Wednesday, January 11, 2006

MAWIO
Na: Obe Mashauri
Ndani ya jela, siku huisha kama jana, funguo ikifunga malango,nafungiwa usiku. Tunahesabiwa kama bidhaa dukani, kitambo kidogo taa zinazimwa na tunalazimishwa kulala kama watoto wa shule.
Usiku unakuja polepole tena kimya kimya. Macho yanatazama dari refu mikono kufikia. Kila mfungwa yupo macho akisubiri saa ili afurahie amani kwa usingizi.
Huu ni wakati mgumu zaidi gerezani. Ni wakati mabao kuta za gereza zinakuliwaza.
Asubuhi unaamshwa mapema sana, unahesabiwa kama ng’ombe wanaopelekwa malishoni, unapangiwa kazi,unachapwa ukitegea hata kama umechoka. Hakuna kupumzika bwana afande anataka akuone unajishughulisha sio unakaa kama uko kwa bibi yako. Kichwani mawazo yamejaa, unasubiri usiku. Hakuna kitu zaidi ya ukimya na mawazo yako kichwani.
Navuta kirago changu, ni kitanda hiki. Baridi ni kali,blanketi lenyewe fupi. Anophelesi wanahimizana kutafuta chakula kwani vyandarua hakuna, sherehe kwao.nawasha sigara natabasamu nikifikiria nilivyoipata,moshi unawafukuza mbu. Siko peke yangu niliye macho, wanautazama moshi wa sgara ukutafuta uhuru darini.
Chumba kimetawalwa na furaha ya upweke, kila mtu yupo kimya. Uso wang’aa,moyo umegubikwa na majonzi,sauti haitoki kijana analia. Kuwezi kuisikia mnyapara anafanya mapenzi na kiherehere,wote wanaume. Kila mtu anataka aishi kikawaida apasipo ukawaida.
Natizama moshi wa sigara unavyopaa,nadhani sasa ni saa 8 usiku. Moshi unazidi kufata dari ukielekea kusikojulikana. Ni kama maisha yangu. Swali liko kichwani mwangu,najaribu kulifukuza kwa bangi, linarejea stimu zikiisha na msokoto umeisha. Swali kuhusu maisha, malengo yangu maishani, wapi mafanikio?
Shuka imechoka, ni fupi, miguu imekataa kukunjwa,baridi linanifariji, kichwa kimechanganyikiwa, maumivu, bahati mbaya, kuta nene ajabu na askari waliokumbatia mianzi ya kizungu.
Nalia ka mbogo, kimya kimya, machozi mishipani yanaondoa nguvu za nafsi. Najisikia hatia, je, nimezaliwa bila bahati? Mbona wengine wanafanikiwa hata kama kichwa changu ni bora kuliko wao. Wengine mwenyewe nachangia mafanikio yao, mbona mimi sibahatiki! Tajiri wa mikosi, natabasamu. Jana imepotea moja kwa moja, kesho ni mbali sana, kuijua ni kama ndoto ya mchana.
Najaribu kurejea ndoto zangu baada ya kukabidhiwa cheti cha kumaliza shule,chuo, nafikiria ofisi nilizopita kutafuta kazi. Namfikiria mke wangu anayependa mambo makubwa nisiyoweza kuyakidhi. Nachoka nikifikiria familia yangu,mama na jamaa zangu. Nachoka kama mtoto anayetambaa, nina kiu, Israel anatabasamu na kunionyeshea kamba iliyo pembeni mwa kirago changu. Nimefungwa muda mrefu kazi bila malipo na nimesoma.
Siko peke yangu, tuko wengi lakini najisikia mchovu, kuzeeka sio kuwa na umri mkubwa tu. Nimezeeka nikiwa kijana tena kijana mbichi. Mzee wangu amekuwa mlevi eti pombezinamfariji baada ya kukosa mafao yake ya iliyokuwa EAC. Kama wameutendea mti mkavu namna hii vipi kwa mti mbichi.
Nimechoka, nitaondokanaje na chaka hili, nitapataje kazi, wacha nisome nani atanilipia karo na serikali ina wenyewe!
Viongozi wajifunze maisha yetu wasione watoto wao wanatabasamu wakafikiri nasisi tuko kama wao.wengine tumefungwa na msamaha hauonekani, upendo hakuna bila pesa.ajira zisitoke kwa upendeleo
Nahitaji mabadiliko, nataka kuishi maisha bora, nahitaji kufanya mapinduzi. Naichukia serikali yangu. Mko wapi mliotoswa?
Nini nifanye nikomeshe upuuzi huu wa kujipendelea. Nafikiria kuua, nafsi inakataa kwani chuki na utengano vikikutawala maisha yako,kutegemea urafiki na msamaha ni upuuzi mtupu.
Nani anamfikiria mwenzake,namtazama mayu ameinama. Nakosa jibu, nakunja shuka naamka kwenda kutafuta kibarua. Siku mpya.

No comments: