Wednesday, April 18, 2007

MGOMO WA CHUO KIKUU, NANI ANAFAIDIKA!!!

Katika kikao chake maalum cha 172 kilichofanyika tarehe 17 april,2007 Baraza la chuo kikuu cha dar es salaam kiliamua kuwasimamisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma udsm pamoja na vyuo vishiriki kwa kushiriki katika mgomo'haramu' wa kupinga malipo ya 40%.Wanafunzi hawa wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana.

Serikali makini hutumia rasilimali zake katika kuhakikisha kuwa inajenga na kuelimisha vijana ili waweze kuwa na manufaa kwa jamii na serikali yote. Vijana huandaliwa kuja kuwa watu makini na maandalizi haya yana gharama zake amabazo wakati mwingine kama mtu binafsi hawezi kuzibeba na kukidhi gharama hizi.

Nchi zetu nyingi za kiafrika zimekumbatiwa na umaskini ambao si wa mali wala watu bali umaskini wa mawazo ya kupanga nini kipewe kipaumbele kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kesho na si kujineemesha leo na kutaka sifa sizo maana.

Serikali zetu nyingi zimekuwa zikitenga fungu kubwa sana kwa ajili ya ulinzi na IKULU huku sekta nyingine zikipewa kiduchu. Sipingani na kutoa vingi kwa ajili ya ulinzi lakini nashindwa kujizuia kujiuliza kwamba sisi Tanzania adui yetu ni nani na kwanini IKULU itumie pesa nyingi saaaana kwa kipindi kifupi!?

hakuna kitu muhimu kama elimu, haijalishi kama ni elimu ya kujitambua ama ni elimu ya kukariri ili upate cheti huku ukishindwa kujitambua. Kujitambua mara zote huanzisha safari moja.

Siwaungi mkono waliogoma kwani naamini kabisa kuna njia nyingine ambazo wangechukua ili kupata haki yao (ambayo hata mimi ninaihitaji). Wengi wa wanafunzi(nikiwamo mimi) tunatoka vijijini na nauli yakutufikisha chuoni hubidi upitishwe mchango, sasa serikali inapotoa mkopo ambao haukidhi mahitaji na bado haikubali kuwa ndani ya nchi kuna matabaka hivyo wengine wanapaswa kupewa zaidi ya wengine na wengine kunyimwa kabisa(hebu wafikirie watoto wa vigogo ambao wamesoma shule za kulipa mamilioni ambao nao wazazi wao wanataka wapewe pesa zinazotustahili makabwela!)

Suala la matumizi ya anasa ya baadhi ya ofisi za umma na watendaji wa umma linachangia sana katika kutengwa kwa vitu muhimu vya kutimizwa.

Najua watu wengi wnawalaumu wanafunzi wa udsm kwa mgomo, lakini kujitambua ni hatua kubwa katika maendeleo hata kama namna ya kuyaleta itaumiza.

Ni lazima kuwepo na vipaumbele katika vitu muhimu hasa suala la elimu ya juu na ya ufundi ili kujenga taifa endelevu. Masuala ya baadhi ya ofisi kutumia pesa za walalahoi kwa ajili ya manufaa yao hayafai katika nchi hii. Tubadilike na tujitambue huku tukiweka ubinafsi, unafiki na ubabzazi pembeni ili tuendelee mbele. Mgomo ulisitahili na mkopo ni budi utolewe kwa wahitaji kwa 100%

No comments: