Thursday, October 18, 2007

MAADHIMISHO YA KIFO CHA NYERERE

Juzi chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere kimeungana na watanzania wote kuadhimisha miaka nane tangu kufariki kwa kiongozi wa kwanza wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere. Sherehe zilikuwa nzuri na zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwamo wazri Kingunge Ngomale Mwiru aliyekuwa mgeni maalum hapa chuoni.

Yaliongewa mengi na tukaoneshwa mengi kuhusu malimu, hakuna aliyepingana nayo. Mada mbalimbali zilizoandaliwa na wahadhiri na wanafunzi zilitolewa katika maadhimisho haya yaliyofanyika kwa siku mbili. Wachangiaji mbalimbali walichangia hii yote ikiwa ni katika kuonesha kuwa kila mmoja anamtambua na kumthamini mwalimu.

Tatizo langu linakuja pale tu wale tuliowategemea kumwonesha mwalimu kama kiongozi wa watanzania wanamwonyesha kama kiongozi wa CCM. Kingunge pamoja na dhamana aliyokuja nayo ya mtumishi wa umma alishindwa kujizuia kutamba kuwa mwalimu ni wa CCM pekee na wanasiasa wanaomwiga wanafanya makosa kwani wao si wanasisisemu.

Kikubwa pia kilichonitatiza ni pale iliposemwa kuwa mwalimu alijali mali na wananchi, hapa naona ni kama tunadanganyana mchana kabisa, ni kweli kwamba mwalimu alijali wanacnhi kwa kutogawa maliasili za nchi.

Wale wanaojidai kuwa mwalimu ni wao leo tunawaona wakiongoza kwa kuuza nchi na utajiri wake, tazama mikataba mibovu inavyosainiwa kila kukicha na pia angalia jinsi mwananchi wa kawaida anavyotaabika kwa bidhaa kuwa ghali huku viongozi na watoto wao wanavyotanua kutokana na kuendekeza matumbo kuliko watu.

Si busara kumuenzi mwalimu kwa kuimba nyimbo zake huku mkicheza ngoma za ubinafsi, ufisadi na mabaya mengine mengi ambayo ni mwiba kwa watanzania, sanamu tu hazitoshi kuonesha kuwa tunamjali mwalimu bali tukumbuke kuwa mwalimu aliona na kuheshimu mali za watanzania na hakutaka kuzitumia kwa manufaa yake binafsi
HE! ETI KISWAHILI SIO LUGHA YA WASOMI!!!??


Kama kuna siku niliyoshangaa basi ni siku ya Alhamisi, tukiwa katika mjadala hapa darasani, nilizuiwa kuchangia mada kwa kuwa tu nilipaswa kuongea kiingereza. Nilikumbushwa kuwa lugha rasmi ya mawasiliano katika vyuo vya elimu ya juu ni kizungu na eti Kiswahili ambacho ni lugha ya taifa huru la Tanzania hakina nafasi kwa wasomi wasiosoma lugha hii kama somo.

Wengi walishangaa, niliamua kukaa na mwenyekiti alinionya kutoongea lugha hii tena, na hasa ninapokuwa darasani. Mwisho sana mhadhiri wa somo alisimama na kuniruhusu kuchangia mawazo yangu katika mada iliyowasilishwa na kundi la pili iliyohusu 'ulinganifu kati mitizamo ya kisiasa mmoja ukiwa ni mtazamo kongwe na mtazamo wa kisasa'

Kikubwa ninachopaswa kuwauliza ninyi wengine ni hiki, Je Kiswahili si lugha ya mawasiliano katika sehemu za elimu ya juu? au ndo nimuamini yule mzazi kule kwetu anayajua kwamba kama huwezi kuongea kizungu wewe si msomi, tena nikakumbushwa tu kuwa Kiswahili si chochote na halafu tunapaswa tujifunze Kichina
NIMERUDI TENA!!!

Mpendwa msomaji wa blogu hii, kwanza naomba uniwie radhi sana kwa kuwa kimya kwa kipindi kirefu. Nilikuwa nimebanwa na majukumu mazito ya masomo, nafurahi kwamba wanajumuia wenzangu wanaoblogu kwa Kiswahili walifanya kile ambacho wote tunahitaji, habari, taarifa, na burudani.

Kubwa zaidi kwa sasa ni kuendeleza kile wenzangu walichonacho na kama unavyojua jukumu la ukurasa huu ni kukuhabarisha na kusikia wewe unasema nini kuhusu mada mbalimbali ambazo ama ntakuwa nimezichokoza ama wewe ndo umeanzisha.

Natambua kabisa yapo mengi sana ya kujadili ambayo magazeti yetu hayana nguvu ya kuvijadili. Kuwepo kwako kutasaidia wengine kufahamu mengi na kuelemika na hivyo kujitambua.

KARIBU SANA

Tuesday, June 19, 2007

SAFARI YA GHANA INAKUJA!!!!

Hata sisi tunaweza. Ndivyo ninavyoweza kusema baada ya timu yetu ya soka inayofundishwa na Maxio Maximo kuifunga timu ngumu ya Bukinabe kwa goli 1-0 katika uwanja wa ugenini (burkinafaso).

Kwa sasa timu yetu si kichwa cha mwendawazimu kama ilivyokuwa imezoeleka hapo mwanzo. Tunaweza. Vijana wamefanya mabo makubwa ambayo kila mtanzania anayapenda. Tumepewa raha na hakuna wa kutuzuia sasa, mwendo mdundo.

Pamoja na hayo napenda kuwasikitikia baadhi ya wachezaji ambao walijiona wao ndo wao na wakawa wanaleta nyodo, sasa wanasaga meno kwani vijana wadogo wanafanya mabo amabyo wote tunayataka.

Nafurahishwa sana na msimamo wa kocha wa kutokubembeleza, huu ni mfano mzuri kwa walimu wazalendo. Tunaweza.

Unamkumbuka Kaseja pamoja na Mgosi walivyotoa maneno ya kipuuzi? yako wapi, Tunaweza bila wao kwani wapo wachezaji kibao vijana na wenye nidhamu ambao wanawajibika kwa taifa si kwa friend s of nini sijui., pumbavu. Kwa sasa wenzao wanapeta tu na jana wamepata shavu bungeni ambako kila mtu anatamani walau aingie. Cheki zawadi walizopata!

Waziri mkuu kawaahidi mambo makubwa sana endapo wataenda Ghana, na nyumba nazo hizo zinakuja yaani kutakuwa na mtaa wa Maksimo. Kitakuwa ni kijiji cha utalii, nami nitatembelea na kupiga picha.

Tunaweza
SAFARI YA GHANA INAKUJA!!!!

Hata sisi tunaweza. Ndivyo ninavyoweza kusema baada ya timu yetu ya soka inayofundishwa na Maxio Maximo kuifunga timu ngumu ya Bukinabe kwa goli 1-0 katika uwanja wa ugenini (burkinafaso).

Kwa sasa timu yetu si kichwa cha mwendawazimu kama ilivyokuwa imezoeleka hapo mwanzo. Tunaweza. Vijana wamefanya mabo makubwa ambayo kila mtanzania anayapenda. Tumepewa raha na hakuna wa kutuzuia sasa, mwendo mdundo.

Pamoja na hayo napenda kuwasikitikia baadhi ya wachezaji ambao walijiona wao ndo wao na wakawa wanaleta nyodo, sasa wanasaga meno kwani vijana wadogo wanafanya mabo amabyo wote tunayataka.

Nafurahishwa sana na msimamo wa kocha wa kutokubembeleza, huu ni mfano mzuri kwa walimu wazalendo. Tunaweza.

Unamkumbuka Kaseja pamoja na Mgosi walivyotoa maneno ya kipuuzi? yako wapi, Tunaweza bila wao kwani wapo wachezaji kibao vijana na wenye nidhamu ambao wanawajibika kwa taifa si kwa friend s of nini sijui., pumbavu. Kwa sasa wenzao wanapeta tu na jana wamepata shavu bungeni ambako kila mtu anatamani walau aingie. Cheki zawadi walizopata!

Waziri mkuu kawaahidi mambo makubwa sana endapo wataenda Ghana, na nyumba nazo hizo zinakuja yaani kutakuwa na mtaa wa Maksimo. Kitakuwa ni kijiji cha utalii, nami nitatembelea na kupiga picha.

Tunaweza

Saturday, June 16, 2007

NIPO NDANI YA NYUMBA

Wasomaji wangu kwanza kabisa ningependa kuwaomba samahani kwa kupotea ghafla, nilibanwa na masomo na mitihani ilikuwa inakuja wanguwangu. Sio neno kwa sasa nipo mapumziko na najua tutakuwa pamoja katika kujadili mambo ya utamaduni, siasa na uchumi bila kujali yale yote yanayojiri na kuhusisha maisha yetu

Sunday, April 29, 2007

SIMBA NI KIBOKO

Katika ligi ndogo ya soka inayoendelea Tanzania timu ya Simba ndiyo klabu pekee ambayo kipa wake Mustafa ndiye kipa pekee ambaye hajaokota mpra katika nyavu anayoilinda ukiacha magoli ya 'TFF' waliyopewa timu ya Ashanti

Kwa utendaji huu wa tiefuefu nadhani kazi bado ipo kwani hakuna haja ya wao kama chama cha soka kufanya kazi kwa ushabiki tena katika ligi hii ndogo ammbayo haina mwenyeji wala mgeni. Kumfungia mechi sita Golota kwa upande wangu si halali kwani kosa moja katika soka haliwezi kuzaa adhabu kubwa namna hiyo
CHESII YAKARIBIA FAINALI YA UEFA

Klabu bingwa ya soka Uingereza majuzi iliweza kuilaza timu ya livapuli kwa bao moja bila majibu katika uwanja wake wa nyumbani Stamford Bridge.

Bao hilo lilifungwa na winga teleza Joe Cole baada ya kupata pande safi kutoka kwa mwanasoka bora wa Afrika na nyota anayeongoza kwa kupachika mabao katika primia ligi Didier Drogba.

Hii ni hatua kubwa sana katika kuelekea finali na endapo jumanne katika mechi ya marudiano chesii watashinda basi ndoto za Mourhino ya kutwaa kombe zitatimia.

Kumbuka kuwa nyota wa Ghana Michael Essien atacheza katika mechi hii japo kuna shaka ya mlinzi 'kavalo' amabye aliumia wakati wa sare ya ligi dhidi ya Bolton jana

Wednesday, April 18, 2007

CHEKA KIDOGOOOOO!!!

Nimetumiwa na rafiki yangu si vibaya nawe ukasoma( hakuna ubaguzi)


Kuna muhindi mmoja alivamiwa na majambazi kwa bahati akawahi kujificha darini yeye na mkewe kwa kuogopa kuuwawa. Sasa wakawa wanamtaka ashuke la sivyo watavunja kila kitu ndani.

Mhindi akajibu: " Kama tavunja mavitu tanunua mengine lakini hapana shuka

Jambazi: Shuka la sivyoo tutachukuwa pesa zako zote
Mhindi: Kama machukua pesa tapata mengine toka Bombei

Jamabazi: Shuka kama utaki tutauwa watoto wako hapa chini !
Mhindi: Kama mauwa matoto hapana tabu tategneza mengine mashine yote bili iko juu hapa (YEYE NA MKEWE)

UMEYAONA MABANGO WALIYOBEBA WASOMI WA UDSM WALIOSIMAMISHWA!!!!

Nimeingia katika blog ya Michuzi na kujionea mabango ambayo wanafunzi wa mwaka wa kwanza udsm waliandika wakishinikiza mkopo uwe 100%. Tazama hapa pembeni kushoto na bonyeza Michuzi, utajionea picha mbalimbali zilizopigwa kwa uzuri kabisa na gwiji la blog za picha nchini. Baadhi ya mabango hayo yanasema:-

SERIKALI PUNGUZENI SIASA KATIKA MASUALA YA MSINGI MNAUA ELIMU

KIKWETE UMESOMA BURE LEO UNATUDAI40%

KIKWETE BAADA YA WAKULIMA KUKUCHAGUA NDIVYO UNAVYOWALIPA

NASI TUUNDIWE KAMATI KAMA YA MALIMA NA MENGI halafu tupewe Milioni 100

Yapo mengi lakini haya ndo yamenivutia

MGOMO WA CHUO KIKUU, NANI ANAFAIDIKA!!!

Katika kikao chake maalum cha 172 kilichofanyika tarehe 17 april,2007 Baraza la chuo kikuu cha dar es salaam kiliamua kuwasimamisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma udsm pamoja na vyuo vishiriki kwa kushiriki katika mgomo'haramu' wa kupinga malipo ya 40%.Wanafunzi hawa wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana.

Serikali makini hutumia rasilimali zake katika kuhakikisha kuwa inajenga na kuelimisha vijana ili waweze kuwa na manufaa kwa jamii na serikali yote. Vijana huandaliwa kuja kuwa watu makini na maandalizi haya yana gharama zake amabazo wakati mwingine kama mtu binafsi hawezi kuzibeba na kukidhi gharama hizi.

Nchi zetu nyingi za kiafrika zimekumbatiwa na umaskini ambao si wa mali wala watu bali umaskini wa mawazo ya kupanga nini kipewe kipaumbele kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kesho na si kujineemesha leo na kutaka sifa sizo maana.

Serikali zetu nyingi zimekuwa zikitenga fungu kubwa sana kwa ajili ya ulinzi na IKULU huku sekta nyingine zikipewa kiduchu. Sipingani na kutoa vingi kwa ajili ya ulinzi lakini nashindwa kujizuia kujiuliza kwamba sisi Tanzania adui yetu ni nani na kwanini IKULU itumie pesa nyingi saaaana kwa kipindi kifupi!?

hakuna kitu muhimu kama elimu, haijalishi kama ni elimu ya kujitambua ama ni elimu ya kukariri ili upate cheti huku ukishindwa kujitambua. Kujitambua mara zote huanzisha safari moja.

Siwaungi mkono waliogoma kwani naamini kabisa kuna njia nyingine ambazo wangechukua ili kupata haki yao (ambayo hata mimi ninaihitaji). Wengi wa wanafunzi(nikiwamo mimi) tunatoka vijijini na nauli yakutufikisha chuoni hubidi upitishwe mchango, sasa serikali inapotoa mkopo ambao haukidhi mahitaji na bado haikubali kuwa ndani ya nchi kuna matabaka hivyo wengine wanapaswa kupewa zaidi ya wengine na wengine kunyimwa kabisa(hebu wafikirie watoto wa vigogo ambao wamesoma shule za kulipa mamilioni ambao nao wazazi wao wanataka wapewe pesa zinazotustahili makabwela!)

Suala la matumizi ya anasa ya baadhi ya ofisi za umma na watendaji wa umma linachangia sana katika kutengwa kwa vitu muhimu vya kutimizwa.

Najua watu wengi wnawalaumu wanafunzi wa udsm kwa mgomo, lakini kujitambua ni hatua kubwa katika maendeleo hata kama namna ya kuyaleta itaumiza.

Ni lazima kuwepo na vipaumbele katika vitu muhimu hasa suala la elimu ya juu na ya ufundi ili kujenga taifa endelevu. Masuala ya baadhi ya ofisi kutumia pesa za walalahoi kwa ajili ya manufaa yao hayafai katika nchi hii. Tubadilike na tujitambue huku tukiweka ubinafsi, unafiki na ubabzazi pembeni ili tuendelee mbele. Mgomo ulisitahili na mkopo ni budi utolewe kwa wahitaji kwa 100%

Wednesday, April 11, 2007

PASAKA BILA PILAU LA NG'OMBE!!!

Kama kuna sherehe ambayo iliwaweka watu wote katika mstari basi ni hii ya pasaka ya mwaka huu. Yaani ilikuwa ni mchicha na kuku kwenda mbele kisa ni RVF.

Thursday, April 05, 2007

JE, DINI NA MUNGU WA WAAFRIKA NI MSHENZI?
Na: Obe Mashauri

Habari hii niliiandika mwaka 2003 na ilitoka katika gazeti la Uhuru, ilihaririwa sana. Nimeona nikupatie uisome kama nilivyokuwa nimeiandika

