Saturday, January 28, 2006

KISWAHILI: NI WAKATI WAKE SASA
Na: Obe M. Mashauri


Si lengo la makala haya kuwalaumu viongozi waswahili wanaotumia lugha za kigeni katika shughuli zao za kitaifa na hata kimataifa. Lengo la makala ni kutaka tu kuonyesha ni jinsi gani lugha hii iliyotulia kama maji ya mtungini ina uwezo wa kuwawakilisha viongozi hawa kwa kundi kubwa la wananchi wanaowaongoza katika dunia hii ya utandawazi.
Kati ya vitu muhimu ambavyo humtofautisha mwanadamu na wanyama ni lugha. Mwanadamu huyu ana lugha halisi ambayo humwezesha kuwasiliana na mwenzake sehemu mbalimbali. Kiswahili ni moja ya lugha nyingi zinazotumika duniani.
Kiswahili ni kitambulisho kikubwa kwa mtanzania na watu wote wa africa ya mashariki na kati. Ni lugha yenye utajiri wa kila kitu kwa ajili ya mawasiliano katika nyanja zote za maendeleo. Lugha hii inayojitosheleza katika shughuli zote za kiuchumi, utamaduni, siasa, elimu, sayansi n.k.
Kitendo cha mtu kuacha kutumia lugha yake kwa makusudi kabisa mbele ya watu wake ni utumwa. Ni utumwa kwa sababu mtu huyu atatakiwa kuiga mawazo ya wenye lugha anayoitumia. Kiswahili katika afrika mashariki ni lugha makini inayomfanya mtumiaji makini kujivunia na kuringa nayo.
Wakati wa ubaguzi wa rangi nchini afrika kusini, makaburu walikuwa na msemo maarufu usemao “lugha ya mvamizi ikiongewa na mvamiwa basi ni lugha ya mtumwa”. Hii ina maana ya kwamba wavamizi hawa walipofika pwani ya nchi hii(mwaka 1652 ),waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Utamaduni, mawazo na ustaarabu wao ulionyeshwa na lugha zao.
Wazungu wa rangi zote walipokuja afrika kwa madhumuni ya kupora utajiri chekwa waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Lugha hizi weupe hawa waliziita eti ‘lugha za kishenzi’. Ni kwa kutozielewa lugha hizi ndipo wakaja na jibu la haraka na kutuita watumiaji wa lugha zetu washenzi. Tukawa watumwa wa lugha zao tena washenzi.
Utumwa huu wa kudharau lugha zetu bado ni donda sugu katika jamii zetu waafrika. Si ajabu hata kidogo kwa nchi zetu kukuta zimejigawa katika makundi yanayojiita: a) waongea kiingereza na hawa waongea kifaransa!. Bahati mbaya sana na waafrika mashariki tumeingizwa katika makundi haya ilhali tuna lugha yetu, kiswahili.
Makala haya hayana lengo la kudharau lugha nyingine au kuzibeza bali ni kuonyesha tu ni vipi kiswahili (kimeundwa na lugha za kibantu) kinaweza kutumika kusini, kati na mashariki mwa afrika. Sehemu hizi zina majimbo mengi yaliyozaa lugha ya Kiswahili. Mwanazuoni Malcon Guthrie anatoa ushahidi wa hili katika tafiti alizofanya katika karne ya 19.
Kiswahili kama kilivyo kiingereza ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali zilizoko katika bara hili. Ndio maana wanazuoni hukiita Kiswahili kuwa ni kibantu sababu tu kinaundwa na maneno yanayoongewa na wakazi wa afrika.
Kwa mseto huu utaona ni jinsi gani lugha hii inajitosheleza kwa misamiati, nahau na mambo yote yanayohitjika katika kikwi hiki cha maendeleo.
Wengi tumekuwa tukikidharau Kiswahili kwamba si lugha ya maendeleo. Tumekuwa ni watumwa tukiaminishwa kwamba kiingereza tu ndio lugha ya kila kitu. Kasumba hii imegubika vichwa vya waswahili wengi kwamba bila kujua ‘kizungu’ wewe si kitu.
Utumwa huu tunao watu wengi tukifikiri kwamba ‘kizungu’kinajitegemea. Hakuna lugha inayojitegemea yenyewe mfano, kiingereza ni lugha yenye mchanganyiko wa maneno toka nchi mbalimbali zenye makabila tofauti.
Kiingereza kina maneno toka uyunani, hispania, ujerumani na uholanzi. Na hata watu wa kwanza kukiandika walikuwa ni waholanzi wa wakati huo waliokuwa na utaalamu wa kutengeneza mashine za kuandikia (taipuleta) maneno.
Pita siku moja sehemu wanakouza pombe na ujionee mwenyewe jinsi wasomi waswahili wasivyopenda kuongea lugha yao ya pili. Wanadharau lugha iliyofanya kazi kubwa ya ukombozi wa bara la Afrika.
‘Wasomi’ hawa hawataki kuongea lugha yao kwani wakiongea watajishushia hadhi yao ya usomi. Huku ni kuunda matabaka ya wanaojua kizungu (bora!)Na wasioongea kizungu (hasara?). matabaka haya yasipoangaliwa yatatugharimu.
Kiswahili kimejaza misamiati na maneno lukuki ambayo wasomi waliooshwa ‘bongo’kizungu hawaelewi. Watasema Kiswahili kinakosa maneno kama: television, computer, osamaphobia n.k. Hakika watu hawa hawajui maneno haya ni wapi yanatoka.
Hawana habari ya kwamba neno ‘computer’ ni matokeo ya maendeleo ya sayansi, ‘television’ ni neno linaloundwa na maneno mawili ya kigiriki yanayomaanisha kuona mbali. Ukiwaeleza kuhusu luninga, tovuti, asasi, wahanga, kikokotozi, king’amuzi watakushangaa na kukosa ulimi.
Jamii kubwa hasa walimu imekuwa ikitathmini akili ya mwanafunzi/mtoto kwa ufahamu wake wa kizungu, je anajua kizungu?. Hivi kizungu kukijua ndio mtu unakuwa na akili?. Huku ni kuchoka kwa mawazo ndani ya jamii yetu.
Wazazi nao hasa wa mijini wenye kipato wanashindana kupeleka watoto wao katika shule zinazotumia mitaala ya kizungu kufundisha. Huko Kiswahili wala utamaduni wa kiafrika hakuna mambo yote kizungu. Mtu asipoongea kizungu ni kweli hana akili? Kweli!
Kwa kudharau lugha yetu yawezekana ndiyo maana maendeleo hatuna. Mtu anasomea shahada ya ukulima morogoro, masomo hapa ni kwa kizungu. Mtu huyu huyu akimaliza masomo yake atakwenda kijijini kwa wakulima wasojua kizungu. Kilimo kitaendelea kweli ikiwa msomi huyu atatumia kizungu chake kufundisha!.
Wataalamu wapo ila lugha hazielewani. Hapa hakuna maana ya kwamba kwa kutojua kizungu wakulima wetu ni mbumbumbu wa ukulima.
Profesa Kihumbi Thairu katika kitabu chake ‘the africani civilization’anasema “nakumbuka mshtuko nilioupata miaka ya 50chuo kikuu cha Makerere, mwanachuo alimuuliza mhadhiri mzungu wa kitengo cha sayansi ya wanyama kwamba ni kwanini watu wanaanguka katika somo lake?
…Msomi huyu mzungu alitoa jibu fupi tu kwamba ‘kizungu’ wanachuo hawawezi kuandika kiingereza. Upofu wa mwanazuoni huyu bado unawaandama wasomi wetu wengi ambao hawataki kukubali kwamba kiswahili kinaweza kutumika na kutoa matunda mazuri kwa maendeleo ya jamii yetu na dunia kwa ujumla. Hata hivyo mwandishi hamlaumu mzungu huyu.
Kizungu kukijua hakimaanishi akili. Mmoja wa walimu wa kujitolea alipata nafasi ya kufundisha katika shule niliyosoma mkoani mwanza. Wakati aliporuhusu kufanya majadiliano ya somo alishangaa kusikia wanafunzi wakitumia Kiswahili.
Japo wachache walienda mbali kwa kutumia lugha ya asili (kisukuma) lakini wengi tulitumia kiswahili na mwalimu alifurahi kwani somo lake tulilifanya vizuri sana tena kwa kuandika kizungu.
Laiti wasomi na viongozi wetu wangekuwa kama mwelimishaji huyu hakika tungekuwa tofauti na wengine. Maana yake ni kwamba tungekuwa na maamuzi bora bila kutegemea mawazo ya lugha nyingine japo si vibaya.
Kiswahili kingetumika kama lugha ya kufundishia mashuleni basi kiwango cha kufaulu kingekuwa ni kikubwa tofauti na sasa. Wanasaikolojia wanaamini mtu anayefundishwa kwa lugha yake mwenyewe anaelewa zaidi tofauti na vinginevyo.
Hivi majuzi wizara ya elimu ilikataa kusajili shule tatu ambazo zingetoa elimu ya sekondari kwa kufundisha masomo yote kwa kiswahili (gazetila kiswahili la tarehe 17/01/2003). Sioni mantiki ya shule hizi kukataliwa ikiwa wenye kumweka madarakani waziri ni wananchi wanaotaka kufundisha kwa lugha ya taifa lao.
Kuruhusiwa kwa shule hizi si tu kwamba kiwango cha kufaulu kitapanda ila matabaka ya wanaojiona ni bora kwa vile wanaongea kizungu yatatoweka na wote tutapata taarifa sahihi zilizoandaliwa kwa umakini na kwa uwazi. Kiwango cha kufaulu kikiwa kikubwa na shule, vyuo vikawepo maendeleo hayaepukiki.
Watanzania hatupendi kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha yetu ya taifa. Makabati yetu yamejaa vitabu vya waandishi wa kizungu hata kama ni hadithi za watoto. Vitabu vilivyoandikwa Kiswahili havina nafasi kabisa.
Wengi hatujui kwamba sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kiweze kuwa na nafasi katika umoja huu ni budi watumiaji wa lugha hii kuitumia kila mahali ili wengine nao wafuate ili kujifunza.
NINI KIFANYIKE
Lugha hii ni ya kiafrika zaidi kutumika katika umoja huu (AU). Hakuna asiyeelewa shughuli pevu iliyofanywa na kiswahili katika ukombozi wa karibu bara lote la afrika. Hivyo ni stahili yake bila maswali kuwa lugha ya bara zima.
Viongozi wa karibu nchi zote zinazoongea lugha hii(japo kidogo)wasisitize matumizi ya kiswahili katika nchi zao ili kuondokana na kasumba ya kutaka tu mawazo yanayotolewa kwa lugha ngeni.
Mabaraza ya Kiswahili yaundwe kila nchi kama ilivyo kwa nchi za Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda pamoja na nchi nyingine. Mabaraza haya kweli yafanye kazi ya kukieneza sehemu mbalimbali duniani.
Katika umoja huu wa afrika matumizi ya lugha hii yatiliwe mkazo si kama azimio lililoamua kutumika kwa lugha hii kule Madagascar lilivyozembewa. Viongozi waafrika waliacha na kufanya lugha zisizo na asili ya afrika kuamua mambo yao.
Ni furaha iliyoje kwa mtu aliyekukuta ukiwa na lugha yako akaiita kuwa ni ya kishenzi, akiwakuta leo mkiongea kwa lugha yake. Nina hakika atasema ‘nisingewatawala watu hawa wasingeweza kuwasiliana’!
Ni kweli kwamba kazi ya kufasiri vitabu kutoka lugha moja kwenda nyingine ni gharama kubwa kwa nchi zetu. Serikali kupitia mabaraza yake ni budi ifanye kazi hiyo. Watu tumechoka kukariri pindi tufundishwapo. Tufanye kile tutakacho sio wao watakacho.
Wananchi ndio wanaowaweka viongozi madarakani kuwaongoza na si kuwatawala, hii ndiyo demokrasia. Viongozi hawa ni wasomi, baadhi wapenda kutumia lugha zisizoeleweka kwa jamii kubwa.
Kwa hapa Tanzania hotuba nyingi zinazotolewa na viongozi wetu ama nje au ndani zinachefusha, hazieleweki kwa wengi, yaani zimeandaliwa kwa lugha ya kigeni. Kuwa kiongozi bora si lazima ujue kizungu japo si vibaya.
Tuige mfano wa kiongozi mmoja maarufu barani kwetu ambaye alisema kwamba anaongea kizungu ili tu wasiojua lugha yake wamwelewe na si kutaka sifa kwamba ni kiongozi mzuri, makini. Uongozi bora sehemu yoyote hauonyeshwi kwa viongozi kuongea na kuhutubia kizungu.
Mwasisi wa taifa huru la India Mahatma Gandhi aliwahi kusema kwamba katika eneo analotoka ni vizuri akatumia Kigujarati kama lugha ya kiserikali. Huyu ni msomi aliyezunguka nchi nyingi kutafuta elimu, masomo yake mengi aliyasoma kwa lugha zilizokuwa zikimpa shida kuelewa. Uamuzi wake wa kuamua Kigujarati kiwe lugha kuu katika India kunaonyesha uwajibikaji.
Katika dhifa za kimataifa walizofanya viongozi wa mashariki ya kati hapa nchini, hotuba zao zilitolewa kwa lugha zao. Ajabu viongozi wetu walitoa hotuba kwa lugha ya kizungu. Si vibaya nikifikiri kwamba wageni hawa walituona sisi ni vichaa.
Kituko kingine kilijitokeza wakati wa ufunguzi wa jengo la utalii hapa nchini. Kulikuwa na ulazima gani wa kutumia lugha tusiyoielewa, huku ni kutufanya sisi watumwa. Pamoja na utalii, sifa yetu nyingine ni lugha yetu.
Waandishi na watunzi wa kiswahili ni watu muhimu kwa ukuaji wa lugha hii. Ni budi wakitumie Kiswahili katika kazi zao bila kukipindisha. Wanamuziki na wasanii nao watoe kazi zao kwa ubora na umakini wakitumia lugha ya hadhira yao.
Watanzania sasa tujenge kasumba mpya ya kujisomea vitabu vyetu. Tununue vitabu ili kuwapa nguvu wachapishaji na watunzi waweze kufanya kazi za kiswahili bila kinyongo.
Sisi ni matajiri, tumebarikiwa kila kitu lakini kutokana na kudharau utajiri wetu ikiwemo lugha, tumekuwa ni wajima. Sifa yetu kubwa ni umaskini. Wakati fulani madiwani wa mkoani Mwanza waliandikiwa taarifa fulani na ‘wataalam’kutoka ‘PWH’taarifa iliandikwa kizungu. Wakapelekewa madiwani waswahili ‘wengi’. Ili uwe kiongozi hapa Tanzania ni lazima ujue kusoma na kuandika! Kwa ‘ripoti’ hii ya eti ‘wataalam kwa vile wameiandika kizungu’ nina uhakika asilimia 85 ya wawakilishi wa watu walikaa kimya katika kuijadili. La kujiuliza hapa ni hili, hivi sisi nani ametoroga ?
Tunathamini mawazo kutoka nje ambayo lengo lake ni kutuibia. Tukitumia lugha yetu katika mambo yetu tutakuwa tumeondokana na utegemezi wa mawazo kutoka nje.
Kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwa kila mtu zitolewe tuzo nia ikiwa ni kuenzi kazi zilizofanywa na watu waliokipigania kiswahili. Tuzo kama za Ibn batuta, Jumbe Akilimali, Shaaban Robert, Mnyampara na wengine wengi zitatoa changamoto kwa watu kutumia lugha hii.
