Tuesday, July 25, 2006

KILA MTU NI MPIGADEBE!

Hata wewe ni mpigadebe
Haya kaandika mwandishi makini wa makala katika gazeti la kila wiki RAI, huyu ni faza Priva Karugendo, nisipoteze kusema alichosema hebu soma mwenyewe na uone alivyoandika na kwa kauli yake hatakomea hapokwani ataandika mengi kuhusu hili(wakati anaandika alikuwa anawahi ndege toka mwanza kuja dar, huyu ni mwanaharakati wa mambo ya kijamii, na mwanafalsafa wa kileo,ukisoma makala yake anayomlaumu Chachage kwa kufa utaelewa ninachokisema) na hivyo usiache kusoma suala hili katika blog hii

Ndugu yangu, Asante sana kuandika. Leo hii nitakuwa Dar. NitaondokaMwanza, na ndege ya saa mbili usiku.Ukipata nafasi uniite kwenye simu. Lakini Juma lote nitakuwa ninakimbia huku na kule. Unajua, Watanzania wote ni wapigadebe! Maana yake ni kwamba: Hatufanyi uzalishaji. Mtu ananunua shati Kampala, analileta Magu, Mwingine ananunua shati lilele na kulipeleka Mwanza, wa Mwanza, analipeleka Moshi, Arusha hadi Dar. Yote hayo ni sawa na kupiga Debe. Mpigadebe, anapata pesa kwa kumleta mtu kwenye gari, ambalo hata kipofu anaweza kujua kwamba linaelekea Mwanza! Anapata pesa bila kuzalisha chochote. Mwisho wa mwezi anakuwa na pesa kuwazidi watu walioajiriwa ofisini!

Umeyaona haya, mengi yaja
WAPIGADEBE

Nimeamua nichokoze mawazo yako wewe mwananchi kuhusu suala la wapigadebe katika vituo vya mabasi ya ndani ya miji (daladala kwa dar na express kwa mwanza)na nje ya miji (yale yaendayo mikoani)

Hawa ni vijana wenye umri wa kati kuanzia miaka 15 hadi45 yaani ni kama marehemu profesa Chachage alivyopenda kuwaita vijana wa kizazi cha dot.com. Aliwaita hivi kwa sababu moja kubwa bayo ni kwamba wengi wa vijana wamezaliwa baada ya tz kupata uhuru yaani baada ya 1961 na wamekulia katika kipindi ambacho nchi imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni,

Tukirudi kwenye mjadala kuhusu kundi hili ambalo sasa linakua kwa kasi mpya na nguvu ya jumbo, hivi ni sababu zipi zinasababisha hali hii itokee

Je jamii inahusika na jamii ni nani kama ni hivyo! serikali na taasisi zake ina mkono katika hili!

karibu utoe maoni yako!

Saturday, July 22, 2006

SOMA UTENZI HUU

Nimeupata toka kwa rafiki yangu anayeblog pia

Utenzi wa Prof Issa Shivji aliouandika juu ya kifo cha ghafla cha guru la sayansi ya jamii prof Seithy Chachage


.Ndugu yangu
Rafiki yangu
Kamaradi Chachage:
Nani kasema umetuacha?

Eti umefariki!
Kwani mwili ndiyo maisha?
Maisha ni fikra. Maisha ni vitendo.
Maisha ni ubinadamu.
Fikra zako,
vitendo vyako,
ubinadamu wako,
utadumu.
leo, kesho, keshokutwa na milele.
Vitendo vyako tutavienzi,
ubinadamu wako tutauiga,
fikra zako tutazieneza.
Msomi wa Afrika,
mteTEzi wa wanyonge,
mshabiki wa fikra za kitabaka,
tabaka la wavujajasho.
nimetumwa.
Nimetumwa na Wasomi wenzako wa Afrika kupitia CODESRIA nikuletee Salaamu zao.
Wameniambia, nikuage.
Nimekataa.
Sikuagi.
Nitakusindikiza tu.
uwaone Wazee Wako,
majirani zako,
watu wema wa Njombe.
Uchanganyike na viumbe wa ardhi na bahari,
viumbe visivyo na ubaguzi,
mipaka,
unyonyaji,
ukandamizaji.
Uwashawishi,
wafundishe wanadamu maana ya ukombozi.
Kama ulivyokuwa unatufundisha sisi daima.
‘Ewe Issa,
kwani,
Shivji siyo mwana wa adamu?’,
Ukanitania,
Ukichota kutoka hazina ya ucheshi wakO bila uchoyo.
"Umejipachikia majina haya yote ya Miungu! MLIMBIKAZI, WE ISSA!’
"Mungu wa Waislamu na Mungu wa Wakristo,
Mungu wa Wahindu na Mungu wa Wasambaa.
unataka wapigane?
wachinjane.
Eti moja ni –a, mwingine ni –ji!’
"Futilieni mbali ushenzi wenu wa kubaguabagua!’,
ukakasirika.
"Unganeni kujikomboa",
umetusihi, "kutoka kwa makucha ya ubeberu na ubepari,
unyonge na udhalilishaji.’
Buriani ndugu yangu,
Buriani rafiki yangu,
Buriani Kamaradi Chachage.
Ufikesalama.
Upumzike na Viumbe visivyonyumbishwa na vituko vya Wanaadamu.
Nakuahidi.
Nitaufikisha ujumbe wa maisha yako.
Kwa WanaUdasa,
Kwa WanaCodersia.
Kwa Wana wa Tanzania,
Kwa Wana wa Afrika………………….Buriani………..

Wednesday, July 12, 2006

BAHATI NASIBU YA MWALIMU NYERERE!!!

Nadhani sasa kila kitu kinafanywa ize isivyo kawaida, umeisikia hii bahati nasibu ya mwalimu!

Inawezekana jina la mwalimu sasa likawa ni ulaji, kama na wewe unachochote unachotaka faida basi andika mswada na tumia jina la mwalimu utapata pesa ule na unywe
PROFESA CHACHAGE KATUTOKA!!!!

Hakika nakosa maneno ya kuandika kuhusu kifo cha ghafla cha guru la midahalo ya kisomi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Inahitaji kuwa na nafasi kubwa kuweza kuandika kile ninachofahamu kuhusu mtaalam huyu wa sayansi ya jamii na mwandishi wa vitabu.

Nakikumbuka kitabu chake ambacho kinapingana na utandawazi usio haki unaopigiwa chapuo na viongozi ambao nia yao si ya jamii nzima bali ni kujitajirisha peke yao na watoto wao, kitabu hicho kinaitwa Makuwadi wa Soko Huria

Si kwamba watanzania tumepoteza lulu bali afrika nzima na wote wanotaka usawa duniani wamepoteza hazina kubwa lakini kupitia maandiko na machapisho yake hakika watazaliwa kina chachage elfu

Nakumbuka msemo wako wakati ukihojiwa na mtayarishaji wa kipindi cha luninga Sema Usikike ulisema neno ambalo sitokaa nilisahau " hakika kuhusu ujambazi kuna sehemu imeoza na wala si sahihi kusema kwamba umaskini ndo chanzo cha ujambazi, jamii na viongozi wa serikali wajiangalie wapi kuna mgogoro unaozalisha wimbi la majambazi na wapiga debe"

Buriani Pro. Seithy Chachage

Thursday, July 06, 2006

KUPANDA KWA ADA MNMA KUNAENDANA NA BAJETI YA KIKWETE?

Linaweza kuwa kama swali la mtu aliyechoka kufikiri. Nimewahi kukuandikia kuhusu kupanda kwa ada hapa chuoni kulikotangazwa na kaimu mkuu wa chuo kama ilivyoamliwa na kikao cha bodi ya chuo hiki chenye jina la muasisi wa taifa hili na aliyekuwa anataka kila mwanachi asome maana yake ni kuwa ada ya masomo iendane na uwezo halisi wa mtanzania wa kawaida.

Sio vibaya kujifikiria kitu ambacho wenzako wanaweza kukufikiria vinginevyo lakini kwa suala la ada kupanda hapa chuoni linamgusa kila mtu anayetoa pesa ili kupata elimu. Inawezekana kabisa waliopandisha ada (bodi) walikuwa na sababu kubwa na za msingi huku wakisaidiwa na utafiti walioufanya kana kwamba kutoza ada kubwa ndo kuonekana chuo bora

Lakini inawezekana kuwa wao kama wao na mishahara yao hawaoni tatizo na ada hii mpya kwani kama watu wanakaa kikao kwa siku na kulipana posho sawa na mshahara na marupurupu ya mwezi ya askari ada hii kwao ni ndogo na ni aibu kuilipa kana kwamba mwalimu alikuwa anafanya biashara ya elimu.

Pia labda bodi ilijua kwamba rais ataongeza mishahara na ndiyo maana ikaamua kuongeza ada ili kutorahisisha maisha kwa namna yoyote na hasa ukizingatia kuwa chuo hiki kipo katika ilani ya ccm katika mkakati wake kukiwezesha na kukikarabati!

Nakaribisha maoni kuhusu suala la kupanda kwa ada. Nenda sehemu iliyoandikwa comment bonyza na andika maoni yako na uyatume. Karibu
TUMEFUNGA CHUO!!!

Ijumaa iliyopita ilikuwa ni siku muhimu sana kwa wote wanachuo kwani ukiacha wengine waliokuwa wanamaliza mwaka wao wa kwanza wa masomo wengine walikuwa wakimaliza kozi zao za stashahada na cheti.

Ilikuwa ni siku ya maagano huku kila mmoja akiwa na huzuni ya kuachana na rafiki yake na furaha ya kupokea cheti na kuanza mwaka mpya wa masomo bila kusahau ada iliyopanda

Blogu hii inawatakia mapumziko mema wanachuo wa vyuo vyote na ni wajibu wetu kutunza afya