Ni falsafa ya uongo kwa mtu kuamini kwamba waafrika hawakuwa na dini kabla ya kuja kwa wageni waliokuja kwa nia ya kupora utajiri wa bara hili.
Dini ni njia ya kuhusiana na Mungu. Kwa tafsiri hii ni uongo wenye kutu kusema kwamba kabla ya wazungu na waarabu kutuvamia tulikuwa watu wasio na diniau kwa lugha nzuri kwao nakwa wafuasi wao wa sasa, wapagani au makafiri.
Wengi wetu tumekuwa tukiamini kwa kuaminishwa kwamba dini zilizoletwa na wageni ndiyo dini za asili.ukoloni na utumwa wa maharamia hawa ulitufanya tuamini kwamba Mungu wa majangiri hawa ni wa kweli. Mungu aliyeabudiwa na wenyeji aliitwa mshenzi na mitume wake wakaitwa mapepo. Huu ndio ustaarabu wa wageni.
Baada ya kuwa zimejikita afrika kwa mabavu na propaganda, zimewajaza wafuasi wake falsafa mpya ya kujibagua na kujiona bora zaidi ya wengine
Tanzania na afrika kwa ujumla katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudia vujo na migogoro mikubwa ya kidini inayoletwa na dini hizi za ukristo na uislam katika ama kujitanua au kujiona bora zaidi ya nyingine.
Mbaya zaidi migogoro baini ya dini hizi inawaathiri hata wasiozifuata. Mambo haya hayakuwahi kutokea kutoea kabla ya kuja kwa dini hizi za kigeni.
Historia ni shahidi wa mengi. Historia ya mwafrika haioneshi machafuko au vita vilivyosababishwa na dini za asili. Dini ambazo ‘wakoloni na mabwana’ waliziita za kishenzi huku waumini wake wakibatizwa majina kama wapagani,kaffir na majina mengine mengi ya kipuuzi.
Ukristo na uislamu ni dini za kibiashara zenye historia ya vita katika kujitanua. Itkadi ya dini hizi ilisambazwa kwa heri au shari kwao waliozikataa. Walikuwa wakimtangaza Mungu wao kwamba ndiye wa kweli na hapana mwingine ila yeye.
Ukristo na uislam uliokumbatiwa na waafrika uliletwa afrika si kwa minajili ya kumtangaza mungu wa kweli bali dini hizi zilikuwa ni mbinu za wazungu na waarabu kujitanua kiuchumi na kisisasa katika bara hili tukufu. Biashara ya utumwa na ukoloni vinadhihirisha haya.
Kwa mantiki hii utaona kwamba mungu anayehubiriwa katika dini hizi ni yule anayehalalisha uporaji na uuwaji wa watu wasiomtaka.
Uislamu ulisambazwa kwa upanga mkali uliokata shingo na viungo kwa wote walioukataa. Jitihada zilizofanywa na uthman dan fodio zinadhihirisha jambo hili.
Mabomu,mishale, risasi na uongo nazo zilitumika kuusimika ukristo na yule aliyeukataa aliitwa msaliti, kifo ni zawai yake.
Mtu aliyepingana na dini hizi aliuawa.
Falsafa iliyopandikizwa na wakristo na waislam vichwani mwa waafrika bado inatutawala mpaka sasa. Ukweli ni kwamba kila mtu ana Mungu wake anayeujua utamaduni wake na kila hali yake ya maisha ya kila siku.
Kwa waafrika Mungu huyu alijulikana kwa majina anuai, wapo waliomwita Ngai, Mulungu, Lyoka na majina mengine mengi yanayoonyesha utukufu wake.
Dini za kiafrika ziliabudu Mungu mmoja tu na si kwamba wageni ndio waliowaletea waafrika dini na kuwatambulisha kwa Mungu. Ustaarabu ulikuwapo afrika na wazungu na waarabu ndio waliokopi ustaarabu huu.
Dini za kigeni ziliudharau utamaduni wa mwafrika na kumtambulisha kwa utamaduni mpya wa kujidharau na kudharau kila kilicho chake, akiiponda dini yake na kukumbatia ukisasa eti huo ndio ustaarabu.
Kwa kuudharau utamaduni wake mwaafrika amekuwa kama kasuku, kazi yake ni kuimba kila anachopewa na bwana wake. Lugha za kiafrika karibuni zitatoweka kwa kuwa tu hazina nafasi katika dunia ya wastaarabu. Lugha muhimu ni kizungu na kiarabu tu.
Ukitaka kumtawala mtu basi mporeulimi wake. Majangiri hawa wamefanikiwa kwa hilo. Kwani kila mtu hata kuamini ukisema umetokewa na Mungu anayeongea lugha yako. Wao Mungu ni yule anayeongea kwa lugha zao,Mungu asyeongea lugha zao basi watamwita shetani kama ilivyotokea Joan of the Arc huko London. Kitabu cha the African civilization kinalieleza hili.
Mwanzoni mwa muongo huu watanzania tumekuwa tukishuhudia migogoro na fujo nyingi za kidini zikitokea na ukijaribu kuchunguza kwa umakini migongano hii imekalia katika maslahi binafsi ya dini hizi na si kumtangaza mungu wao.
Machafuko haya yanayotokea ndiyo yanayonifanya nijiulize kama kweli dini zetu zilikuwa za kishenzi?
Hivi matusi, vita, migongano na machafuko yanayotokea katika nyumba za ibadandio ustaarabu tulioletewa?
Hivi wageni hawa walituletea Mungu tuliyemjua sisi au mungu wao mpenda vita, mwenye wivuna mbaguzi? Je, ni kweli kwamba sisis hatukuwa na Mungu? Swali hili nisingependa waljibu wasomi waliokaririshwa kwamba cha mzungu na mwarabu ndio bora
Kama tusingekuwa na Mungu ‘wastaarabu’ hawa wangetukuta kweli? Moyo wa ukarimu tuliowaonyesha japo walitutemea mate, ulitoka kwa Mungu wa kishenzi kweli? Hivi Mungu wetu aliyetulinda na kutupa akili ya kumjua alikuwa ni Mungu aliyevaa ngozi ya kondoo.
Je, mungu aliyeruhusu wengine kupora,kutawala kwa mabavu na kuuza binaadamu kama bidhaa ndiye mungu wa kweli?
Maswali haya pamoja na hili linalosema kwamba ukristo na uislam ni dini za ulimwengu (universal) yananifanya nijiulize na kuchoshwa na hadithi za vitabuni.
Ukweli usiolazimishwa kuukubali ni kwamba dini hizi mbili si dini za ulimwengu kama tunavyopotoshwa. Kwa afrika dini hizi ni ngeni kabisa na hatukuwa na migogoro ya kidini kama tunayoishuhudia sasa katika dini hizi ngeni.
Ni wakati wa waafrika sasa kurejea katika imani ya asili tuliyokuwa nayo, imani inayotutambua sisi na utamaduni wetu. Turudi katika dini zetu ili tutunze ustaarabu wetu, utamaduni wetukila fahari yetu.
Dini zetu za jadi ndizo zitakazotuepusha na migogoro tunayoishuhudia sasa na kwa bahati mbaya sana tunaishiriki tu eti kwa kuwa tumebatizwa na kusilimishwa katika majina mapya tusiyojua maana yake.
Vilevile tujue dini hizi mwanzo wake na wafuasi wake wa mwanzo. Ukristo ulianzishwa na kikundi cha waalimu (rabbi) Yesu akiwa mwanzilisha wakati Uislamu ulianzishwa na mfanyabiashara aliyeitwa Muhamad aliyejiita mtume huko mashariki ya mbali na kuusambaza kwa vita akianzia huko Makka.
Kuzifuata na kuzikubali dini hizi ni kukubaliana na waanzilishi wa dini hiziz na misemo yao kama…ya kaisari mpe kaisari…., na bakora ndizo zitakazoleta usuluhishi kati yetu!
Kukataa kurudia dini zetu ni kukumbatia laana tulizopata kwa kuaminishwa kwamba waafrika hatuna Mungu
Ufumbuzi wa migogoro tunayoishuhudia katika dini za kigeni ni kurudi katika dini zetu za asili zinazotutambua kwamba sisi ni nani na ni kwa ajili ya nani.
Tumekuwa na tunakuwa wanyonge kwa kukumbatia dini hizi zinazotunyima uhuru wa kuhoji kwani mafundisho yake yanatumia lugha tusizozielewa na zinatokana na mawazo ya watu wenye utamaduni tofauti na wetu.
Tujiuliza kama zingekuwa ni dini za kweli mbona zinabaguana na viongozi wa dini hizi wanajiona wao ni bora kuliko waumini wake.
Ukweli hata ukipingwa haubadiliki kuwa uongo. Ukweli ukishindwa ni kama umesakafiwa tu na siku moja utaibuka na waliopinga wataficha nyuso zao kwa aibu

Monday, April 02, 2007

SULUHU KAMA USHINDI VILE......

