itokee

Je jamii inahusika na jamii ni nani kama ni hivyo! serikali na taasisi zake ina mkono katika hili!

karibu utoe maoni yako!

Saturday, July 22, 2006

SOMA UTENZI HUU

Nimeupata toka kwa rafiki yangu anayeblog pia

Utenzi wa Prof Issa Shivji aliouandika juu ya kifo cha ghafla cha guru la sayansi ya jamii prof Seithy Chachage


.Ndugu yangu
Rafiki yangu
Kamaradi Chachage:
Nani kasema umetuacha?

Eti umefariki!
Kwani mwili ndiyo maisha?
Maisha ni fikra. Maisha ni vitendo.
Maisha ni ubinadamu.
Fikra zako,
vitendo vyako,
ubinadamu wako,
utadumu.
leo, kesho, keshokutwa na milele.
Vitendo vyako tutavienzi,
ubinadamu wako tutauiga,
fikra zako tutazieneza.
Msomi wa Afrika,
mteTEzi wa wanyonge,
mshabiki wa fikra za kitabaka,
tabaka la wavujajasho.
nimetumwa.
Nimetumwa na Wasomi wenzako wa Afrika kupitia CODESRIA nikuletee Salaamu zao.
Wameniambia, nikuage.
Nimekataa.
Sikuagi.
Nitakusindikiza tu.
uwaone Wazee Wako,
majirani zako,
watu wema wa Njombe.
Uchanganyike na viumbe wa ardhi na bahari,
viumbe visivyo na ubaguzi,
mipaka,
unyonyaji,
ukandamizaji.
Uwashawishi,
wafundishe wanadamu maana ya ukombozi.
Kama ulivyokuwa unatufundisha sisi daima.
‘Ewe Issa,
kwani,
Shivji siyo mwana wa adamu?’,
Ukanitania,
Ukichota kutoka hazina ya ucheshi wakO bila uchoyo.
"Umejipachikia majina haya yote ya Miungu! MLIMBIKAZI, WE ISSA!’
"Mungu wa Waislamu na Mungu wa Wakristo,
Mungu wa Wahindu na Mungu wa Wasambaa.
unataka wapigane?
wachinjane.
Eti moja ni –a, mwingine ni –ji!’
"Futilieni mbali ushenzi wenu wa kubaguabagua!’,
ukakasirika.
"Unganeni kujikomboa",
umetusihi, "kutoka kwa makucha ya ubeberu na ubepari,
unyonge na udhalilishaji.’
Buriani ndugu yangu,
Buriani rafiki yangu,
Buriani Kamaradi Chachage.
Ufikesalama.
Upumzike na Viumbe visivyonyumbishwa na vituko vya Wanaadamu.
Nakuahidi.
Nitaufikisha ujumbe wa maisha yako.
Kwa WanaUdasa,
Kwa WanaCodersia.
Kwa Wana wa Tanzania,
Kwa Wana wa Afrika………………….Buriani………..

Wednesday, July 12, 2006

BAHATI NASIBU YA MWALIMU NYERERE!!!

Nadhani sasa kila kitu kinafanywa ize isivyo kawaida, umeisikia hii bahati nasibu ya mwalimu!

Inawezekana jina la mwalimu sasa likawa ni ulaji, kama na wewe unachochote unachotaka faida basi andika mswada na tumia jina la mwalimu utapata pesa ule na unywe
PROFESA CHACHAGE KATUTOKA!!!!

Hakika nakosa maneno ya kuandika kuhusu kifo cha ghafla cha guru la midahalo ya kisomi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Inahitaji kuwa na nafasi kubwa kuweza kuandika kile ninachofahamu kuhusu mtaalam huyu wa sayansi ya jamii na mwandishi wa vitabu.

Nakikumbuka kitabu chake ambacho kinapingana na utandawazi usio haki unaopigiwa chapuo na viongozi ambao nia yao si ya jamii nzima bali ni kujitajirisha peke yao na watoto wao, kitabu hicho kinaitwa Makuwadi wa Soko Huria

Si kwamba watanzania tumepoteza lulu bali afrika nzima na wote wanotaka usawa duniani wamepoteza hazina kubwa lakini kupitia maandiko na machapisho yake hakika watazaliwa kina chachage elfu

Nakumbuka msemo wako wakati ukihojiwa na mtayarishaji wa kipindi cha luninga Sema Usikike ulisema neno ambalo sitokaa nilisahau " hakika kuhusu ujambazi kuna sehemu imeoza na wala si sahihi kusema kwamba umaskini ndo chanzo cha ujambazi, jamii na viongozi wa serikali wajiangalie wapi kuna mgogoro unaozalisha wimbi la majambazi na wapiga debe"

Buriani Pro. Seithy Chachage

Thursday, July 06, 2006

KUPANDA KWA ADA MNMA KUNAENDANA NA BAJETI YA KIKWETE?

Linaweza kuwa kama swali la mtu aliyechoka kufikiri. Nimewahi kukuandikia kuhusu kupanda kwa ada hapa chuoni kulikotangazwa na kaimu mkuu wa chuo kama ilivyoamliwa na kikao cha bodi ya chuo hiki chenye jina la muasisi wa taifa hili na aliyekuwa anataka kila mwanachi asome maana yake ni kuwa ada ya masomo iendane na uwezo halisi wa mtanzania wa kawaida.

Sio vibaya kujifikiria kitu ambacho wenzako wanaweza kukufikiria vinginevyo lakini kwa suala la ada kupanda hapa chuoni linamgusa kila mtu anayetoa pesa ili kupata elimu. Inawezekana kabisa waliopandisha ada (bodi) walikuwa na sababu kubwa na za msingi huku wakisaidiwa na utafiti walioufanya kana kwamba kutoza ada kubwa ndo kuonekana chuo bora

Lakini inawezekana kuwa wao kama wao na mishahara yao hawaoni tatizo na ada hii mpya kwani kama watu wanakaa kikao kwa siku na kulipana posho sawa na mshahara na marupurupu ya mwezi ya askari ada hii kwao ni ndogo na ni aibu kuilipa kana kwamba mwalimu alikuwa anafanya biashara ya elimu.

Pia labda bodi ilijua kwamba rais ataongeza mishahara na ndiyo maana ikaamua kuongeza ada ili kutorahisisha maisha kwa namna yoyote na hasa ukizingatia kuwa chuo hiki kipo katika ilani ya ccm katika mkakati wake kukiwezesha na kukikarabati!

Nakaribisha maoni kuhusu suala la kupanda kwa ada. Nenda sehemu iliyoandikwa comment bonyza na andika maoni yako na uyatume. Karibu
TUMEFUNGA CHUO!!!

Ijumaa iliyopita ilikuwa ni siku muhimu sana kwa wote wanachuo kwani ukiacha wengine waliokuwa wanamaliza mwaka wao wa kwanza wa masomo wengine walikuwa wakimaliza kozi zao za stashahada na cheti.

Ilikuwa ni siku ya maagano huku kila mmoja akiwa na huzuni ya kuachana na rafiki yake na furaha ya kupokea cheti na kuanza mwaka mpya wa masomo bila kusahau ada iliyopanda

Blogu hii inawatakia mapumziko mema wanachuo wa vyuo vyote na ni wajibu wetu kutunza afya

Friday, June 23, 2006

GHANA KATUKOMBOA WAAFRIKA

Wakati mwanablogu mkongwe Ndesanjo Macha wa jikomboe.com analalamika kuwa afika si kitu yaani ni sifuri kwa kila kitu anachokitazama yeye na hasa akatilia maanani eti aibu inayozikuta timu zetu ambazo baadhi zimetolewa katika raundi za makundi

Jana Ghana wamemdhihirishia kuwa afica ndiko mpira unachezwa kwani black star waliwachabanga vijana wa Joji Kichaka kwa mabao mawili kwa moja huku ushujaa ukionekana karibu katika kila sekta ya timu ya Ghana hongera kwa wote na hasa kwa mashabiki tuliojitokeza kwa wingi kuwapa shavu vijana wa Africa.

Tunakutana na Brazil! Tutawashinda na ni bora nikasema kama kiungo mahiri wa Ghana Michel Essien alivyosema "tumecheza nao katika under 17 na 21, tunawajua kwani tuliwafunga bila kusubiri uda wa nyongeza" hakika brazil atapigwa bao 3-1 huku Appiah, na Essien wakifunga na Gyan bao kali la kichwa

SHANGILIA GHANA MABINGWA WAPYA WA KLD

Kwa ushindi huu Afrika imepata nafasi moja ya kuwa na timu ya 6 hapo 2010
NI WAKATI WA MITIHANI

Ukisoma bila kufanya mitihani sidhani kama unastahili kuitwa msomi japo hili linaweza kuwa na maana nyingine ila kwa mtazamo wa machweo mithihani ndicho kipimo sahihi kabisa cha kumtambulisha mwanafunzi na mtu mwingine

Mitihani inaanza j3 hapa MNMA kwa niaba ya wachangiaji na wasomaji wa mada mbalimbali katika machweo ninawatakia mitihani salama wale wote tutakaokaa na kufanya mitihani hii.

Vilevile ni kipindi hiki ndipo tunaagana na wenzetu wanaomaliza mafunzo yao ya diploma na hivyo tunawatakia mafanikio mema huko waendako kutafuta ajira katika dunia hii ya utandawazi

Thursday, June 15, 2006

TUNASUBIRI KUAPISHWA!!!

Hassan Jani ndiye Rais mpya aliyechaguliwa kuiongoza serikali ya MASO-MNMA baada ya kuwashinda wapinzani wake wawili Rama Warioba na Rehema H, katibu wake bado hajapatikana kwani Emmanuel Ndunguru na Janeth Soka walilingana kura na hivyo bado tunasubiri utaratibu mpya wa kumpata katibu mkuu, Viongozi waliochaguliwa ni hawa hapa chini na wanasubiri muda tu waweze kuapishwa ili kuingia kazini na kufanya kazi

Rais;- Hassan Masoud Jani SSI
M/Rais:- Bado
Waziri wa Fedha: Edward Biashara Baridi EDI
Waziri wa Afya: F Katanzi GI I
Waziri wa Ulinzi na Makazi: Adam R. Kikono SSI
Waziri wa Michezo na Mahusiano ya Nje: Samwel Mhinga SSI
Waziri wa Habari: Obeid M. Mashauri SSI
KOMBE LA DUNIA 'KLD'

Kama ilivyo ada kwa watanzania kazi yetu sisi ni kushabikia tu timu za wenzetu. Najua sasa wengi wetu tunajiita Waghana, Angola na wengine tunajiona tuna ukoo na kina kafu! Ronaldo. Hizi tabia ndo zetu na wala hatuna haja ya kujiuliza ni kwanini hatuioni timu yetu ikishiriki katika kombe kubwa kama hili japo mara moja.

Tushiriki ya nini bwana kama watu kombe lilishaletwa tena lile orijinali na tukapiga nalo picha na kisha rais akalibeba kuonesha kwamba sisi si wageni katika suala zima la kabumbu.

najua tumejigawa lakini swali tunalopaswa kujiuliza ni nini tunajifunza kwa kombe hili ukizingatia timu kama Angola inashiriki na kuvitoa jasho vigogo! Tanzania ni nchi ya amani lakini haipendeza kuona ndani ya amani hakuna nafasi ya kujitangaza na sasa soka licha ya kutoa ajira ila ni utalii tosha na nchi kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali

Nilitaka kusahau mimi ninashabikia timu hya Ghana na nikiwa kama mchezaji wa soka nafasi ya kiungo mzuiaji na mara mojamoja kufunga ninapendezwa na uchezaji wa Essien, wewe unashabikia timu gani ukiacha Brazil ambayo ni timu ya wote

Furahia michuano mikubwa hii ukijiuliza utafanya nini Tanzania nasi tuweze kushiriki japo raundi ya kwanza

Sunday, June 11, 2006

UCHAGUZI MASO-MNMA UMEKWISHA!!!!!!!!

Mpenzi msomaji wa gazeti hili, juma lililokwisha nilikueleza kuhusu mchakato wa uchaguzi wa serikali ya wanafunzi katika chuo cha kumbukumbu ya mwalimu Nyerere, uchaguzi ulifanyika siku ya ijumaa kuanzia saa kumi jioni na mpaka kufikia saa 12 jioni kazi ya kupiga kura ikawa imemalizika wakasubiriwa mawakala waanze kuhesabu kura 'kula'

nafikiri unajua kuwa nilikuwa ni mmoja wa wagombea nikigombea nafasi ya uwaziri wa habari (usishangae hapa MASO uwaziri unagombea, hawateuliwi yaani wote ni kama maraisi) na nilikuwa na nashindania nafasi hii na mtangazaji wa television Zanzibar.

katika uchaguzi huu nafasi zilizokuwa na ushindani mkali ni nafasi ya urais ambayo ilikuwa na wagombea watatu akiwamo mwanamke mmoja pekee aliyejitokeza ( Anna Senkoro!!!) na vivyo hivyo kwa nafasi ya ukatibu mkuu na makamu wa rais (mtu mmoja anakuwa na cheo chenye nyadhifa mbili).

Upande wa nafasi za mawaziri wizara zilizoshuhudia upinzani mkali ni wizara ya michezo na mahusiano ya nje pamoja na wizara ya afya na kafteria.

Najua unadhani nilishindwa na ndio maaana nazunguka tu bila kukupa matokeo hususani ya wizara niliyogombea.

hakuna kitu kizuri kama kusoma ishara za nyakati na kuzifuata, usipozitii basi yatakayokukuta unaweza ukatafuta wachawi na sababu chekwa huku wapiga kura wakiwa pembeni na tabasamu zito wakikuangalia jinsi unavyohangaika kutafuta chanzo cha wewe kushindwa.

Mpinzani wangu, dada mrembo anayepaka rangi ya shaba nywele zake huku tabasamu tamu likiwa usoni kwake kwa wale anaowafahamu alisoma alama za nyakati na akaona hakika hata angeingia katika mbio hizo basi ingekuwa mashindano ya chui na kobe ambapo mshindi anajulikana.

Siku ya mwisho kabisa alijitoa na nikawa mgombea pekee na ushindi nilioupata siwezi kuuita wa tsunami kwani janga hili linaendana na maafa ila tambua kwamba nilipata ushindi mtamu na ni kura 11tu zilimchagua'mwenzangu' na hizi ni kura mhuhimu kwani zinanifanya nijitambue mimi ni nani na ninapaswa kufanya nini si kwa wale walionichagua tu bali kwa wale muhimu wachache walioamua kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa mpinzani (niruhusu nmwite kivuli)

Bado tunasubiri nafasi moja kwani wagombea katika nafasi katibu mkuu na makamu wa rais hawakufikisha nusu ya kura ili mshindi aamuliwe na hivyo uchaguzi wao jumanne jioni

Tegemea mazuri katika mchakato huu mapema kwani nitakuletea orodha ya wagombea na kura zao.

tafadhari kumbuka gazeti hili sasa liko chini ya wazir wa Habari-MASO

Saturday, June 03, 2006

ADA JUUUUUUUU!!!!!!

Nilikuandikia wiki jana na kukutaarifu juu ya kupaa kwa ada kwa wanachuo wa MNMA.
Jana Ijumaa kaimu wa mkuu wa chuo akaitisha kikao cha wanafunzi na ajenda kubwa ilikuwa ni kututangazia ada mpya ambayo ni tshs 820,000/= toka laki sita, yaani ongezeko la tshs220,000/=
Shabaaaash!!!!!!

Ongezeko hili ni kutokana na kikao cha bodi kilichoketi na kufanya utafiti wa ada katika vyuo vingine! Vyuo vingine vinavyosemwa kuwa ni adfa kubwa ni vile ambavyo havina mkono wa serikali kwa asilimia mia kama kilivyo vhuo hiki.

Kuna maoni mbalimbali kuhusu ongezeko la ada hii,

Nitakuandikia

Wednesday, May 24, 2006

NYERERE 'FEES' INAPANDA! UMEJIANDAA!!!!!!!!!

Huu sio kama ni uzushi bali ni utabiri halisi.

Chuo kimeamua kuongeza ada kwa wanafunzi wa diploma kisa eti wanatoa mafunzo ya komputa.

kweli jina la Nyerere sasa linatumiwa kibiashara

Nitakuandikia tena kwani kama watu tshs 600,000/= nanga inapaa itakuwa hii 800,000/= wanayopanga au ni kwa ajili ya masirahi binafsi ya kujilimbikizia pesa kwa mgongo wa wavuja jasho!!

tangazo hili likitolewa hakika mwalimu atajigeuza alipopumzika

More 2 come
Jamani, nimekuwa nikiwaza na kuwazua; Ni nani mfanyakazi bora katika ofisi zetu Tanzania?

Nauliza hivi kwa kuwa kila ifikapo tarehe kama ya leo kila mwaka, ofisi huwa zinahaha kutangaza wafanyakazi bora. Sijui wanatumia vigezo vipi.
Muda wote wachapakazi ndo wanakosa nafasi hizo na wanaopata ni wale wanaopendwa na wanaowateua; iwe manajimenti, ofisa mtendaji mkuu na wote wanaofanana na hao.
Sasa mimi nasema hakuna cha mfanyakazi bora wala nini. Wote n i watumishi tu na mtindo huo wa kuwepo wafanyakazi bora unadumaza utendaji wa kazi wa watu wengine na ndiyo maana nchi zetu haziendelei.
Nimemaliza

Tuesday, May 23, 2006

NAGOMBEA!!

Unashangaa, huu ndo ukweli ninagombea hata kama hakuna katiba ya kuongoza uchaguzi huu,

Naomba kura zenu katika nafasi ya michezo, kwani mimi nina uzoefu wa michezo yote ya ndani na ya nje
UCHAGUZI BILA KATIBA!!!

Usije ukafikiri ninachokuandikia hapa ni utani. 'Kaimu' rais wa MASO ametoa tangazo la kuwataka wale wote wanaotaka kuingia katika mchakato wa uchaguzi wa serikali ya wanafunzi hapa chuoni basi wachukue fomu katika ofisi za MASO!

Kila mmoja maeliona tangazo hilo lenye sahihi tu ya rais bila muhuri wa MASO yaani kwa ufupi kama usipokuwa makini tangazo limekaa kama barua tu unayoweza kumwandikia shangazi yako. Kila mtu anajiuliza hivi kweli uongozi hauna muhuri na kama hauna muhuri na kama hauna basi huu ni uhuni na haupaswi kuwepo.
WALIOCHELEWA WAMESAMEHEWA!!!!!!!!!


Juzi nilikuandikia kuhusu suala la wanachuo wachache waliokuwa wamechelewa na chuo kupitia kwa dean! wakaamriwa wafukuzwe na kama watapenda basi warudia mwaka wa masomo.

Wengi wa hawa waliochelewa ni wanafunzi wa mwaka wa pili ambao ni kama wamebakiza siku 26 wamaliza kozi na kutunukiwa diploma yao kama watakuwa wamefaulu.

Mapema leo asubuhi wamepewa barua za kuondoshwa chuoni zikiwa zimesainiwa na kaimu wa naibu wa mkuu wa chuo.Barua hizo hazina rejea hata moja na kuonyesha kosa la mhusika, zimemshangaza kila mmoja hata yule asiyekuwa na elimu ya sheria kifupi ni kwamba zinakanganya sana.

mkanyiko huu hauishii kwenye barua tu kwani wakati wa kipindi cha tatu leo mchana Naibu wa mkuu wa chuo hiki cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, aliwaita wahanga wa msala huu na kuwasamehe, tena kwa msamaa usio na barua.

Inachanganya kuona kwamba mtu umemfukuza kwa barua na unamrudisha kwa kutompa barua, hii haina matatizo ya kisheriakweli au ndo mtindo wa mazoea kwamba mimi ndo kila kitu na ninachosema ndicho kifanywe hata kama kuna bodi yenye dhamana ya chuo hiki

Sunday, May 14, 2006

NIRIPOTI KWA NANI!!!!

Inashangaza sana kama unahubiri kitu bila kuwashirikisha unaowahubiria.

Hivi nikitoka likizo ninaripoti kwa nani au ni kutafuta visa tu. Nitaandika tena kuhusiana na hili kwani kuna mwanafunzi amerudishwa nyumbani kisa amechelewa kuripoti na mbaya zaidi huu ni mwaka wake wa mwisho. Tuelezwe tulipoti kwa nani au kuna kingine nyuma ya pazia

Saturday, May 06, 2006

UMEISOMA HABARI HII!!!!!

Imetoka katika gazeti la Mtanzania April1 eti kuwa kaimu msajili wa chuo cha MNMA amemkaba na kumpora mwanachuo. Hii si habari njem a kwa chuo chenye jina la muasisi wa Tanzania na kama haina ukweli basi ni vizuri tukapewa ukweli halisi ili kuondoa mawazo na maneno yanayoibuka bila mpango. UPOOOOOOO!
UMEISOMA HABARI HII!!!!!

Imetoka katika gazeti la Mtanzania April1 eti kuwa kaimu msajili wa chuo cha MNMA amemkaba na kumpora mwanachuo. Hii si habari njem a kwa chuo chenye jina la muasisi wa Tanzania na kama haina ukweli basi ni vizuri tukapewa ukweli halisi ili kuondoa mawazo na maneno yanayoibuka bila mpango. UPOOOOOOO!
KOMPYUTA NDANI YA MILANGO YA CHUMA!!!!!!

Ndugu msomaji nimeamua kuipandisha kurasa hii ambayo niliiandika mwaka jana wakati chuo hiki kikiwa hakina huduma acha ya kompyuta kwa wanafunzi bali hata mtandao kwa ajili ya kuwasaidia katika kutafuta 'material' kulingana na kozi wanazosoma.

Hali sasa ni tofauti kwani milango ya chuma sasa imefunguliwa na kompyuta zipo huku wasimamizi wa maktaba wakiwepo kusaidia wale wote wanaotatizwa na teknolojia hii. Haya ni mabadiliko na tunajua kuna mengi yanakuja. hebu soma nilichoandika kipindi hicho ambacho leo ni historia


Ukifika na kuuliza ni hakika utaambiwa wanachuo wanasoma kompyuta kwani ni kweli kabisa kuna madarasa mawili yaliyojaa kompyuta na bahati nzuri nyingine zimeunganishwa katika intanet. Majibu utakayopewa ukaridhika na upande mmoja basi ukweli halisi huwezi kuupata na utaondoka ukiwa na furaha ya kwamba kweli chuo kimebeba jina linalostahili hivyo nacho kinastahili.

Labda nikuonyeshe upande wa pili wa majibu uatakayoyapata kutoka kwa walengwa wenyewe, wanachuo. Hakuna mafunzo ya komyuta na hakuna mwanachuo anayeruhusiwa wacha kuzigusa kompyuta zenyewe bali hata kusogelea karibu a milango miwili ni shida, milango yote inalindwa na mageti ya chuma na kufuli maalum yaani kama za benki.

Inashangaza sana kwa chuo kama hiki kutowaruhusu wanafunzi kutumia vifaa hivi kwa ajili yua kujisomea na kufanya kazi nyingine za kitaaluma kwani hakuna ubishi kwamba intaneti inamwezesha msomaji kusoma vitabu vingi na vya wakati huu.

Juzi nimekutana na rafiki yangu namfahamu tangu tukiwa A-level, yupo hapa chuoni na alikuwa library akitafuta kitabu cha Rural Sociology ambacho hakipo katika 'shefu' za maktaba, alisikitika na nikamwona akimjongea mhusika wa library kujaribu kumwomba agoogle' apate japo nini cha kusoma

Hii haipendezi na hasa kama mtu mzima anapohubiri mabadiliko bila kubadilika akitegemea anaowahubiria wabadilike! Inawezekana tu kama wanaohubiriwa wataamua kumbadilisha yeye kwanza na bila kujali watatumia nini kumbadilisha

Nadhani ujumbe huu ni salamu tosha kabisa kwa MASO kutambua kwamba wapo kama daraja la kutusemea sisis tunataka nini, na si kukaa tu wakilipana posho kwa pesa tunazokatwa kama ada ya chama

Pia uongozi hasa kamati ya taaluma ambayo naamini kabisa inaongozwa na mtu anayependa wanafunzi wajifunze vizuri katika mazingira rafiki uatalifikiria jambo
hili

Tuesday, April 18, 2006

MAMBO TAYARI USIKU MSIUWEKE!!!
Ni matumaini yangu kuwa mmekuwa na mapumziko mazuri kwa kila mmoja, nami nimekuwa na mapumziko swaafi kabisa na kuweza kuwasiliana nndugu na marafiki kama unavyojua tena mapumziko yakiisha unapaswa uwe kambini ili kufanya kile chuo,jamii na wewe mwenyewe unachotarajiwa kufanya.
Naam, mambo yamekwisha anza na mapema tu kipyenga kikapulizwa 18/04 na kama kawaida malekchara wakaanza kumwaga lekcha! Unashangaa kuna darasa lilikuwa mahudhurio ya wanafunzi 5, hii haijakaa mwake jamani msiuweke kwani imeshatangazwa kwamba siku ya kufungua na masomo kama kawa.
Wahi usiuweke, duh! inaonekana nyasi zilizozunguka mazingira ya chuo zinapenda sana mvua kwani zilivyoota uatashangaa na laiti kama makwanja yangekuwa yanafanya kazi basi zingeweza kufyekwa kwa ustadi ili kuzifanya zivutie zaidi, nadhani kila mtu analiona

Monday, April 17, 2006

DALADALA NA WANAFUNZI!!!!

Kama kuna mji ambao wanafunzi wanakuwa na wakati mgumu wa kwenda na kutoka shuleni ni Dar. Hii ni kwa sababu namba kubwa ya wanafunzi hawa wanasoma shule za kutwa zilizo mbali hivyo kuwafanya wategemee usafiri wa daladala kwani serikali ya Dar haitoi maelezo ya kutosha kuhusu mradi wa magari ya wanafunzi.
Juzi nimepanda daladala na nikashuhudia sheshe zito kati ya kondakta na 'dent' Hakuna aliyetaka kushindwa kila mmoja alikuwa ni mbabe kwa mwenzake konda anataka nauli ya mtu mzima na denti anatoa 50/=na kitambulisho cha shule anayosoma. Tafrani inaishia kwa abiria kuwa upande wa dent na kila kitu kikawa kama kawaida.
Inanikumbusha wakati ninasoma sekondari na siku moja nikampa konda50/= na kitambulisho cha shule niliyosoma Ndanda (Naleo Pasona en grata, Mwaimu, Limbu, na wengi najua mnaikumbuka shule hii) kumpa kitambulisho akashangaa na kuniuliza kama Ndanda Kosovo ( mwanamuziki wa wajelajela) kama ana shule. Sikutaka kumjibu kwani ni mazoea kwa konda na denti kila mtu kumtegea mwenzake nani aanze kutoa kashfa inayofuatiwa na vita kali ya maneno baini ya wawili.
Bahati nzuri mzee mmoja wa makamo akamshangaa konda kwa kutofahamu hata shule ambayo rais mstaafu Ben Mkapa aka Mr Clean alisoma, konda ulimi ukakatwa nami nikatulia kwa kujiamiani kituo kilichofuata nikashuka.
Nadhani ni wakati muafaka kwa wanadar kujadili ni kwa vipi tatizo la usafiri wa wanafunzi linaweza kutatuliwa pia na mikoa mingine, kila mmoja ashiriki bila kujali ni nani na ana nini!
Jumatatu njema ya pasaka

Saturday, April 15, 2006

ILIKUWA NI TERM YA FURAHA!!!

Wow! Kwa mara ya kwanza!

Barua ya Kaimu Mkuu wa Chuo cha MNMA ilibandikwa ubaoni ikitoa 'shavu' kwa Mr O. K. Temwende ( Kaimu Naibu wa Mkuu wa MNMA) na kamati yake ya taaluma kwa kufanikisha utaratibu wa chuo kuanza kutoa B.A. Mara zote tunajua wakubwa hupongezana ndani kwa ndani na wakati mwingine mkubwa sana hampongezi mdogo na hatambui mchango wake lakini kwa mara ya kwanza barua ya Dk Magotti inasomwa na kila mtu na wote tunakubali na kuithamini kazi ya Mr Temwende. Bravo Mr Temwende na kamati yako!

Wanachuo wote tunapewa vitambulisho vizuri kabisa ( sina uhakika na ubora wake hususani ile nailoni kuachia na kufanya karatasi kuchanika! nakumbuka jinsi dean of student alivyochachalika kuhakikisha vijana wake tunatembea tukiwa tunatambulika,( unamkumbuka yule jamaa wa SS1 aliyesema kwamba alikamatwa na polisi kitambulisho cha kuazimia vitabu maktaba kikamuokoa! Alikuwa anatoka kuwachangia tbl kuwafanya watoe kodi kubwa kwa serikali na mishahara minono kwa wafanyakazi wakitukutanisha pamoja bushtrekker tehetehete!

Hivi tangazokwamba kuna mafunzo ya kompyuta linatuhusu wote

Saturday, April 08, 2006

SIKUKUU NJEMA!!!


Najua kila mtu anajiandaa kwa ajili ya sikukuu mbili kubwa kwa watu wa madhehebu yote makubwa ya dini za kigeni, Waislamu na Wakristo

Najua kabisa kwamba waislamu mtakuwa na maulid ya Mtume na baadaye Wakristo watafungua kwarezima na hivyo kusheherekea Pasaka

Machweo inawatakia sikukuu njema na mkae mkijua kwamba jumatatu chuo kinafunguliwa na usishangae jumanne kukawa na paper si unajua mambo ya kasi mpya na kwa mara ya kwanza
Peace&Love from Geka
HII HAIJATULIA WAZEE

Sina hakika na mitihani tuliyofanya kama ilikuwa imeandaliwa kwa umakini wa kina na kwa kuzingatia hali halisi na jina la chuo.

Usishangae kwani kwa sasa kila kiti kiko wazi kwani sheria ya nchi inatamka wazi bila kigugumizi kuwa sasa hakuna chuo kinachoitwa Kivukoni Academy of Social Science (KASS). Cha ajabu kabisa ambacho kwa sababu tu ya mazoea ya watu kushindwa kuhoji ni kwamba mitihani tuliyofanya ratiba ilikuwa inaonyesha kuwa wanaofanya ni wanachuo wa KASS na si wa MNMA.

Ukiachana na ratiba bado karatasi za kujibia zilikuwa na mihuri ya KASS na si MNMA kama inavyotakiwa kuwa kwani shughuli zote za KASS zimerithiwa na MNMA.
Hii inachanganya na wakati mwingine mtu yeyote bila nia ya kutaka kumsema mtu utaona kwamba ni kama uandaaji wa ratiba na upigaji mihuri ulikuwa ni wa kushangaza kwani mitihani imeandikwa MNMA ratiba na karatasi za kufanyia mitihani zinaandikwa KASS, labda inawezekana kabisa kwamba haya matangazo ni danganya toto na MNMA haijarithi chochote toka KASS

Ninakaribisha maoni kama unaweza kuchangia kwa hili bila kumkashifu na kumsingizia mtu.
Najua wengi sasa mtakuwa na hamu ya kujua nini kinaendelea katika chuo hiki kisicho na journal wala gazeti. Tumia blog hii kusema nini unafikiri na toa mawazo yako ya kitaaluma ili kusaidia wanachuo wote kwani chuo ni zaidi ya majengo na wanafunzi

Monday, March 27, 2006

TUKO MAPUMZIKO


YaaaH! Baada ya mitihani kwisha sasa tuko katika mapumziko ya kama wiki tatu. Ningependa sana nikusimulie kuhusu yale yote yaliyojiri katika kipindi cha examz, nakuahidi nitafanya hivyo kwa sas relax

Sunday, March 19, 2006

Wow! Nmerudi tena. Baada ya kimya kifupi, sasa ninakuja tena na kitu kipya na cha kawaida kabisa kwenye higher institution kama hii ya kwetu. Wiki kesho tunaanza mitihani ya kwa ajili ya term ya pili kwa mwakahuu. Ninachukia mitihani lakini ndo hivyo tena kwani hakuna maana ya kusoma kama hujaribiwi kwa kile ulichokisoma.
Nawajua wengi amabo kila wakisikia mitihani baaasi kuumwa si kuumwa na kila kitu kinabadilika yaani wanaweza kusahau hata kuoga.
Ninachukia mitihani lakini si kama ninaiogopa, la , siwezi kuiogopa kwangu mtihani mgumu kabisa ulikuwa ni wa darasa la nne ambapo kila mwanafunzi kipindi kile alikuwa na kitete cha kuingia darasa la tano. Siidharau mitihani hii ila ni kwamba ninataka kuwaencourage watahiniwa wenzangu kwamba kama wao waliomaliza walifaulu kwa nini sisi tushindwe,
Nawatakia mitihani mizuri na mfanye mkiwa na moyo wa kijiamini. Love

Thursday, March 09, 2006

MWANA 'MASO' BLOGU HII NDILO GAZETI LAKO, LITUMIE




Ni jambo la kushangaza kwamba jumuia ya chuo hiki kilichobeba jina la baba wa taifa la Tanzania Mwl. J. K. Nyerere hakina gazeti la wanachuo. Kila mwenye mawazo yake timamu atajiuliza na kupata jibu lazima awatafute wahusika, nimewatafuta na jibu kutoka kasso halieleweki

Si kwamba hawajui maaana ya gazeti kwa wanachuo la, ni uzembe na mazoea ya labda kwa kuwa library kuna Mtanzania na Rai, Daily Newz na hivi wanachuo wanapaswa wasome na si kuchangia hoja zao katika gazeti lao.

Kwa kuona tatizo hili ninakuomba mwanachuo mwenzangu tumia blogu hii kutoa maoni yako ya aina yoyote ilmradi tu haumtukani yeyote. Tumia lugha yoyote ila ningependa sana kama ukatumia Kiswahili ili na wengine wengi wanaojua maana ya lugha hii katika kuwasiliana wakasoma na kufurahi, kuongeza uelewa na kushiriki katika mijadala mbalimbali ninayoitegemea kutoka kwako.

Nina imani kabisa hata serikali ya wanachuo itakuwa na nafasi ya kuchangia na kueleza yote yanayojitokeza ofisini kwao. Najua matangazo yao mengi wanayatoa kwa kuandikwa kwa mkono lakini kwa kuwa chuo kitaendesha kozi ya kompyuta basi natumaini hali itabadilika na pale ubaoni hatutaona tena tangazo lililoandikwa kwa mkono toka Administration na katika serikali ya wanachuo.

nakukaribisha sana katika blogu hii jisikie huru kutoa mawazo yako yenye kujenga jamii nzima si ya wanachuo tu bali ya wasomaji wote wa ndani na nje ya nchi kwani ni ukweli kwamba blogu haina mipaka na kazi ya kuihariri inahitaji busara ya kutembea na taa mchana
KIKAO CHA SERIKALI YA WANACHUO


Kwa mara ya kwanza tangu nijisajili kama mwanachuo wa hapa THE MNMA juzi tumekaa kikao cha kwanza huku mkuu wa Principal akiwa mgeni rasmi na katika hali ya kushangaza kabisa Dean of Student akawa ndio kama 'MC'wa kikao hicho.

Nilitegemea lugha itakayotumiwa itakuwa ni ya kistaarabu na kirafiki hasa kwa kikao kama hiki cha watu wenye akili zao wanaohitaji kuelezwa yote yanayoona sawa si sawa kwao.

Nitajitahidi kukuletea yote yaliyojiri katika ukumbi huu wa bush trekker

Muhimu ni kwamba kumbuka kwamba ada inatarajiwa kuongezwa kwa kuwa tu kutakuwa na masomo ya kompyuta

Monday, February 13, 2006

KASSO HII NI AIBU

Huwezi kutegemea kitu hiki kitokee katika taasisi ya elimu ya juu kama hapa The Mwl. Nyerere Memorial Academy, imetokea

Inashindikana nini kwa matangazo yanayowahusu wanachuo kuandikwa kwa kompyuta, katibu mzima wa kasso anaandika tangazo na linabandikwa notice board likiwa na maandishi ya mkono na bado huyuhuyu unamtegemea aingie karne ya 21
jirekebishe
KARIBU THE MWALIMU NYERERE MEMORIAL ACADEMY

Hii sio zile Academy zinazoibuka hapa nchini kama uyoga kwa kuwa tu zinawafundisha watoto kiingereza, Ni ACADEMY kwa maana yake.
Siku za nyuma nilikuhadithia kidogo kuhusu kubadilika kwa jina kwa chuo cha Syansi jamii kivukoni, naam sasa kwa sheria rasmi namba 6 iliyopitishwa na bunge na kutiwa sahihi na rais wa jamhuri ya Tanzania imeruhusu kuanzishwa kwa chuo cha kumbukumbu ya Mwl Nyerere.
Kuna mengi ya kukueleza lakini tulia na nitakuwa nikikupa vyote unavyotaka kujua kuhusu chuo hiki kinachotoa shahada, stashahada na astashahada katika sayansi jamii na uchumi/maendeleo
MAHITA ANAPOKUWA MWANASIASA

Huku akiwa ameshika visu vipya vikali vya jikoni, IGP huyu anatoa siri ya kwamba ni jinsi gani alivyokuwa mwiba mkali kwa wanaCUF na kuwafanya wasipate ushindi katika uchaguzi ulioiweka CCM madarakani.
Kamanda nandai kwamba Chama cha Wananchi ndicho kinahusika na mipango ya ujambazi unaotokea katika mabenki hapa Dar. Kwa wasiojua ni kwamba wimbi la ujambazi limetokea katika mabank kadhaa hapa Dar huku mamilioni ya shilingi yakiporwa mchana kweupe na watu wenye silaha, sio visu vya kukatia vitunguu Mahita anavyotaka kutuaminisha kuwa wenye visu hivyo (CUF) wanahusika na uporaji huu.
Hakuna benk/maduka ya fedha na vito hata moja ambapo majambazi yamengia na visu katika kutekeleza majukumu yao. Yanaingia na bunduki kubwa kubwa na si visu kwani hayaendi kuiba vitunguu au kukata kachumbari hivyo kutuonyesha visu na kujisifu kuwa umewazuia CUF kupata ushindi unakuondolea sifa zote za kuwa IGP wa Tanzania, bora ufanye kazi ya siasa na si kutumia ofisi ya watanzania kwa manufaa yako
Pumzika ule pensheni yako waachie Mapolisi wafanye kazi kwa masilahi ya Watanzania na wala si kwa malslahi ya CCM, CUF au CHADEMA

Saturday, January 28, 2006

KISWAHILI: NI WAKATI WAKE SASA
Na: Obe M. Mashauri


Si lengo la makala haya kuwalaumu viongozi waswahili wanaotumia lugha za kigeni katika shughuli zao za kitaifa na hata kimataifa. Lengo la makala ni kutaka tu kuonyesha ni jinsi gani lugha hii iliyotulia kama maji ya mtungini ina uwezo wa kuwawakilisha viongozi hawa kwa kundi kubwa la wananchi wanaowaongoza katika dunia hii ya utandawazi.
Kati ya vitu muhimu ambavyo humtofautisha mwanadamu na wanyama ni lugha. Mwanadamu huyu ana lugha halisi ambayo humwezesha kuwasiliana na mwenzake sehemu mbalimbali. Kiswahili ni moja ya lugha nyingi zinazotumika duniani.
Kiswahili ni kitambulisho kikubwa kwa mtanzania na watu wote wa africa ya mashariki na kati. Ni lugha yenye utajiri wa kila kitu kwa ajili ya mawasiliano katika nyanja zote za maendeleo. Lugha hii inayojitosheleza katika shughuli zote za kiuchumi, utamaduni, siasa, elimu, sayansi n.k.
Kitendo cha mtu kuacha kutumia lugha yake kwa makusudi kabisa mbele ya watu wake ni utumwa. Ni utumwa kwa sababu mtu huyu atatakiwa kuiga mawazo ya wenye lugha anayoitumia. Kiswahili katika afrika mashariki ni lugha makini inayomfanya mtumiaji makini kujivunia na kuringa nayo.
Wakati wa ubaguzi wa rangi nchini afrika kusini, makaburu walikuwa na msemo maarufu usemao “lugha ya mvamizi ikiongewa na mvamiwa basi ni lugha ya mtumwa”. Hii ina maana ya kwamba wavamizi hawa walipofika pwani ya nchi hii(mwaka 1652 ),waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Utamaduni, mawazo na ustaarabu wao ulionyeshwa na lugha zao.
Wazungu wa rangi zote walipokuja afrika kwa madhumuni ya kupora utajiri chekwa waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Lugha hizi weupe hawa waliziita eti ‘lugha za kishenzi’. Ni kwa kutozielewa lugha hizi ndipo wakaja na jibu la haraka na kutuita watumiaji wa lugha zetu washenzi. Tukawa watumwa wa lugha zao tena washenzi.
Utumwa huu wa kudharau lugha zetu bado ni donda sugu katika jamii zetu waafrika. Si ajabu hata kidogo kwa nchi zetu kukuta zimejigawa katika makundi yanayojiita: a) waongea kiingereza na hawa waongea kifaransa!. Bahati mbaya sana na waafrika mashariki tumeingizwa katika makundi haya ilhali tuna lugha yetu, kiswahili.
Makala haya hayana lengo la kudharau lugha nyingine au kuzibeza bali ni kuonyesha tu ni vipi kiswahili (kimeundwa na lugha za kibantu) kinaweza kutumika kusini, kati na mashariki mwa afrika. Sehemu hizi zina majimbo mengi yaliyozaa lugha ya Kiswahili. Mwanazuoni Malcon Guthrie anatoa ushahidi wa hili katika tafiti alizofanya katika karne ya 19.
Kiswahili kama kilivyo kiingereza ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali zilizoko katika bara hili. Ndio maana wanazuoni hukiita Kiswahili kuwa ni kibantu sababu tu kinaundwa na maneno yanayoongewa na wakazi wa afrika.
Kwa mseto huu utaona ni jinsi gani lugha hii inajitosheleza kwa misamiati, nahau na mambo yote yanayohitjika katika kikwi hiki cha maendeleo.
Wengi tumekuwa tukikidharau Kiswahili kwamba si lugha ya maendeleo. Tumekuwa ni watumwa tukiaminishwa kwamba kiingereza tu ndio lugha ya kila kitu. Kasumba hii imegubika vichwa vya waswahili wengi kwamba bila kujua ‘kizungu’ wewe si kitu.
Utumwa huu tunao watu wengi tukifikiri kwamba ‘kizungu’kinajitegemea. Hakuna lugha inayojitegemea yenyewe mfano, kiingereza ni lugha yenye mchanganyiko wa maneno toka nchi mbalimbali zenye makabila tofauti.
Kiingereza kina maneno toka uyunani, hispania, ujerumani na uholanzi. Na hata watu wa kwanza kukiandika walikuwa ni waholanzi wa wakati huo waliokuwa na utaalamu wa kutengeneza mashine za kuandikia (taipuleta) maneno.
Pita siku moja sehemu wanakouza pombe na ujionee mwenyewe jinsi wasomi waswahili wasivyopenda kuongea lugha yao ya pili. Wanadharau lugha iliyofanya kazi kubwa ya ukombozi wa bara la Afrika.
‘Wasomi’ hawa hawataki kuongea lugha yao kwani wakiongea watajishushia hadhi yao ya usomi. Huku ni kuunda matabaka ya wanaojua kizungu (bora!)Na wasioongea kizungu (hasara?). matabaka haya yasipoangaliwa yatatugharimu.
Kiswahili kimejaza misamiati na maneno lukuki ambayo wasomi waliooshwa ‘bongo’kizungu hawaelewi. Watasema Kiswahili kinakosa maneno kama: television, computer, osamaphobia n.k. Hakika watu hawa hawajui maneno haya ni wapi yanatoka.
Hawana habari ya kwamba neno ‘computer’ ni matokeo ya maendeleo ya sayansi, ‘television’ ni neno linaloundwa na maneno mawili ya kigiriki yanayomaanisha kuona mbali. Ukiwaeleza kuhusu luninga, tovuti, asasi, wahanga, kikokotozi, king’amuzi watakushangaa na kukosa ulimi.
Jamii kubwa hasa walimu imekuwa ikitathmini akili ya mwanafunzi/mtoto kwa ufahamu wake wa kizungu, je anajua kizungu?. Hivi kizungu kukijua ndio mtu unakuwa na akili?. Huku ni kuchoka kwa mawazo ndani ya jamii yetu.
Wazazi nao hasa wa mijini wenye kipato wanashindana kupeleka watoto wao katika shule zinazotumia mitaala ya kizungu kufundisha. Huko Kiswahili wala utamaduni wa kiafrika hakuna mambo yote kizungu. Mtu asipoongea kizungu ni kweli hana akili? Kweli!
Kwa kudharau lugha yetu yawezekana ndiyo maana maendeleo hatuna. Mtu anasomea shahada ya ukulima morogoro, masomo hapa ni kwa kizungu. Mtu huyu huyu akimaliza masomo yake atakwenda kijijini kwa wakulima wasojua kizungu. Kilimo kitaendelea kweli ikiwa msomi huyu atatumia kizungu chake kufundisha!.
Wataalamu wapo ila lugha hazielewani. Hapa hakuna maana ya kwamba kwa kutojua kizungu wakulima wetu ni mbumbumbu wa ukulima.
Profesa Kihumbi Thairu katika kitabu chake ‘the africani civilization’anasema “nakumbuka mshtuko nilioupata miaka ya 50chuo kikuu cha Makerere, mwanachuo alimuuliza mhadhiri mzungu wa kitengo cha sayansi ya wanyama kwamba ni kwanini watu wanaanguka katika somo lake?
…Msomi huyu mzungu alitoa jibu fupi tu kwamba ‘kizungu’ wanachuo hawawezi kuandika kiingereza. Upofu wa mwanazuoni huyu bado unawaandama wasomi wetu wengi ambao hawataki kukubali kwamba kiswahili kinaweza kutumika na kutoa matunda mazuri kwa maendeleo ya jamii yetu na dunia kwa ujumla. Hata hivyo mwandishi hamlaumu mzungu huyu.
Kizungu kukijua hakimaanishi akili. Mmoja wa walimu wa kujitolea alipata nafasi ya kufundisha katika shule niliyosoma mkoani mwanza. Wakati aliporuhusu kufanya majadiliano ya somo alishangaa kusikia wanafunzi wakitumia Kiswahili.
Japo wachache walienda mbali kwa kutumia lugha ya asili (kisukuma) lakini wengi tulitumia kiswahili na mwalimu alifurahi kwani somo lake tulilifanya vizuri sana tena kwa kuandika kizungu.
Laiti wasomi na viongozi wetu wangekuwa kama mwelimishaji huyu hakika tungekuwa tofauti na wengine. Maana yake ni kwamba tungekuwa na maamuzi bora bila kutegemea mawazo ya lugha nyingine japo si vibaya.
Kiswahili kingetumika kama lugha ya kufundishia mashuleni basi kiwango cha kufaulu kingekuwa ni kikubwa tofauti na sasa. Wanasaikolojia wanaamini mtu anayefundishwa kwa lugha yake mwenyewe anaelewa zaidi tofauti na vinginevyo.
Hivi majuzi wizara ya elimu ilikataa kusajili shule tatu ambazo zingetoa elimu ya sekondari kwa kufundisha masomo yote kwa kiswahili (gazetila kiswahili la tarehe 17/01/2003). Sioni mantiki ya shule hizi kukataliwa ikiwa wenye kumweka madarakani waziri ni wananchi wanaotaka kufundisha kwa lugha ya taifa lao.
Kuruhusiwa kwa shule hizi si tu kwamba kiwango cha kufaulu kitapanda ila matabaka ya wanaojiona ni bora kwa vile wanaongea kizungu yatatoweka na wote tutapata taarifa sahihi zilizoandaliwa kwa umakini na kwa uwazi. Kiwango cha kufaulu kikiwa kikubwa na shule, vyuo vikawepo maendeleo hayaepukiki.
Watanzania hatupendi kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha yetu ya taifa. Makabati yetu yamejaa vitabu vya waandishi wa kizungu hata kama ni hadithi za watoto. Vitabu vilivyoandikwa Kiswahili havina nafasi kabisa.
Wengi hatujui kwamba sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kiweze kuwa na nafasi katika umoja huu ni budi watumiaji wa lugha hii kuitumia kila mahali ili wengine nao wafuate ili kujifunza.
NINI KIFANYIKE
Lugha hii ni ya kiafrika zaidi kutumika katika umoja huu (AU). Hakuna asiyeelewa shughuli pevu iliyofanywa na kiswahili katika ukombozi wa karibu bara lote la afrika. Hivyo ni stahili yake bila maswali kuwa lugha ya bara zima.
Viongozi wa karibu nchi zote zinazoongea lugha hii(japo kidogo)wasisitize matumizi ya kiswahili katika nchi zao ili kuondokana na kasumba ya kutaka tu mawazo yanayotolewa kwa lugha ngeni.
Mabaraza ya Kiswahili yaundwe kila nchi kama ilivyo kwa nchi za Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda pamoja na nchi nyingine. Mabaraza haya kweli yafanye kazi ya kukieneza sehemu mbalimbali duniani.
Katika umoja huu wa afrika matumizi ya lugha hii yatiliwe mkazo si kama azimio lililoamua kutumika kwa lugha hii kule Madagascar lilivyozembewa. Viongozi waafrika waliacha na kufanya lugha zisizo na asili ya afrika kuamua mambo yao.
Ni furaha iliyoje kwa mtu aliyekukuta ukiwa na lugha yako akaiita kuwa ni ya kishenzi, akiwakuta leo mkiongea kwa lugha yake. Nina hakika atasema ‘nisingewatawala watu hawa wasingeweza kuwasiliana’!
Ni kweli kwamba kazi ya kufasiri vitabu kutoka lugha moja kwenda nyingine ni gharama kubwa kwa nchi zetu. Serikali kupitia mabaraza yake ni budi ifanye kazi hiyo. Watu tumechoka kukariri pindi tufundishwapo. Tufanye kile tutakacho sio wao watakacho.
Wananchi ndio wanaowaweka viongozi madarakani kuwaongoza na si kuwatawala, hii ndiyo demokrasia. Viongozi hawa ni wasomi, baadhi wapenda kutumia lugha zisizoeleweka kwa jamii kubwa.
Kwa hapa Tanzania hotuba nyingi zinazotolewa na viongozi wetu ama nje au ndani zinachefusha, hazieleweki kwa wengi, yaani zimeandaliwa kwa lugha ya kigeni. Kuwa kiongozi bora si lazima ujue kizungu japo si vibaya.
Tuige mfano wa kiongozi mmoja maarufu barani kwetu ambaye alisema kwamba anaongea kizungu ili tu wasiojua lugha yake wamwelewe na si kutaka sifa kwamba ni kiongozi mzuri, makini. Uongozi bora sehemu yoyote hauonyeshwi kwa viongozi kuongea na kuhutubia kizungu.
Mwasisi wa taifa huru la India Mahatma Gandhi aliwahi kusema kwamba katika eneo analotoka ni vizuri akatumia Kigujarati kama lugha ya kiserikali. Huyu ni msomi aliyezunguka nchi nyingi kutafuta elimu, masomo yake mengi aliyasoma kwa lugha zilizokuwa zikimpa shida kuelewa. Uamuzi wake wa kuamua Kigujarati kiwe lugha kuu katika India kunaonyesha uwajibikaji.
Katika dhifa za kimataifa walizofanya viongozi wa mashariki ya kati hapa nchini, hotuba zao zilitolewa kwa lugha zao. Ajabu viongozi wetu walitoa hotuba kwa lugha ya kizungu. Si vibaya nikifikiri kwamba wageni hawa walituona sisi ni vichaa.
Kituko kingine kilijitokeza wakati wa ufunguzi wa jengo la utalii hapa nchini. Kulikuwa na ulazima gani wa kutumia lugha tusiyoielewa, huku ni kutufanya sisi watumwa. Pamoja na utalii, sifa yetu nyingine ni lugha yetu.
Waandishi na watunzi wa kiswahili ni watu muhimu kwa ukuaji wa lugha hii. Ni budi wakitumie Kiswahili katika kazi zao bila kukipindisha. Wanamuziki na wasanii nao watoe kazi zao kwa ubora na umakini wakitumia lugha ya hadhira yao.
Watanzania sasa tujenge kasumba mpya ya kujisomea vitabu vyetu. Tununue vitabu ili kuwapa nguvu wachapishaji na watunzi waweze kufanya kazi za kiswahili bila kinyongo.
Sisi ni matajiri, tumebarikiwa kila kitu lakini kutokana na kudharau utajiri wetu ikiwemo lugha, tumekuwa ni wajima. Sifa yetu kubwa ni umaskini. Wakati fulani madiwani wa mkoani Mwanza waliandikiwa taarifa fulani na ‘wataalam’kutoka ‘PWH’taarifa iliandikwa kizungu. Wakapelekewa madiwani waswahili ‘wengi’. Ili uwe kiongozi hapa Tanzania ni lazima ujue kusoma na kuandika! Kwa ‘ripoti’ hii ya eti ‘wataalam kwa vile wameiandika kizungu’ nina uhakika asilimia 85 ya wawakilishi wa watu walikaa kimya katika kuijadili. La kujiuliza hapa ni hili, hivi sisi nani ametoroga ?
Tunathamini mawazo kutoka nje ambayo lengo lake ni kutuibia. Tukitumia lugha yetu katika mambo yetu tutakuwa tumeondokana na utegemezi wa mawazo kutoka nje.
Kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwa kila mtu zitolewe tuzo nia ikiwa ni kuenzi kazi zilizofanywa na watu waliokipigania kiswahili. Tuzo kama za Ibn batuta, Jumbe Akilimali, Shaaban Robert, Mnyampara na wengine wengi zitatoa changamoto kwa watu kutumia lugha hii.
Kuondokana na utegemezi wa kila kitu katika jamii yetu kumo ndani ya mikono na akili zetu. Kutumia lugha yetu hakuhitaji mzungu kutushauri. Ni wakati wa Watanzania na waafrika kuamka. Tutumie lugha ambazo ni za kiafrika zaidi.
Kujikana kwetu na kudharau na lugha yetu kunatufanya sisi tunaojiona bora (kwa kuongea kizungu) kuharibu hata hizo lugha tunazozikumbatia. Si jambo la kushangaza kumkuta mtanzania anyejidai na kizungu anashindwa kuongea kwa ufasaha lugha hizi za wakoloni.
Maendeleo tunayoyahitaji watanzania yawezekana hata kama tutatumia lugha yetu. Haiingii akilini mtoto anafundishwa lugha ya Kiswahili shule ya msingi tu na akiingia sekondari basi kizungu mtindo mmoja, huku ni kutuchanganya sisi vijana. Tunashindwa kuhoji, kwani Kiswahili hakina nafasi.
Suala la kutumia Kiswahili katika shule na vyuo vyetu halihitaji siasa. Wakati umefika kwa watu wote kuamka na kwa kauli moja kusema sasa ni wakati wa kiswahili.
Utamaduni wa wenye madaraka kutoheshimu matakwa ya wananchi ndio uliomfanya mwenye dhamana ya kusajili shule kuzinyima usajili shule hizo tatu nilizoongelea hapo juu. Nina uhakika kama ni wazungu ndio wangeomba kusajili shule hizo basi kusingekuwa na matatizo, wasomi wanaopenda kiswahili kitumike wanachukiwa.
Sababu kubwa ya kuchukiwa kwa wenye busara hawa ni labda kama kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia basi watapata pesa ya kufasiri vitabu kuwa katika kiswahili. Huu ni upofu wa fikra, hoja hii wala haina mashiko, taifa tulitakalo ni lile linaloona mbali si lenyo watu wanaoona umbali wa pua zao tu.
Serikali inadai kwamba inatoa nafasi kwa wananchi na asasi mbalimbali kutoa mawazo yao ili kuleta maendeleo. Mtazamo huu ninashindwa kuuelewa nikifiria kuhusu kubanwa kwa kiswahili katika kuleta maendeleo.
