Saturday, January 28, 2006

KISWAHILI: NI WAKATI WAKE SASA
Na: Obe M. Mashauri


Si lengo la makala haya kuwalaumu viongozi waswahili wanaotumia lugha za kigeni katika shughuli zao za kitaifa na hata kimataifa. Lengo la makala ni kutaka tu kuonyesha ni jinsi gani lugha hii iliyotulia kama maji ya mtungini ina uwezo wa kuwawakilisha viongozi hawa kwa kundi kubwa la wananchi wanaowaongoza katika dunia hii ya utandawazi.
Kati ya vitu muhimu ambavyo humtofautisha mwanadamu na wanyama ni lugha. Mwanadamu huyu ana lugha halisi ambayo humwezesha kuwasiliana na mwenzake sehemu mbalimbali. Kiswahili ni moja ya lugha nyingi zinazotumika duniani.
Kiswahili ni kitambulisho kikubwa kwa mtanzania na watu wote wa africa ya mashariki na kati. Ni lugha yenye utajiri wa kila kitu kwa ajili ya mawasiliano katika nyanja zote za maendeleo. Lugha hii inayojitosheleza katika shughuli zote za kiuchumi, utamaduni, siasa, elimu, sayansi n.k.
Kitendo cha mtu kuacha kutumia lugha yake kwa makusudi kabisa mbele ya watu wake ni utumwa. Ni utumwa kwa sababu mtu huyu atatakiwa kuiga mawazo ya wenye lugha anayoitumia. Kiswahili katika afrika mashariki ni lugha makini inayomfanya mtumiaji makini kujivunia na kuringa nayo.
Wakati wa ubaguzi wa rangi nchini afrika kusini, makaburu walikuwa na msemo maarufu usemao “lugha ya mvamizi ikiongewa na mvamiwa basi ni lugha ya mtumwa”. Hii ina maana ya kwamba wavamizi hawa walipofika pwani ya nchi hii(mwaka 1652 ),waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Utamaduni, mawazo na ustaarabu wao ulionyeshwa na lugha zao.
Wazungu wa rangi zote walipokuja afrika kwa madhumuni ya kupora utajiri chekwa waliwakuta wenyeji wakiwa na lugha zao. Lugha hizi weupe hawa waliziita eti ‘lugha za kishenzi’. Ni kwa kutozielewa lugha hizi ndipo wakaja na jibu la haraka na kutuita watumiaji wa lugha zetu washenzi. Tukawa watumwa wa lugha zao tena washenzi.
Utumwa huu wa kudharau lugha zetu bado ni donda sugu katika jamii zetu waafrika. Si ajabu hata kidogo kwa nchi zetu kukuta zimejigawa katika makundi yanayojiita: a) waongea kiingereza na hawa waongea kifaransa!. Bahati mbaya sana na waafrika mashariki tumeingizwa katika makundi haya ilhali tuna lugha yetu, kiswahili.
Makala haya hayana lengo la kudharau lugha nyingine au kuzibeza bali ni kuonyesha tu ni vipi kiswahili (kimeundwa na lugha za kibantu) kinaweza kutumika kusini, kati na mashariki mwa afrika. Sehemu hizi zina majimbo mengi yaliyozaa lugha ya Kiswahili. Mwanazuoni Malcon Guthrie anatoa ushahidi wa hili katika tafiti alizofanya katika karne ya 19.
Kiswahili kama kilivyo kiingereza ni mchanganyiko wa lugha mbalimbali zilizoko katika bara hili. Ndio maana wanazuoni hukiita Kiswahili kuwa ni kibantu sababu tu kinaundwa na maneno yanayoongewa na wakazi wa afrika.
Kwa mseto huu utaona ni jinsi gani lugha hii inajitosheleza kwa misamiati, nahau na mambo yote yanayohitjika katika kikwi hiki cha maendeleo.
Wengi tumekuwa tukikidharau Kiswahili kwamba si lugha ya maendeleo. Tumekuwa ni watumwa tukiaminishwa kwamba kiingereza tu ndio lugha ya kila kitu. Kasumba hii imegubika vichwa vya waswahili wengi kwamba bila kujua ‘kizungu’ wewe si kitu.
Utumwa huu tunao watu wengi tukifikiri kwamba ‘kizungu’kinajitegemea. Hakuna lugha inayojitegemea yenyewe mfano, kiingereza ni lugha yenye mchanganyiko wa maneno toka nchi mbalimbali zenye makabila tofauti.
Kiingereza kina maneno toka uyunani, hispania, ujerumani na uholanzi. Na hata watu wa kwanza kukiandika walikuwa ni waholanzi wa wakati huo waliokuwa na utaalamu wa kutengeneza mashine za kuandikia (taipuleta) maneno.
Pita siku moja sehemu wanakouza pombe na ujionee mwenyewe jinsi wasomi waswahili wasivyopenda kuongea lugha yao ya pili. Wanadharau lugha iliyofanya kazi kubwa ya ukombozi wa bara la Afrika.
‘Wasomi’ hawa hawataki kuongea lugha yao kwani wakiongea watajishushia hadhi yao ya usomi. Huku ni kuunda matabaka ya wanaojua kizungu (bora!)Na wasioongea kizungu (hasara?). matabaka haya yasipoangaliwa yatatugharimu.
Kiswahili kimejaza misamiati na maneno lukuki ambayo wasomi waliooshwa ‘bongo’kizungu hawaelewi. Watasema Kiswahili kinakosa maneno kama: television, computer, osamaphobia n.k. Hakika watu hawa hawajui maneno haya ni wapi yanatoka.
Hawana habari ya kwamba neno ‘computer’ ni matokeo ya maendeleo ya sayansi, ‘television’ ni neno linaloundwa na maneno mawili ya kigiriki yanayomaanisha kuona mbali. Ukiwaeleza kuhusu luninga, tovuti, asasi, wahanga, kikokotozi, king’amuzi watakushangaa na kukosa ulimi.
Jamii kubwa hasa walimu imekuwa ikitathmini akili ya mwanafunzi/mtoto kwa ufahamu wake wa kizungu, je anajua kizungu?. Hivi kizungu kukijua ndio mtu unakuwa na akili?. Huku ni kuchoka kwa mawazo ndani ya jamii yetu.
Wazazi nao hasa wa mijini wenye kipato wanashindana kupeleka watoto wao katika shule zinazotumia mitaala ya kizungu kufundisha. Huko Kiswahili wala utamaduni wa kiafrika hakuna mambo yote kizungu. Mtu asipoongea kizungu ni kweli hana akili? Kweli!
Kwa kudharau lugha yetu yawezekana ndiyo maana maendeleo hatuna. Mtu anasomea shahada ya ukulima morogoro, masomo hapa ni kwa kizungu. Mtu huyu huyu akimaliza masomo yake atakwenda kijijini kwa wakulima wasojua kizungu. Kilimo kitaendelea kweli ikiwa msomi huyu atatumia kizungu chake kufundisha!.
Wataalamu wapo ila lugha hazielewani. Hapa hakuna maana ya kwamba kwa kutojua kizungu wakulima wetu ni mbumbumbu wa ukulima.
Profesa Kihumbi Thairu katika kitabu chake ‘the africani civilization’anasema “nakumbuka mshtuko nilioupata miaka ya 50chuo kikuu cha Makerere, mwanachuo alimuuliza mhadhiri mzungu wa kitengo cha sayansi ya wanyama kwamba ni kwanini watu wanaanguka katika somo lake?
…Msomi huyu mzungu alitoa jibu fupi tu kwamba ‘kizungu’ wanachuo hawawezi kuandika kiingereza. Upofu wa mwanazuoni huyu bado unawaandama wasomi wetu wengi ambao hawataki kukubali kwamba kiswahili kinaweza kutumika na kutoa matunda mazuri kwa maendeleo ya jamii yetu na dunia kwa ujumla. Hata hivyo mwandishi hamlaumu mzungu huyu.
Kizungu kukijua hakimaanishi akili. Mmoja wa walimu wa kujitolea alipata nafasi ya kufundisha katika shule niliyosoma mkoani mwanza. Wakati aliporuhusu kufanya majadiliano ya somo alishangaa kusikia wanafunzi wakitumia Kiswahili.
Japo wachache walienda mbali kwa kutumia lugha ya asili (kisukuma) lakini wengi tulitumia kiswahili na mwalimu alifurahi kwani somo lake tulilifanya vizuri sana tena kwa kuandika kizungu.
Laiti wasomi na viongozi wetu wangekuwa kama mwelimishaji huyu hakika tungekuwa tofauti na wengine. Maana yake ni kwamba tungekuwa na maamuzi bora bila kutegemea mawazo ya lugha nyingine japo si vibaya.
Kiswahili kingetumika kama lugha ya kufundishia mashuleni basi kiwango cha kufaulu kingekuwa ni kikubwa tofauti na sasa. Wanasaikolojia wanaamini mtu anayefundishwa kwa lugha yake mwenyewe anaelewa zaidi tofauti na vinginevyo.
Hivi majuzi wizara ya elimu ilikataa kusajili shule tatu ambazo zingetoa elimu ya sekondari kwa kufundisha masomo yote kwa kiswahili (gazetila kiswahili la tarehe 17/01/2003). Sioni mantiki ya shule hizi kukataliwa ikiwa wenye kumweka madarakani waziri ni wananchi wanaotaka kufundisha kwa lugha ya taifa lao.
Kuruhusiwa kwa shule hizi si tu kwamba kiwango cha kufaulu kitapanda ila matabaka ya wanaojiona ni bora kwa vile wanaongea kizungu yatatoweka na wote tutapata taarifa sahihi zilizoandaliwa kwa umakini na kwa uwazi. Kiwango cha kufaulu kikiwa kikubwa na shule, vyuo vikawepo maendeleo hayaepukiki.
Watanzania hatupendi kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha yetu ya taifa. Makabati yetu yamejaa vitabu vya waandishi wa kizungu hata kama ni hadithi za watoto. Vitabu vilivyoandikwa Kiswahili havina nafasi kabisa.
Wengi hatujui kwamba sasa Kiswahili ni lugha rasmi katika shughuli za Umoja wa Afrika. Ili kiweze kuwa na nafasi katika umoja huu ni budi watumiaji wa lugha hii kuitumia kila mahali ili wengine nao wafuate ili kujifunza.
NINI KIFANYIKE
Lugha hii ni ya kiafrika zaidi kutumika katika umoja huu (AU). Hakuna asiyeelewa shughuli pevu iliyofanywa na kiswahili katika ukombozi wa karibu bara lote la afrika. Hivyo ni stahili yake bila maswali kuwa lugha ya bara zima.
Viongozi wa karibu nchi zote zinazoongea lugha hii(japo kidogo)wasisitize matumizi ya kiswahili katika nchi zao ili kuondokana na kasumba ya kutaka tu mawazo yanayotolewa kwa lugha ngeni.
Mabaraza ya Kiswahili yaundwe kila nchi kama ilivyo kwa nchi za Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda pamoja na nchi nyingine. Mabaraza haya kweli yafanye kazi ya kukieneza sehemu mbalimbali duniani.
Katika umoja huu wa afrika matumizi ya lugha hii yatiliwe mkazo si kama azimio lililoamua kutumika kwa lugha hii kule Madagascar lilivyozembewa. Viongozi waafrika waliacha na kufanya lugha zisizo na asili ya afrika kuamua mambo yao.
Ni furaha iliyoje kwa mtu aliyekukuta ukiwa na lugha yako akaiita kuwa ni ya kishenzi, akiwakuta leo mkiongea kwa lugha yake. Nina hakika atasema ‘nisingewatawala watu hawa wasingeweza kuwasiliana’!
Ni kweli kwamba kazi ya kufasiri vitabu kutoka lugha moja kwenda nyingine ni gharama kubwa kwa nchi zetu. Serikali kupitia mabaraza yake ni budi ifanye kazi hiyo. Watu tumechoka kukariri pindi tufundishwapo. Tufanye kile tutakacho sio wao watakacho.
Wananchi ndio wanaowaweka viongozi madarakani kuwaongoza na si kuwatawala, hii ndiyo demokrasia. Viongozi hawa ni wasomi, baadhi wapenda kutumia lugha zisizoeleweka kwa jamii kubwa.
Kwa hapa Tanzania hotuba nyingi zinazotolewa na viongozi wetu ama nje au ndani zinachefusha, hazieleweki kwa wengi, yaani zimeandaliwa kwa lugha ya kigeni. Kuwa kiongozi bora si lazima ujue kizungu japo si vibaya.
Tuige mfano wa kiongozi mmoja maarufu barani kwetu ambaye alisema kwamba anaongea kizungu ili tu wasiojua lugha yake wamwelewe na si kutaka sifa kwamba ni kiongozi mzuri, makini. Uongozi bora sehemu yoyote hauonyeshwi kwa viongozi kuongea na kuhutubia kizungu.