Kuondokana na utegemezi wa kila kitu katika jamii yetu kumo ndani ya mikono na akili zetu. Kutumia lugha yetu hakuhitaji mzungu kutushauri. Ni wakati wa Watanzania na waafrika kuamka. Tutumie lugha ambazo ni za kiafrika zaidi.
Kujikana kwetu na kudharau na lugha yetu kunatufanya sisi tunaojiona bora (kwa kuongea kizungu) kuharibu hata hizo lugha tunazozikumbatia. Si jambo la kushangaza kumkuta mtanzania anyejidai na kizungu anashindwa kuongea kwa ufasaha lugha hizi za wakoloni.
Maendeleo tunayoyahitaji watanzania yawezekana hata kama tutatumia lugha yetu. Haiingii akilini mtoto anafundishwa lugha ya Kiswahili shule ya msingi tu na akiingia sekondari basi kizungu mtindo mmoja, huku ni kutuchanganya sisi vijana. Tunashindwa kuhoji, kwani Kiswahili hakina nafasi.
Suala la kutumia Kiswahili katika shule na vyuo vyetu halihitaji siasa. Wakati umefika kwa watu wote kuamka na kwa kauli moja kusema sasa ni wakati wa kiswahili.
Utamaduni wa wenye madaraka kutoheshimu matakwa ya wananchi ndio uliomfanya mwenye dhamana ya kusajili shule kuzinyima usajili shule hizo tatu nilizoongelea hapo juu. Nina uhakika kama ni wazungu ndio wangeomba kusajili shule hizo basi kusingekuwa na matatizo, wasomi wanaopenda kiswahili kitumike wanachukiwa.
Sababu kubwa ya kuchukiwa kwa wenye busara hawa ni labda kama kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia basi watapata pesa ya kufasiri vitabu kuwa katika kiswahili. Huu ni upofu wa fikra, hoja hii wala haina mashiko, taifa tulitakalo ni lile linaloona mbali si lenyo watu wanaoona umbali wa pua zao tu.
Serikali inadai kwamba inatoa nafasi kwa wananchi na asasi mbalimbali kutoa mawazo yao ili kuleta maendeleo. Mtazamo huu ninashindwa kuuelewa nikifiria kuhusu kubanwa kwa kiswahili katika kuleta maendeleo.
Tafiti zilizofanywa na Mlama na Materu mwaka 1976 mpaka 1977 zilibainisha kwamba lugha yetu ya taifa itumike katika sekta nzima ya elimu. Mradi wa kuboresha ufundishaji wa kiingereza uliandaa ripoti ya utafiti uliofanywa na wazungu mwaka1991 na kuainisha kuwa bado wanafunzi hawaelewi wanapofundishwa kizungu na wakapendekeza kizungu kifundishwe vizuri tangu shule za upili. Ripoti hii inaonyesha ni jinsi gani watafiti hawa waligundua kwamba kiswahili ndiyo lugha muhimu ya kufundishia katika nchi hii.
Uelewa mdogo wa mambo na elimu baguzi inayotolewa nchini unasababisha tukose wagunduzi na wataalamu mbalimbali katika nyanja zote muhimu kwa maendeleo yetu. Lugha zinazotumika kufundishia ni ngumu. Zinahitaji mtu ukariri na si uelewe. Unategemea nini kwa mtu asiyeelewa?
Viongozi wetu waandamizi nao ni vizuri wakatumia lugha hii ili tusichanganyane. Kitendo cha kutoa hotuba au miswada kizungu ni kutuminya wenye nchi tusihoji na hasa ukizingatia wengi tuna elimu ya msingi kwani sekondari ni chache na ghali. Wadau wote tupate kuhoji na kuelewa kwa lugha yetu sio kwa kizungu tusichokielewa. Hakuna haja ya kuibiana eti kwa kuwa tu sisi wengi hatujui kizungu. Uchumi wetu na maendeleo yetu ni budi tuyaelewe kwa lugha yetu ili inapobidi tuhoji.