Lilikuwa ni bao la kusawazisha liliofungwa kipindi cha pili muda wa lala salam ndilo lililobadilisha matokeo na kuiokoa timu ya chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere isiadhirishwe na chuo cha ustawi- Kijitonyama.

Mechi hiyo iliyofanyika katika uwanja wa MNMA ilishuhudia timu ya MNMA ikiwa ya kwanza kupachika bao lililofungwa na mshambuliaji mahiri Magesa dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza na hivyo kuamsha ari kwa wachezaji na washangiliaji waliokuwa wamejazana kwa wingi kuisapoti timu yao ambayo haina rekodi nzuri ya kushinda mechi inazocheza katika uwanja wake wa nyumbani.

Hatahivyo Ustawi walisawazisha kabla ya mapumziko. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Ustawi wakifunga bao 'tamu' la luninga lililofungwa na mshambuliaji mwenye jezi namba9mgongoni. Bao hili liliwachanganya wachezaji na mashabiki pia huku wakijikuta wakirejea kumbukumbu za timu ya taifa kufungwa na simba wa teranga. Lakini alikuwa ni Marijani aliyefuta ndoto za wageni kuongoza baada ya kusawazisha goli baada ya kupokea pasi safi toka kwa winga mahiri Joshua 'basopa'.

Mpira huu ulioshuhudia kazi kubwa kati ya mshambuliaji wa Ustawi na beki wa pembeni wa MNMA Allain, ulitawalaliwa na rafu za kimchezo huku mwamuzi akijitahidi kuumudu mchezo. Ustawi walipata bao la tatu baada ya kiungo mchezaji jezi namba14 alipounganisha krosi safi toka winga ya kushoto. Lakini ni Ayub Denge maarufu kama Jobe ndiye alieleta faraja kubwa kwa MNMA baada ya kufunga bao la shuti lililomshinda kipa wa Ustawi na kuleta furaha kubwa kwa mashabiki wa MNMA.

Hadi mwisho wa mchezo timu zote zilitoka nguvu sawa. Baada ya pasaka timu ya MNMA inataraji kucheza na timu ya IFM

Timu ya MNMA iliwakilishwa na
1 SWEDI
2 Allen (
3 Maximilian
4 MUDI
5 Father
6 RASHIDI
7 Baseke
8 Mungai
9 Hamad (Marijani)
10. Jobe
11 Magesa(Joshua)
RVF: KILA MMOJA ANAJIDAI ETI YE'VEJETARIANI'

Homa inayoogopwa kabisa kwa sasa imeingia dar. Inaogopwa kwa sababu inapatikana katika kitoweo tena kitoweo chenyewe kikiwa ni nyama ya ng'ombe. Homa hii kitaalamu imepewa jina la Rift Valley Fever ama kwa kiswahili homa ya bonde la ufa.

Hapa chuoni kwa sasa kila mtu amejipachika 'urasi' kwamba yeye si mtu wa nyama bali ni matunda na mboga za majani. Ukienda kafteria chakula kinacholiwa sana ni ugali ama wali na mbogamboga ambazo hata hivyo zimepikiwa mafuta ya wanyama.

Labda tueleweshwe zaidi kuhusu hii homa, hivi haya mafuta ya wanyama hayana HBU

Wednesday, March 28, 2007

KILA MTU NI MPIGADEBE!!

Unapotembelea vituo vya mabasi na ama unapotaka kusafiri si ajabu kufuatwa na vijana wa rika la kati wakijitahidi kukushawishi kupanda magari yao, hawa ndio wapigadebe.

Sitaki ujenge picha ya hawa, lakini katika hali ya sasa hivi kila mtu amekuwa ni mpigadebe, sijui tunakwenda wapi. Kuanzia rais mpaka wenye NGO wote wanapigadebe sema kinachotofautiana ni sehemu, namna na mahali pa kupigia debe. hata wenye blog ni wapigadebe
KANISA LILISHIRIKI UTUMWA!!!

Niliyofundishwa kwamba walipokuja wamisionari hawakuja kufundisha juu ya Mungu, walikuja kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kwamba wazungu wanapata watumwa kwa namna yoyote ile. Walikuja wakiwa wameshika baibo na wakakiri kabisa kwamba wao ni wema na mungu wao anaruhusu utumwa.

Usishangae! Majuzi kanisa la Angilikana limekubali na kusikitishwa na kitendo chake cha kushiriki katika biashara 'haramu kwa kipindi hiki' halali ya utumwa kwa kipindi kile. Akiongea mjini Landani jumamosi wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka200 tangu bunge la Uingereza lilipopitisha sheria ya kuzuia biashara na utumwa wenyewe, askofu mkuu wa canterbury daktari Rowan Williams alisema kwamba kanisa linasikitishwa na hali ile na linapanga kulipa fidia.

Swali, Watamlipa nani

Wednesday, March 21, 2007

NINI KINAMBEBA 'MTOTO WA MJINI'!!!

Unaikumbuka ile kesi ya wale jamaa waliomuua wakili Kapinga mnamo mwaka2002! Jamaa hawa walikaa rumande kwa muda wa miaka5 na hukumu ya kesi ilitaja kuwa walikuwa wakituhumiwa kumuua wakili huyo maarufu. Hawa hawakuonwa. Dito kaua hadharana na bado kamanda wa polisi anajaribu kutuaminisha kuwa bastola ilivyatuka kwa bahati mbaya! Amefanikiwa kwani mapema tu DPP aliibadili kesi toka mauaji mpaka kukusudia kuua.

Mahabusu wengi wenye kesi za namna ya 'mtoto wa mjini' wamekaa rumande kwa muda mrefu sana kwa kuwa tu 'upelelezi haujakamilika' (hawa si matajiri) jiulize jamaa waliotuhumiwa kumuua Kapinga hawakuona na yeyote lakini mahakama imewahukumu hukumu nzito kabisa. Dito, hadharani kabisa katoka ndani ya shangingi lake kashika bastola na kuifyatua ikimlenga dereva bado tunaambiwa eti hakukusudia kuua! Tunakokwenda siko.