Mwasisi wa taifa huru la India Mahatma Gandhi aliwahi kusema kwamba katika eneo analotoka ni vizuri akatumia Kigujarati kama lugha ya kiserikali. Huyu ni msomi aliyezunguka nchi nyingi kutafuta elimu, masomo yake mengi aliyasoma kwa lugha zilizokuwa zikimpa shida kuelewa. Uamuzi wake wa kuamua Kigujarati kiwe lugha kuu katika India kunaonyesha uwajibikaji.
Katika dhifa za kimataifa walizofanya viongozi wa mashariki ya kati hapa nchini, hotuba zao zilitolewa kwa lugha zao. Ajabu viongozi wetu walitoa hotuba kwa lugha ya kizungu. Si vibaya nikifikiri kwamba wageni hawa walituona sisi ni vichaa.
Kituko kingine kilijitokeza wakati wa ufunguzi wa jengo la utalii hapa nchini. Kulikuwa na ulazima gani wa kutumia lugha tusiyoielewa, huku ni kutufanya sisi watumwa. Pamoja na utalii, sifa yetu nyingine ni lugha yetu.
Waandishi na watunzi wa kiswahili ni watu muhimu kwa ukuaji wa lugha hii. Ni budi wakitumie Kiswahili katika kazi zao bila kukipindisha. Wanamuziki na wasanii nao watoe kazi zao kwa ubora na umakini wakitumia lugha ya hadhira yao.
Watanzania sasa tujenge kasumba mpya ya kujisomea vitabu vyetu. Tununue vitabu ili kuwapa nguvu wachapishaji na watunzi waweze kufanya kazi za kiswahili bila kinyongo.
Sisi ni matajiri, tumebarikiwa kila kitu lakini kutokana na kudharau utajiri wetu ikiwemo lugha, tumekuwa ni wajima. Sifa yetu kubwa ni umaskini. Wakati fulani madiwani wa mkoani Mwanza waliandikiwa taarifa fulani na ‘wataalam’kutoka ‘PWH’taarifa iliandikwa kizungu. Wakapelekewa madiwani waswahili ‘wengi’. Ili uwe kiongozi hapa Tanzania ni lazima ujue kusoma na kuandika! Kwa ‘ripoti’ hii ya eti ‘wataalam kwa vile wameiandika kizungu’ nina uhakika asilimia 85 ya wawakilishi wa watu walikaa kimya katika kuijadili. La kujiuliza hapa ni hili, hivi sisi nani ametoroga ?
Tunathamini mawazo kutoka nje ambayo lengo lake ni kutuibia. Tukitumia lugha yetu katika mambo yetu tutakuwa tumeondokana na utegemezi wa mawazo kutoka nje.
Kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwa kila mtu zitolewe tuzo nia ikiwa ni kuenzi kazi zilizofanywa na watu waliokipigania kiswahili. Tuzo kama za Ibn batuta, Jumbe Akilimali, Shaaban Robert, Mnyampara na wengine wengi zitatoa changamoto kwa watu kutumia lugha hii.
Kuondokana na utegemezi wa kila kitu katika jamii yetu kumo ndani ya mikono na akili zetu. Kutumia lugha yetu hakuhitaji mzungu kutushauri. Ni wakati wa Watanzania na waafrika kuamka. Tutumie lugha ambazo ni za kiafrika zaidi.
Kujikana kwetu na kudharau na lugha yetu kunatufanya sisi tunaojiona bora (kwa kuongea kizungu) kuharibu hata hizo lugha tunazozikumbatia. Si jambo la kushangaza kumkuta mtanzania anyejidai na kizungu anashindwa kuongea kwa ufasaha lugha hizi za wakoloni.
Maendeleo tunayoyahitaji watanzania yawezekana hata kama tutatumia lugha yetu. Haiingii akilini mtoto anafundishwa lugha ya Kiswahili shule ya msingi tu na akiingia sekondari basi kizungu mtindo mmoja, huku ni kutuchanganya sisi vijana. Tunashindwa kuhoji, kwani Kiswahili hakina nafasi.
Suala la kutumia Kiswahili katika shule na vyuo vyetu halihitaji siasa. Wakati umefika kwa watu wote kuamka na kwa kauli moja kusema sasa ni wakati wa kiswahili.