Mpaka sasa sina uhakika kama watanzania tuna kitu kinachotutambulisha kwa wenzetu zaidi ya wimbo wa taifa ambao nahisi kuna watu wanatamani ungekuwa unaimbwa kizungu. Huu ni wakati muafaka wa kiswahili kutumika katika Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Maneno yaliyosemwa na mkuu wa chuo kikuu cha Mzumbe wakati wa ufunguzi wa chuo hivho mwaka jana kwamba wataanzisha utoaji wa elimu ya juu kwa kutumia lugha ya kiswahili ni changamoto kwetu. Hii ya kusikia tu kwamba Libya wanafundisha Kiswahili katika vyuo vyao ni aibu kwetu. Tuamke viongozi wa tanzania, kiswahili si wakati wa kampeni tu.
Inauma sana pindi unapotaka kupata habari juu ya kitu fulani habari hiyo unashindwa kuielewa kisa tu lugha iliyotumiwa kwa kumbukumbu hiyo ni ile isiyoeleka kwako. Hivi Kiswahili hakiwezi kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu jamani, au tunashobokea vitu tu. Nafasi ya lugha yetu katika kuhifadhi nyaraka na uhakika ni kubwa, nzuri na ya kudumu.
Hapo juu nimeongelea kwamba Kiswahili si wakati wa kampeni tu kwa viongozi wa tanzania. Watu watumie lugha hii hata kama wamekuwa viongozi. Hivi inakuwaje, unaomba kwa lugha moja na kutenda watenda kwa lugha nyingine wapi na wapi? Hii ndiyo inayotokea nchini kwetu kama huamini na haujaona mimi sina vidhibiti. Vya nini wakati ambapo hata hiyo lugha inayotumiwa siielewi, japo nikiielewa si vibaya.
Inasikitisha kuona waafrika tumesahau utu wetu na hatutaki kuulinda tena, uzungu umetuingia. Tunataka kujionyesha kwa wazungu kwamba sisi ni watu bora kwa kuiga kile wakifanyacho. Tunaiga hata jinsi wazungu wanavyoongea. Tunakwenda wapi sisi waafrika na tunalipeleka wapi bara hili tajiri. Lugha yetu ni budi tuipe heshima tusiivue nguo na kuiaibisha. Kiswahili yafaa kitumike katika shughuli zote za kila siku tuzifanyazo.
Napingana na kauli ya mhadhiri wa lugha za kigeni ya chuo kikuu cha Dar es Salaam aliyoitoa katika gazeti la ‘Sunday Observer’ la tarehe 19/01/2003. Msomi huyu M. Kadeghe anasema kwamba “wazazi wa Tanzania wanajua umuhimu wa Kiingereza katika kipindi hiki…” Kauli ya msomi anayeamini kizungu ndiyo uelewa!
Kutumia Kiswahili katika vyuo vyetu hakutatuweka kando katika kipndi hiki cha kutafuta maendeleo. Hivi nchi kama Japan, Italia, Ujerumani na nyingie zimemudu kupata maendeleo kwa kutumia lugha zao, kwa nini sisi na Kiswahili chetu tushindwe? Nchi hizi zote zinatumia lugha zao na kiwango cha maendeleo zilizonayo zinashinda hata zile nchi ambazo ‘msomi wetu’anazifagilia.
Kauli hii pamoja na ile iliyotolewa na waziri wa elimu ni moja ya kauli zisizofaa kutolewa na watu kama hawa. Watu hawa pamoja na wengine wenye dhamana katika nchi wanatakiwa kutoa kauli zenye busara, walizozifanyia utafiti wa kina na si mjini na kwa watoto wao wanaosoma katika shule za ‘…akademia’. Waende hata kule Mwabayanda, Mpitimbi na sehemu nyingine za vijijini kufanya utafiti na tuone watarudi na ni lugha ipi ifaayo hapa kwetu katika kipindi hiki.
Dk. Kadeghe ni mwalimu wa lugha, alifanya utafiti mwaka 2000 na kuweka wazi kuwa lugha hizi zote mbili zitumike katika ufundishaji lakini mtafiti mwingine Mwinsheikh aliweka wazi kuwa lugha ya kizungu ifundishwe kama somo tu, na masomo mengine yafundishwe kiswahili.
Kwa kutumia taaluma yake ya ualimu toka shule ya msingi mpaka chuo kikuu dk. Kadeghe anaelewa ni jinsi gani mwanafunzi anaelewa somo analofundishwa na kukariri somo analofundishwa. Haiitaji ‘PHD’ kujua kwamba mtanzania anayefundishwa kiswahili anaelewa zaidi kuliko mswahili anayefundishwa kizungu ambaye hakuna anachoelewa zaidi ya kukariri. Usitegemee swali kwa mtu anayekariri.
Lugha ‘ya kizungu’ hawa imefundishwa shuleni na vyuoni kwa karibu miongo minne sasa na hakuna kilichobadilika zaidi ya kuwepo makundi tu. Haijatusaidia kutatua tatizo la kilimo cha kutegemea mvua n.k. Tukipe nafasi Kiswahili na tuone kama hatujawafukuzia Wajapani. Wengi mtaona kama ninaota lakini ni kweli kwamba mtu akifundishwa kwa lugha yake huelewa zaidi na si kukariri.
Wengi mtasema kwamba mbona hata hicho Kiswahili kinachofundishwa wanafunzi wanashindwa kufaulu. Jibu ni rahisi tu kwamba kiswahili hakijapewa nafasi kubwa katika masomo, vijana wanaona ni bora kukariri masomo ambayo karibu yote ukiacha kiswahili yanafundishwa kizungu.
Masomo yakiendeshwa kwa lugha yetu nina uhakika maendeleo yatakuwepo kwani utafiti uliofanywa na Mwinsheikh ulitanabaisha bayana kwamba masomo ya sayansi (yanafundishwa kizungu!) yakifundishwa kiswahili wanafunzi wanaelewa zaidi. Sasa kama mtu anaelewa somo analofundishwa kwanini asivumbue vitu. Ukielewa kitu tabia ya kukariri waliofanya watu wengine itakwisha kwani mtu utavumbua chako.
Kompyuta sasa ni kitu ambacho wengi tunakiona ni kwa ajili ya ‘wateule’wanaojua kizungu. Hii si sawa. Mungu awazidishie nguvu na maarifa wataalamu wanaoweka ‘program’ za kiswahili katika chombo hiki cha kurahisisha kazi. Wote tutaweza kutumia na kupata vitu mbalimbali vitakavyoleta unafuu katika jamii zetu.
Kizungu na lugha zote za kizungu ni bora zikawa kama masomo ya kawaida tu. Ikibidi vyuo vya kufundisha lugh viongezwe ili kurahisisha mawasiliano kwani marafiki zetu wa Ulaya na sehemu nyingine si wote wanajua lugha ya ‘malkia’
Kuiga vitu kunafanya muigaji awe kama mtumwa, mtumwa ni yule mtu anayefanya kitu asichopenda kufanya. Hata kiongozi asiye na msimamo wa kuamua mambo mazuri hatoki ndani ya kundi hili. Kiongozi ni budi aongoze kwa matakwa ya jamii yake.
Hivi hatuna washauri wazalendo ambao ni wataalam wa mambo mbalimbali. Nani ameturoga yaani mpaka mshauri wa kujua nini tunataka atoke ‘uzunguni’ nje.
Kwani kiswahili kutumika mahakamani haki haitatendeka? Hapana
Kutumia lugha yetu shuleni na vyuoni ni dhambi? Hapana
Kiswahili kutumika kwenye makongamano no kosa? Hapana
Je, bila kuongea kizungu mtu anaonyesha kwamba hana akili? Hapana
Tunahitaji washauri wazungu ili watueleze kwama tutumie lugha yetu? Kwa hili jibu zuri laweza kutolewa na viongozi wetu wanaoamini mshauri anayetoa ushauri wake kwa kiswahili si msomi.

No comments: