Tuesday, February 23, 2010

Picha itakayotoka sitokudai

JE, DINI NA MUNGU WA WAAFRIKA NI MSHENZI?



Ni falsafa ya uongo kwa mtu kuamini kwamba waafrika hawakuwa na dini kabla ya kuja kwa wageni waliokuja kwa nia ya kupora utajiri wa bara hili.
Dini ni njia ya kuhusiana na Mungu. Kwa tafsiri hii ni uongo wenye kutu kusema kwamba kabla ya wazungu na waarabu kutuvamia tulikuwa watu wasio na diniau kwa lugha nzuri kwao nakwa wafuasi wao wa sasa, wapagani au makafiri.
Wengi wetu tumekuwa tukiamini kwa kuaminishwa kwamba dini zilizoletwa na wageni ndiyo dini za asili.ukoloni na utumwa wa maharamia hawa ulitufanya tuamini kwamba Mungu wa majangiri hawa ni wa kweli. Mungu aliyeabudiwa na wenyeji aliitwa mshenzi na mitume wake wakaitwa mapepo. Huu ndio ustaarabu wa wageni.
Baada ya kuwa zimejikita afrika kwa mabavu na propaganda, zimewajaza wafuasi wake falsafa mpya ya kujibagua na kujiona bora zaidi ya wengine
Tanzania na afrika kwa ujumla katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudia vujo na migogoro mikubwa ya kidini inayoletwa na dini hizi za ukristo na uislam katika ama kujitanua au kujiona bora zaidi ya nyingine.
Mbaya zaidi migogoro baini ya dini hizi inawaathiri hata wasiozifuata. Mambo haya hayakuwahi kutokea kutoea kabla ya kuja kwa dini hizi za kigeni.
Historia ni shahidi wa mengi. Historia ya mwafrika haioneshi machafuko au vita vilivyosababishwa na dini za asili. Dini ambazo ‘wakoloni na mabwana’ waliziita za kishenzi huku waumini wake wakibatizwa majina kama wapagani,kaffir na majina mengine mengi ya kipuuzi.
Ukristo na uislamu ni dini za kibiashara zenye historia ya vita katika kujitanua. Itkadi ya dini hizi ilisambazwa kwa heri au shari kwao waliozikataa. Walikuwa wakimtangaza Mungu wao kwamba ndiye wa kweli na hapana mwingine ila yeye.
Ukristo na uislam uliokumbatiwa na waafrika uliletwa afrika si kwa minajili ya kumtangaza mungu wa kweli bali dini hizi zilikuwa ni mbinu za wazungu na waarabu kujitanua kiuchumi na kisisasa katika bara hili tukufu. Biashara ya utumwa na ukoloni vinadhihirisha haya.
Kwa mantiki hii utaona kwamba mungu anayehubiriwa katika dini hizi ni yule anayehalalisha uporaji na uuwaji wa watu wasiomtaka.
Uislamu ulisambazwa kwa upanga mkali uliokata shingo na viungo kwa wote walioukataa. Jitihada zilizofanywa na uthman dan fodio zinadhihirisha jambo hili.
Mabomu,mishale, risasi na uongo nazo zilitumika kuusimika ukristo na yule aliyeukataa aliitwa msaliti, kifo ni zawai yake.
Mtu aliyepingana na dini hizi aliuawa.
Falsafa iliyopandikizwa na wakristo na waislam vichwani mwa waafrika bado inatutawala mpaka sasa. Ukweli ni kwamba kila mtu ana Mungu wake anayeujua utamaduni wake na kila hali yake ya maisha ya kila siku.
Kwa waafrika Mungu huyu alijulikana kwa majina anuai, wapo waliomwita Ngai, Mulungu, Lyoka na majina mengine mengi yanayoonyesha utukufu wake.
Dini za kiafrika ziliabudu Mungu mmoja tu na si kwamba wageni ndio waliowaletea waafrika dini na kuwatambulisha kwa Mungu. Ustaarabu ulikuwapo afrika na wazungu na waarabu ndio waliokopi ustaarabu huu.
Dini za kigeni ziliudharau utamaduni wa mwafrika na kumtambulisha kwa utamaduni mpya wa kujidharau na kudharau kila kilicho chake, akiiponda dini yake na kukumbatia ukisasa eti huo ndio ustaarabu.
Kwa kuudharau utamaduni wake mwaafrika amekuwa kama kasuku, kazi yake ni kuimba kila anachopewa na bwana wake. Lugha za kiafrika karibuni zitatoweka kwa kuwa tu hazina nafasi katika dunia ya wastaarabu. Lugha muhimu ni kizungu na kiarabu tu.
Ukitaka kumtawala mtu basi mporeulimi wake. Majangiri hawa wamefanikiwa kwa hilo. Kwani kila mtu hata kuamini ukisema umetokewa na Mungu anayeongea lugha yako. Wao Mungu ni yule anayeongea kwa lugha zao,Mungu asyeongea lugha zao basi watamwita shetani kama ilivyotokea Joan of the Arc huko London. Kitabu cha the African civilization kinalieleza hili.
Mwanzoni mwa muongo huu watanzania tumekuwa tukishuhudia migogoro na fujo nyingi za kidini zikitokea na ukijaribu kuchunguza kwa umakini migongano hii imekalia katika maslahi binafsi ya dini hizi na si kumtangaza mungu wao.
Machafuko haya yanayotokea ndiyo yanayonifanya nijiulize kama kweli dini zetu zilikuwa za kishenzi?
Hivi matusi, vita, migongano na machafuko yanayotokea katika nyumba za ibadandio ustaarabu tulioletewa?
Hivi wageni hawa walituletea Mungu tuliyemjua sisi au mungu wao mpenda vita, mwenye wivuna mbaguzi? Je, ni kweli kwamba sisis hatukuwa na Mungu? Swali hili nisingependa waljibu wasomi waliokaririshwa kwamba cha mzungu na mwarabu ndio bora
Kama tusingekuwa na Mungu ‘wastaarabu’ hawa wangetukuta kweli? Moyo wa ukarimu tuliowaonyesha japo walitutemea mate, ulitoka kwa Mungu wa kishenzi kweli? Hivi Mungu wetu aliyetulinda na kutupa akili ya kumjua alikuwa ni Mungu aliyevaa ngozi ya kondoo.
Je, mungu aliyeruhusu wengine kupora,kutawala kwa mabavu na kuuza binaadamu kama bidhaa ndiye mungu wa kweli?
Maswali haya pamoja na hili linalosema kwamba ukristo na uislam ni dini za ulimwengu (universal) yananifanya nijiulize na kuchoshwa na hadithi za vitabuni.
Ukweli usiolazimishwa kuukubali ni kwamba dini hizi mbili si dini za ulimwengu kama tunavyopotoshwa. Kwa afrika dini hizi ni ngeni kabisa na hatukuwa na migogoro ya kidini kama tunayoishuhudia sasa katika dini hizi ngeni.
Ni wakati wa waafrika sasa kurejea katika imani ya asili tuliyokuwa nayo, imani inayotutambua sisi na utamaduni wetu. Turudi katika dini zetu ili tutunze ustaarabu wetu, utamaduni wetukila fahari yetu.
Dini zetu za jadi ndizo zitakazotuepusha na migogoro tunayoishuhudia sasa na kwa bahati mbaya sana tunaishiriki tu eti kwa kuwa tumebatizwa na kusilimishwa katika majina mapya tusiyojua maana yake.
Vilevile tujue dini hizi mwanzo wake na wafuasi wake wa mwanzo. Ukristo ulianzishwa na kikundi cha waalimu (rabbi) Yesu akiwa mwanzilisha wakati Uislamu ulianzishwa na mfanyabiashara aliyeitwa Muhamad aliyejiita mtume huko mashariki ya mbali na kuusambaza kwa vita akianzia huko Makka.
Kuzifuata na kuzikubali dini hizi ni kukubaliana na waanzilishi wa dini hiziz na misemo yao kama…ya kaisari mpe kaisari…., na bakora ndizo zitakazoleta usuluhishi kati yetu!
Kukataa kurudia dini zetu ni kukumbatia laana tulizopata kwa kuaminishwa kwamba waafrika hatuna Mungu
Ufumbuzi wa migogoro tunayoishuhudia katika dini za kigeni ni kurudi katika dini zetu za asili zinazotutambua kwamba sisi ni nani na ni kwa ajili ya nani.
Tumekuwa na tunakuwa wanyonge kwa kukumbatia dini hizi zinazotunyima uhuru wa kuhoji kwani mafundisho yake yanatumia lugha tusizozielewa na zinatokana na mawazo ya watu wenye utamaduni tofauti na wetu.
Tujiuliza kama zingekuwa ni dini za kweli mbona zinabaguana na viongozi wa dini hizi wanajiona wao ni bora kuliko waumini wake.
Ukweli hata ukipingwa haubadiliki kuwa uongo. Ukweli ukishindwa ni kama umesakafiwa tu na siku moja utaibuka na waliopinga wataficha nyuso zao kwa aibu