Tafiti zilizofanywa na Mlama na Materu mwaka 1976 mpaka 1977 zilibainisha kwamba lugha yetu ya taifa itumike katika sekta nzima ya elimu. Mradi wa kuboresha ufundishaji wa kiingereza uliandaa ripoti ya utafiti uliofanywa na wazungu mwaka1991 na kuainisha kuwa bado wanafunzi hawaelewi wanapofundishwa kizungu na wakapendekeza kizungu kifundishwe vizuri tangu shule za upili. Ripoti hii inaonyesha ni jinsi gani watafiti hawa waligundua kwamba kiswahili ndiyo lugha muhimu ya kufundishia katika nchi hii.
Uelewa mdogo wa mambo na elimu baguzi inayotolewa nchini unasababisha tukose wagunduzi na wataalamu mbalimbali katika nyanja zote muhimu kwa maendeleo yetu. Lugha zinazotumika kufundishia ni ngumu. Zinahitaji mtu ukariri na si uelewe. Unategemea nini kwa mtu asiyeelewa?
Viongozi wetu waandamizi nao ni vizuri wakatumia lugha hii ili tusichanganyane. Kitendo cha kutoa hotuba au miswada kizungu ni kutuminya wenye nchi tusihoji na hasa ukizingatia wengi tuna elimu ya msingi kwani sekondari ni chache na ghali. Wadau wote tupate kuhoji na kuelewa kwa lugha yetu sio kwa kizungu tusichokielewa. Hakuna haja ya kuibiana eti kwa kuwa tu sisi wengi hatujui kizungu. Uchumi wetu na maendeleo yetu ni budi tuyaelewe kwa lugha yetu ili inapobidi tuhoji.
Mpaka sasa sina uhakika kama watanzania tuna kitu kinachotutambulisha kwa wenzetu zaidi ya wimbo wa taifa ambao nahisi kuna watu wanatamani ungekuwa unaimbwa kizungu. Huu ni wakati muafaka wa kiswahili kutumika katika Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Maneno yaliyosemwa na mkuu wa chuo kikuu cha Mzumbe wakati wa ufunguzi wa chuo hivho mwaka jana kwamba wataanzisha utoaji wa elimu ya juu kwa kutumia lugha ya kiswahili ni changamoto kwetu. Hii ya kusikia tu kwamba Libya wanafundisha Kiswahili katika vyuo vyao ni aibu kwetu. Tuamke viongozi wa tanzania, kiswahili si wakati wa kampeni tu.
Inauma sana pindi unapotaka kupata habari juu ya kitu fulani habari hiyo unashindwa kuielewa kisa tu lugha iliyotumiwa kwa kumbukumbu hiyo ni ile isiyoeleka kwako. Hivi Kiswahili hakiwezi kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu jamani, au tunashobokea vitu tu. Nafasi ya lugha yetu katika kuhifadhi nyaraka na uhakika ni kubwa, nzuri na ya kudumu.
Hapo juu nimeongelea kwamba Kiswahili si wakati wa kampeni tu kwa viongozi wa tanzania. Watu watumie lugha hii hata kama wamekuwa viongozi. Hivi inakuwaje, unaomba kwa lugha moja na kutenda watenda kwa lugha nyingine wapi na wapi? Hii ndiyo inayotokea nchini kwetu kama huamini na haujaona mimi sina vidhibiti. Vya nini wakati ambapo hata hiyo lugha inayotumiwa siielewi, japo nikiielewa si vibaya.
Inasikitisha kuona waafrika tumesahau utu wetu na hatutaki kuulinda tena, uzungu umetuingia. Tunataka kujionyesha kwa wazungu kwamba sisi ni watu bora kwa kuiga kile wakifanyacho. Tunaiga hata jinsi wazungu wanavyoongea. Tunakwenda wapi sisi waafrika na tunalipeleka wapi bara hili tajiri. Lugha yetu ni budi tuipe heshima tusiivue nguo na kuiaibisha. Kiswahili yafaa kitumike katika shughuli zote za kila siku tuzifanyazo.
Napingana na kauli ya mhadhiri wa lugha za kigeni ya chuo kikuu cha Dar es Salaam aliyoitoa katika gazeti la ‘Sunday Observer’ la tarehe 19/01/2003. Msomi huyu M. Kadeghe anasema kwamba “wazazi wa Tanzania wanajua umuhimu wa Kiingereza katika kipindi hiki…” Kauli ya msomi anayeamini kizungu ndiyo uelewa!
Kutumia Kiswahili katika vyuo vyetu hakutatuweka kando katika kipndi hiki cha kutafuta maendeleo. Hivi nchi kama Japan, Italia, Ujerumani na nyingie zimemudu kupata maendeleo kwa kutumia lugha zao, kwa nini sisi na Kiswahili chetu tushindwe? Nchi hizi zote zinatumia lugha zao na kiwango cha maendeleo zilizonayo zinashinda hata zile nchi ambazo ‘msomi wetu’anazifagilia.
Kauli hii pamoja na ile iliyotolewa na waziri wa elimu ni moja ya kauli zisizofaa kutolewa na watu kama hawa. Watu hawa pamoja na wengine wenye dhamana katika nchi wanatakiwa kutoa kauli zenye busara, walizozifanyia utafiti wa kina na si mjini na kwa watoto wao wanaosoma katika shule za ‘…akademia’. Waende hata kule Mwabayanda, Mpitimbi na sehemu nyingine za vijijini kufanya utafiti na tuone watarudi na ni lugha ipi ifaayo hapa kwetu katika kipindi hiki.
Dk. Kadeghe ni mwalimu wa lugha, alifanya utafiti mwaka 2000 na kuweka wazi kuwa lugha hizi zote mbili zitumike katika ufundishaji lakini mtafiti mwingine Mwinsheikh aliweka wazi kuwa lugha ya kizungu ifundishwe kama somo tu, na masomo mengine yafundishwe kiswahili.
Kwa kutumia taaluma yake ya ualimu toka shule ya msingi mpaka chuo kikuu dk. Kadeghe anaelewa ni jinsi gani mwanafunzi anaelewa somo analofundishwa na kukariri somo analofundishwa. Haiitaji ‘PHD’ kujua kwamba mtanzania anayefundishwa kiswahili anaelewa zaidi kuliko mswahili anayefundishwa kizungu ambaye hakuna anachoelewa zaidi ya kukariri. Usitegemee swali kwa mtu anayekariri.
Lugha ‘ya kizungu’ hawa imefundishwa shuleni na vyuoni kwa karibu miongo minne sasa na hakuna kilichobadilika zaidi ya kuwepo makundi tu. Haijatusaidia kutatua tatizo la kilimo cha kutegemea mvua n.k. Tukipe nafasi Kiswahili na tuone kama hatujawafukuzia Wajapani. Wengi mtaona kama ninaota lakini ni kweli kwamba mtu akifundishwa kwa lugha yake huelewa zaidi na si kukariri.
Wengi mtasema kwamba mbona hata hicho Kiswahili kinachofundishwa wanafunzi wanashindwa kufaulu. Jibu ni rahisi tu kwamba kiswahili hakijapewa nafasi kubwa katika masomo, vijana wanaona ni bora kukariri masomo ambayo karibu yote ukiacha kiswahili yanafundishwa kizungu.
Masomo yakiendeshwa kwa lugha yetu nina uhakika maendeleo yatakuwepo kwani utafiti uliofanywa na Mwinsheikh ulitanabaisha bayana kwamba masomo ya sayansi (yanafundishwa kizungu!) yakifundishwa kiswahili wanafunzi wanaelewa zaidi. Sasa kama mtu anaelewa somo analofundishwa kwanini asivumbue vitu. Ukielewa kitu tabia ya kukariri waliofanya watu wengine itakwisha kwani mtu utavumbua chako.
Kompyuta sasa ni kitu ambacho wengi tunakiona ni kwa ajili ya ‘wateule’wanaojua kizungu. Hii si sawa. Mungu awazidishie nguvu na maarifa wataalamu wanaoweka ‘program’ za kiswahili katika chombo hiki cha kurahisisha kazi. Wote tutaweza kutumia na kupata vitu mbalimbali vitakavyoleta unafuu katika jamii zetu.
Kizungu na lugha zote za kizungu ni bora zikawa kama masomo ya kawaida tu. Ikibidi vyuo vya kufundisha lugh viongezwe ili kurahisisha mawasiliano kwani marafiki zetu wa Ulaya na sehemu nyingine si wote wanajua lugha ya ‘malkia’
Kuiga vitu kunafanya muigaji awe kama mtumwa, mtumwa ni yule mtu anayefanya kitu asichopenda kufanya. Hata kiongozi asiye na msimamo wa kuamua mambo mazuri hatoki ndani ya kundi hili. Kiongozi ni budi aongoze kwa matakwa ya jamii yake.
Hivi hatuna washauri wazalendo ambao ni wataalam wa mambo mbalimbali. Nani ameturoga yaani mpaka mshauri wa kujua nini tunataka atoke ‘uzunguni’ nje.
Kwani kiswahili kutumika mahakamani haki haitatendeka? Hapana
Kutumia lugha yetu shuleni na vyuoni ni dhambi? Hapana
Kiswahili kutumika kwenye makongamano no kosa? Hapana
Je, bila kuongea kizungu mtu anaonyesha kwamba hana akili? Hapana
Tunahitaji washauri wazungu ili watueleze kwama tutumie lugha yetu? Kwa hili jibu zuri laweza kutolewa na viongozi wetu wanaoamini mshauri anayetoa ushauri wake kwa kiswahili si msomi.