Jiulize waziri mmoja anasimama na kusema kuwa kesi ya kigogo huyo imekuwa hivyo kwa sababu ana mawakili wazuri! mawakili wazuri ama kuna kitu kingine kilichoanzia kwa Tibaigana, mkurugenzi wa mashtaka na 'serikali'

Tunakokwenda siko na itafikia wakati wenye kutosikia watasikia na mabubu watasema, nimalize kwa kukumegea kipande ambacho mwanamuziki na mwanaharakati Tracy Chapman anasema katika wimbo wake 'Revolution'. Utafute na uusikilize utapata zaidi ya sauti nzuri na milio murua ya magitaa (mara nyingi hutumia gitaa tu)

Saturday, March 17, 2007

YA DITO, NDUGU ZAKE, DHAMANA NA MAHAKIMU!!!

Juma hili linamalizika huku mawaziri wanaohusika na usalama na haki za raia wakishindwa kuwashawishi mahabusu amabo wamekuwa wakigoma sasa mpaka nao kesi zinazowakabili mahakama zitasikilizwa kwa haraka kama ilivyotokea kwa mtuhumiwa wa kesi ya kukusudia kuua ndugu Ditto amabye kesi yake imechukua miezi mitatu tu na sasa yupo nje kwa dhamana kwani kosa lake lina dhaminika ilhali mahabusu wengi wakiwa gerezani kwa takribani miaka10 mpaka 15 kesi zao zikitajwa tu bila chochote kuendelea.

Wamegoma!

Nawashangaa sana hawa mahabusu amabo wameamua kugoma ili kushinikiza kesi zao ziharakishwe kama inavyotokea kwa kesi zinazowakabili vigogo ama watoto wao ama watu maarufu. Kesi zinatofautiana na watuhumiwa wanatofautiana sana kwani hata binadamu wote si sawa japo katiba yetu inayoongozwa na mfumo wa ujamaa kutamka kuwa binadamu wote ni sawa.

Kesi inayoendelea ya mheshimiwa inadhihirisha yale G. Orwell aliyosema katika kitabu chake maarufu kinachoitwa 'the animal farm' shamba la wanyama kuwa kuna binadamu wengine ni zaidi ya wengine.

ninakuwa ninajiuliza kuwa inawezekana ni mfumo wetu wa sheria una macho ama watendaji wenye dhamana ndio wanaoangalia na kuifanya sheria kuwa na macho na kuipotezea imani yake kuwa sheria ni msumeno!

Nimemshangaa jaji mkuu amabye ameshangazwa na kitendo cha wasalama kumpitisha kigogo katika mlango unaotumiwa na mahakimu, hivi hajui kuwa watuhumiwa wengine ni mahakimu tayari, kwenda mahakamani kwao ni kama kuwazuga tu na ndiyo maana wakati wanaogoma wanarundikwa kwenye makarandinga wao wanaletwa na taksi amabyo inalindwa na polisi wenye silaha ili kutotota nafasi kwa 'washenzi' kutotoa habari kwa umma.

Najiuliza wale ndugu wa mtuhumiwa waliowafanyia uhuni wapigapicha wa habari corparation walikuwa wanajua kuwa ni lazima ndugu yao atapewa dhamana! Hivi kama hakimu angekataza dhamana nani angeshambuliwa na ndugu hawa amabo mahakama waliifanya kama sehemu ambako mwali anatolewa kwa kwenda na kanga huku walinzi wa usalama wakiwaangalia kana kwamba wanachofanya kinaruhusiwa.

Ingekuwa ni 'kapuku' kweli angeruhusiwa kwenda hata na 'leso' ikiwa tu simu ya kapuku ikiita basi hima askari atakufuata na kukugombeza huku hakimu akitishia kukuadhibu kwa kuleta kelele kortini.

Sheria haina macho lakini waliodhaminiwa na wanachi kuitunza na kuiimarisha wamekuwa wabaguzi huku vigogo wakikrimiwa na walalahoi wakinyanyaswa hata kwa kufanya mepesi dhidi ya mazito yanayofanywa na vigogo
ETI TIMU YA MNMA KAMA 'ASENO'

Ni jana tu ambapo wanachuo walishuhudia timu yao ya mpira wa miguu ikicheza na timu ya vijana wa mtaani wanaojulikana kama 'nantes' timu ambayo mfadhili wake mkuu inaaminiwa ni mhasibu wa chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere ndugu Magulumengi.

Ikicheza kitimu timu ya chuo ilikukuwa ya kwanza kuliona lango la wapinzani wao kupitia kwa mfungaji wake makini Magesa aliyefunga bao tamu baada ya kupata pasi safi toka kwa kiungo mfungaji Marijani.

Bao hilo liliwafanya wageni wachanganyikiwe huku kiungo wa nantes Dinno akihangaika kuipita ngome ya chuo iliyokuwa chini ya ulinzi wa dogo Allan. Hadi kipindi cha kwanza kinakwisha chuo walikuwa wakiongoza kwa goli moja.

Kipindi cha pili timu ya wageni ilifanya mabadiliko yaliyosaidia kupatikana kwa goli la kusawazisha lililofungwa dakika 20 baada ya kipindi cha pili. Bao hili liliwaduwaza chuo na kujikuta wakicheza bila mpangilio na mabeki wakicheza faulo zilizosababisha chuo kufungwa goli la pili. faulo iliyopigwa dakika za majeruhi pembeni mwa lango la timu ya chuo ilizaa goli lililowaduwaza wachezaji na mashabiki wa chuo kwani licha ya kuwa timu yao ilifungwa bali lilimaanisha uteja wa kudumu kwani tangu 2005 timu ya chuo haijawahi kuwafunga vijana wa nantes ambao huongozwa na kapteni mwenye maneno mengi Ben Shoo.

Pamoja na mabdiliko makubwa yaliyofanywa na chuo ya kuwaingizi Chidi, Munga na seki timu ya chuo ililala na kumwacha mshabiki ambaye hujifanya kocha hanzuruni akiapa kutoshangilia tena timu ambayo haina dhamana.

Mashabiki walioongea na mwandishi wa blog hii walionekana kukerwa na kufungwa huku na wakaifananisha timu yao kama timu ya aseno ambayo mbali na kucheza mpira na kuumiliki kwa muda mrefu alkini wamejikuta hawana chao msimu huu.

