Friday, January 25, 2008

HE! UNAFIKIRI HII NDIO NJIA SAHIHI?

Wakati wananchi wa sehemu fulani hapa Tanzania waliposikia kuwa 'gavana' ametolewa katika nafasi yake, baadhi ya wanajamii walivamia mashamba yake kilometa chache nje ya mji mkuu wa kibiashara.

Mimi kitendo hiki ninakiona ni cha kipekee kabisa, yaani mtu anapigiwa simu kuwa waende wakagawane mashamba ya fulani kwa kuwa tu huyo fulani ni fisadi! Wapi tunakwenda.

Sina hakika kama yale mwimbaji maarufu na mwanaharakati wa Marekani Tracy Chapman aliyoimba katika REVOLUTION 'mapinduzi ya watu wa chini' yanatimia.

Je!, wasiosema wameanza kusema! au wasiosikia wameanza kusikia, na nini kitafuata endapo mikononi watashika kilichokaribu yao!

Tusubiri
SAKATA LA BOT: WALIO KIMYA NAO WAMEKULA


Sidhani kama kuna yeyote mwenye uchungu na Tanzania anahitaji kuelezwa mwanzo wa mabilioni 133 yaliyotafunwa, kwa taarifa, pale kwenye benki kuu ya Tanzania. Kwa sasa kila mtu anamnyooshea mkono Ballali, gavana ambaye rais Kiwete ametengua uteuzi wake kama gavana.

Kwa maoni yangu, mimi nadhani mtu kama Ballali hawezi kuzitumbua pesa hizo peke yake hata kama angekuwa anakula kama funza. Kawaida ya funza huwa anakula na k****a wakati huo huo na ndio maana funza ni waharibifu wakubwa na mazao ya nafaka.

Hizi pesa zimeliwa na wengi, wengi tena sana ila kwa kuwa Ballali alimuonesha 'mungu' tumbo pale alipokanusha taarifa ya dk Slaa basi ndo leo umma umeamua kumuhukumu, na hakika hata kama atasafishwa vipi bado sisi tunamuona kama fisadi anayestahili kuhukumiwa na kufilisiwa kabisa na kama ndo ingekuwa katika zile nchi za kisoshalisti za kweli basi angeuawa hadjharani baada ya kuwa amewataja mafisadi wenzake.

Namtetea Ballali kuwa hizo pesa hajazila peke yake, amekula na wengi ambao wapo bado madarakani tena wanashikilia nyadhifa kubwa sana zinazowawezesha kusaini mikataba kwa niaba yetu huku wakitanguliza maslahi yao kwani hii ni kawaida yao. Tunaimba pamoja kijamaa wao wanacheza kifisadi.

Wengi waliokula wamekaa kimya huku wakijifanya hawahusiki na tena wengine bado ni 'wajumbe' wa bodi. Tunawasubiri hawa waseme kwa hiari la sivyo umma utawataka waseme wakiwa uchi
AFCON: TUNA MENGI YA KUJIFUNZA WATANZANIA


Tangu mwanzo wa mwaka huu 2008 si kwamba kila mtanzania amekuwa makini kufuatilia mashindani ya Mataifa ya Afrika yanayoendelea katika miji mbalimbali ya Ghana bali kila mtu na mpenzi wa soka duniani amekuwa makini kuna nini kinaendelea huko ambako miamba ya soka la kiafrika inakutana tangu kipite kindi cha miaka miwili ambapo Misri ilitwaa kombe hilo mbele ya 'Tembo' Ivory Coast.

Sitakuwa mchambuzi wa kuelezea mechi ambazo ndo kwanza zinaelekea katika hatua ya robo fainali bali mimi nitajaribu kujikita katika uga ambapo sisi kama watanzania tunaweza kuchota chochote kutoka Ghana.

Hakuna mtanzania ambaye anaweza kusahau namna timu yetu ya taifa ilivyoandaliwa kwa kupewa kila aina ya msaada na seriali ilivyoshindwa kushinda mechi muhimu za nyumbani na hivyo kutukosesha nafasi ya kuwakilisha nchi za jumuia ya Afika mashariki katika AFCON Ghana2008

Kikubwa ambacho ninaweza kuelezea mwanzoni kabisa ni namna ya kuthamini vipaji vya vijana wadogo bila kusahau uzoefu wa wachezaji wenye umri mkubwa lakini unaowawezesha kucheza soka. Pia nafasi ya wataalamu wa soka wazalendo katika kufanikisha mipango ya ushindi na si kushirikia na kutolewa katika hatua za mwanzo.

Tangu awasili kocha aliyetafutwa na serikali toka Brazil wengi tulikuwa na mawazo makubwa ambapo kila mtu alitazamia kabisa kuiona taifa stars ikicheza na kupata nafasi ya kwenda Ghana. Matarajio haya yalionekana kuwa kweli kutokana na namna serikali na wadau wengine walivyojitolea kuisadia timu hii ambayo mwanznoni ilionekana kama imetelekezwa.

Tatizo limejitokeza pale mtaalamu wa kibrazil alipoonesha kuwadharau watanzania akijifanya kuwa wakati alipokuja sisi hatukuwa tukijua mpira wowote na hivyo hatuwezi kumshauri katika kitu kinachoitwa soka. Kung'ang'ania kwake wachezaji chipukizi si vibaya lakini siku zote 'kijiji hakikosi wazee' lakini kuwatupa wazoefu ni tatizo kubwa. Katika safari mara zote ni lazima wawepo wanaoijua njia.

Vijana walioandaliwa vizuri tangu shuleni wana nafasi kubwa sana ya kuwa hodari katika fani nyingi, ni vizuri sasa kwa serikali na chama cha soka kuweka mikakati ili hata hiyo nafasi ya 2010 tuweze kuipata.

Ushauri wa wachezaji wazoefu, makocha wazalendo usidharauliwe. Hawa ni muhimu sana katika maendeleo ya soka letu. Tunashuhudia leo huko Ghana ambako timu nyingi zina nyota vijana wanaoungwanishwa na wakongwe.

Kwa kuwa mashindano bado yanaendelea na nzuri zaidi kwetu kuwa TVT inarusha matangazo 'live' tuna nafasi ya kujifunza mengi