Wednesday, March 14, 2007

NIPO NDANI YA MCHEZO!

Msomaji wangu tegemea kitu adimu toka katika blog hii, kinakuja

Thursday, March 08, 2007

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI!
JAMII IWAANGALIE WANAWAKE WAJAWAZITO!!!

Nimeamua kuandika waraka huu nia kubwa ikiwa ni kutaka kukuonesha wewe msomaji adha wanayoipata wanawake wengi wa Kitanzania hasa wanapokuwa wajawazito. Wanawake wajawazito hasa wale wa vijijini wanapata wakati mgumu sana na unaoogopesha pindi wanapokuwa wakifuata huduma ya 'kujifungua' katika hospitali za serikali.

Hospitali nyingi za serikali zimekuwa si rafiki wa wajawazito hasa wale wanaotoka vijijini ambako umaskini humsabahi kila mtu katika nchi hii inayohubiri maisha bora kwa kila mtanzania. Wanapofika hospitali wanalazimika kununua mahitaji ya kupatiwa huduma ilhali serikali imetangaza kuwa 'vifaa' hivi hupatikana bure kwa wote, hii si kweli.

Wanahitajika kujinunulia vifaa hivi ambavyo kwao ni ghali sana na wengine huamua kabisa kuacha kwenda hospitali kwani masaibu watakayokutana nayo huko yanatisha.

Kuna baadhi ya hospitali, tena nyingine zipo mijini kabisa kina mama wajawazito wamekuwa wakirundikwa wodini kama magunia ya viazi, huku kitanda kimoja kikilaliwa na wajawazito wawili 'wenye bahati' na wasiona bahati basi wasubiri saa katika sakafu.
Ni serikali yenye jukumu la kuhakikisha kuwa hospitali zake zina si huduma bora na vifaa tu bali wahudumu wapo wa kutosha na wanaowezestoa huduma kwa kila mmoja bila kujali hali ya kipato chake.

Leo tunapoungana na wanawake kushehereke siku yao duniani ni jukumu la kila mwanajamii na serikali kujiuliza wanawake wajawazito wanasaidiwa vipi
PONGEZI ZANGU KWA MAMA KATIKA SIKUKUU YA WANAWAKE DUNIANI!!!

Mama, mwanao nakuandikia waraka huu mfupi kwa ajili ya kukupongeza na kukushukuru kwa yote uliyofanya na unaendelea kuyafanya nia kubwa ikiwa ni kuhakikisha kuwa mwanao ninakuwa 'huru'. Mama, leo unaungana na wanawake wengi duniani kusheherekea siku hii nzuri na inayoheshimiwa na kila mwanadamu. Nakupongeza mama yangu kwa kuwa makini katika kuhakikisha ninakuwa na ustawi ulio mzuri na wenye maisha mazuri.

Nina mengi ya kukuandikia kuonyesha furaha yangu wakati unaungana na wenzako katika siku hii muhimu, sitaki nikuchoshe ila tu tambua ya kuwa u mwanamke bora zaidi na unastahili yote jamii inayoweza kutoa kwa ajili ya ustawi wako ambao unamaanisha ustawi wa jamii nzima.
Hongera mama
LEO NI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI!!!!

Wanawake duniani kote leo tarehe 8mwezi wa 3 wanaungana wote duniani kutambua siku yao. Jamii nyingi duniani zinawachukulia wanawake kama binadamu wa 'pili' huku wanaume wakiwa ni wa kwanza bila kujali mchango mkubwa unaoletwa na wanawake katika suala zima la kuleta maendeleo kwa taifa na familia kwa ujumla.

wanawake ni muhimu sana kwa taifa kwani ukiachana na jukumu lao kubwa la kuongeza 'wanachama' katika taifa, wamekuwa ni mstari wa mbela katika kujenga jamii bora kabisa kwa kujenga misingi imara ya tabia za watoto na hivyo kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya jamii.

Jamii zetu kwa sasa zimebadilika sana katika suala la kumtambua na kumthamini mwanamke, hapo zamani mwanamke alikuwa anabaguliwa na familia katika suala zima la elimu lakini kwa sasa hali ni tofauti kwa uwezo wao mkubwa darasani na mawazo yao endelevu vimechangia kujenga misingi madhubuti katika nyanja ya elimu. Kwa nchi kama tanzania, wasichana miaka miwili mfululizo wamekuwa wakiongoza katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na sita. Hii imeongeza changamoto kwa jamii kuona kuwa mtoto wa kike anafaa sana kusomeshwa na kama ule usemi wa msomi maarufu unaosema 'kumwelimisha mwanamke ni kuelimisha jamii' unatimia

Wednesday, March 07, 2007

ETI KIKWETE ANASAFIRI SANA!!!!!!!

Ni majuzi tu rais wetu mpendwa na ambaye pia ni mwenyekiti wa chama chetu kinachodumu amerejea kutoka safari ambazo sasa zimekuwa ni za kawaida kwake. Inawezekana watu wanaolaum safari hizi hawajui kuwa huyu aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje! Wewe unaonaje, unadhani hajasahau kuwa cheo sasa ni kipya?
HATA BLOG HII INABADILIKA!!!!

Msomaji wa machweo, nimekuwa nikikuandikia kuhusu mabadiliko makubwa yanayoendelea hapa chuoni ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya jina la chuo cha kumbukumbu ya nyerere mpaka kuteuliwa kwa viongozi wa kuongoza chuo na kubwa zaidi maktaba ya kompyuta kuanza kutumika.

Kwa mabadiliko haya, nami pamoja na waandaaji wa blog hii tunajipanga ili kuiboresha blog hii ivutie na pia kuongeza 'utamu' kwako msomaji.

Kwa sasa unapofungua blog pembeni utaona viunganishi ambapo utaweza kutembelea blog nyingine za kiswahili ikiwemo ya Ndesanjo, Mkina, Ngurumo na ile ya katuni za Kipanya.

Mengi yanakuja nami nawaahidi kuwapa kile mnachoona kinafaa, tafadhari msisite kutuma maoni yenu katika blog hii

Friday, March 02, 2007

NI MABADILIKO TU KILA KONA, UMEYAONA MASHANGINGI...

Leo imekuwa ni siku njema na ya furaha sana kwa walioteuliwa kushika nyadhifa hapa chuoni, kama huna habari ya uteuzi huu ngoja nikupashe kidogo. Juma lililopita bodi ya chuo chini ya m/kiti dr Salim A. Salim iliwateua ndugu Mushi na ndugu Luambano kushika nyadhifa za juu kabisa hapa chuoni, Mushi aliteuliwa kuwa naibu wa mkuu wa chuo na Luambano kuwa msajiri wa chuo, hii imekuwa ni habari njema kwao.

Licha ya uteuzi kumaanisha 'posho' kuongezeka na majukumu tele lakini uteuzi huo umeendana na kuletwa kwa 'mashangingi' magari mazuri ya kifahari (sema ya anasa) ili kurahisisha utendaji kazi wa vionngozi hawa.

Jumuia tumeombwa kutoa ushirikiano kwao lakini hatujaona sehemu wao walipoombwa kutoa ushirikiano kwetu, labda tutapata lifti! Tusubiri tuone
WAMESIKIA KILIO CHETU, SASA TUPO MTANDAONI!!!!!

Niliwahi kukuandikeni kuhusu kutokuwapo kwa huduma ya kisasa ya intanet hapa katika chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere, kwa sasa hii leo inaweza kuwa ni historia kwani kwa muda huu ninapokuandikia nimo ndani ya chumba ambacho zamani kilikuwa kimefungwa kwa makufuri makubwa ya solex na milango ya vyuma yakihifadhi kompyuta, ninakuandikia habari hii huku mwalimu wa somo akiwa pembeni.

Wanachuo sasa hatuna haja kwenda 'ferry' ili kupata huduma hii muhimu ambayo baadhi ya 'watu' wanaiona kama ni ya anasa.

lakini kikubwa kinachoonekana hapa ni ratiba ya kuingia madarasani kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanaamua kushinda 'lab' wakiamini mtandao ndo kila kitu, labda ni 'ugeni'.
Tusubiri tuone mabadiliko ambayo yameendana kabisa na uongozi mpya wa chuo

Friday, February 16, 2007

BARABARA YA KATI INAHITAJI MIUJIZA...!!!!!

Wiki jana nilikuwa ndani ya basi toka Dar kuelekea Mwanza kwa ajili ya kukamilisha utafiti wangu kuhusu kuongezeka kwa wapigadebe katika vituo vya mabasi. Chuo kilitoa muda mfupi uliolazimu sisi tunaotoka mikoani kutafuta usafiri wa haraka ili kuwahi kalenda. najua unafikiria ndege, kwangu mimi usafiri wa haraka si ndege, ni basi.

Tuliondoka kwa basi la Mohammed ambalo nalo kama ilivyokuwa kwa barabara ya kati toka dodoma kwenda singida, lilikuwa ni bovu isivyo kawaida kiasi cha kutulazimu kuingia Dodoma saa 4 usiku. hata hivyo hii si ishu yangu ya leo, leo nataka kuongelea ubovu wa barabara hii maarufu kama njia ya kati.

Barabara hii ni mbovu sana na hasa katika kipindi hiki cha mvua, maeneo ya manyoni na baadhi ya vipande vya tinde hali ni mbovu sana.
Hali hii inashangaza sana kwani serikali kuanzia ile ya awamu ya tatu ilikuwa ikihubiri kwamba ni mapema tu mtu ataweza kutoka mwanza mpaka mtwara kwa gari dogo 'tax'.

Kandarasi aliyepewa kufanya shughuli ya kujenga barabara hii angekuwa ni mtanzania basi tungesema ni ndugu wa kigogo lakini kwa kuwa ni mgeni basi hapo kwa akili ya kawaida kabisa tuliyozoea sis basi tunasema kuna mtu kala, kwani huwezi kumpa mkandarasi asiye na uwezo kazi kubwa kama hii.

Nitakuandikia tena kuhusu tatizo la usafiri ambalo kwa kuwa viongozi wanatumia usafiri wa haraka,ndege, kwao si tatizo

Thursday, February 01, 2007

KUKOSEKANA KWA HUDUMA ZA KOMPYUTA CHUONI KUNA SABABISHA USUMBUFU KWA WANAFUNZI......

Unashangaa kuona kichwa hicho, najua unategemea kabisa hili kutokuwa tatizo katika chuo tena cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere. Umekosea.

wakati shule zinazoitwa za 'academy' (sio academy ya mwalimu nyerere) siku hizi watoto wanafundishwa kompyuta, hali hii ni tatizo hapa chuoni kwani ukitaka kufahamu ni wanachuo wangapi wana uwezo wa kutumia kompyuta basi idadi yao itakusikitisha na kukufanya labda ufikiri kuwa hapa kumejaa ubabaishaji tu.

Sio kwamba kompyuta hakuna, la, zipo kama 40 lakini zima ndani ya vyumba vyenye milango ya chuma na mlinzi nje kuhakikisha kuwa hakuna anayechungulia na kuona vitu vya ajabu, kompyuta.

Mkuu kateuliwa na labda tunaweza kuanza kuiona kompyuta 'live'

Tungoje na kwa wale wasiojua basi wasubiri au waende wakajiandikishe katika akademia za kitoto
KAULA TENA!!!

Kila mmoja alikuwa na mshawasha wa kutaka kujua ni nani atashika nafasi ya ukuu wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, wengi walikuwa wakifikiria mabadiliko......

Majuzi waziri wa elimu ya juu kafanya kile ambacho alipaswa akifanye, kuteua mkuu wa chuo nafasi ambayo ilikuwa inashikiliwa na daktari Magotti ambaye pia ni kada mkubwa chama tawala CCM.

Uteuzi umefanyika na aliyeteuliwa kuwa mkuu wa chuo ni yuleyule aliyekuwa akikaimu na ambaye amekuwa mkuu wa chuo tangu kilipokuwa chuo cha chama na sasa chini ya serikali.

Ndiyo, jina jipya la chuo lakini mkuu yuleyule, hii ina maanisha kuwa tutegemee mengi na makubwa toka kwa kiongozi mkongwe.

machweo inamtakia dr Magotti kazi njema na itampa ushirikiano wa kutosha kama tulivyoombwa na msarifu ambaye naye ana kaimu nafasi hii, kwa maoni yetu sisi wana machweo tunadhani hata msarifu arudishwe yuleyule na pia korando likarabatiwe liwe jipya.