Utamaduni wa wenye madaraka kutoheshimu matakwa ya wananchi ndio uliomfanya mwenye dhamana ya kusajili shule kuzinyima usajili shule hizo tatu nilizoongelea hapo juu. Nina uhakika kama ni wazungu ndio wangeomba kusajili shule hizo basi kusingekuwa na matatizo, wasomi wanaopenda kiswahili kitumike wanachukiwa.
Sababu kubwa ya kuchukiwa kwa wenye busara hawa ni labda kama kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia basi watapata pesa ya kufasiri vitabu kuwa katika kiswahili. Huu ni upofu wa fikra, hoja hii wala haina mashiko, taifa tulitakalo ni lile linaloona mbali si lenyo watu wanaoona umbali wa pua zao tu.
Serikali inadai kwamba inatoa nafasi kwa wananchi na asasi mbalimbali kutoa mawazo yao ili kuleta maendeleo. Mtazamo huu ninashindwa kuuelewa nikifiria kuhusu kubanwa kwa kiswahili katika kuleta maendeleo.
Tafiti zilizofanywa na Mlama na Materu mwaka 1976 mpaka 1977 zilibainisha kwamba lugha yetu ya taifa itumike katika sekta nzima ya elimu. Mradi wa kuboresha ufundishaji wa kiingereza uliandaa ripoti ya utafiti uliofanywa na wazungu mwaka1991 na kuainisha kuwa bado wanafunzi hawaelewi wanapofundishwa kizungu na wakapendekeza kizungu kifundishwe vizuri tangu shule za upili. Ripoti hii inaonyesha ni jinsi gani watafiti hawa waligundua kwamba kiswahili ndiyo lugha muhimu ya kufundishia katika nchi hii.
Uelewa mdogo wa mambo na elimu baguzi inayotolewa nchini unasababisha tukose wagunduzi na wataalamu mbalimbali katika nyanja zote muhimu kwa maendeleo yetu. Lugha zinazotumika kufundishia ni ngumu. Zinahitaji mtu ukariri na si uelewe. Unategemea nini kwa mtu asiyeelewa?
Viongozi wetu waandamizi nao ni vizuri wakatumia lugha hii ili tusichanganyane. Kitendo cha kutoa hotuba au miswada kizungu ni kutuminya wenye nchi tusihoji na hasa ukizingatia wengi tuna elimu ya msingi kwani sekondari ni chache na ghali. Wadau wote tupate kuhoji na kuelewa kwa lugha yetu sio kwa kizungu tusichokielewa. Hakuna haja ya kuibiana eti kwa kuwa tu sisi wengi hatujui kizungu. Uchumi wetu na maendeleo yetu ni budi tuyaelewe kwa lugha yetu ili inapobidi tuhoji.
Mpaka sasa sina uhakika kama watanzania tuna kitu kinachotutambulisha kwa wenzetu zaidi ya wimbo wa taifa ambao nahisi kuna watu wanatamani ungekuwa unaimbwa kizungu. Huu ni wakati muafaka wa kiswahili kutumika katika Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Maneno yaliyosemwa na mkuu wa chuo kikuu cha Mzumbe wakati wa ufunguzi wa chuo hivho mwaka jana kwamba wataanzisha utoaji wa elimu ya juu kwa kutumia lugha ya kiswahili ni changamoto kwetu. Hii ya kusikia tu kwamba Libya wanafundisha Kiswahili katika vyuo vyao ni aibu kwetu. Tuamke viongozi wa tanzania, kiswahili si wakati wa kampeni tu.
Inauma sana pindi unapotaka kupata habari juu ya kitu fulani habari hiyo unashindwa kuielewa kisa tu lugha iliyotumiwa kwa kumbukumbu hiyo ni ile isiyoeleka kwako. Hivi Kiswahili hakiwezi kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu jamani, au tunashobokea vitu tu. Nafasi ya lugha yetu katika kuhifadhi nyaraka na uhakika ni kubwa, nzuri na ya kudumu.
Hapo juu nimeongelea kwamba Kiswahili si wakati wa kampeni tu kwa viongozi wa tanzania. Watu watumie lugha hii hata kama wamekuwa viongozi. Hivi inakuwaje, unaomba kwa lugha moja na kutenda watenda kwa lugha nyingine wapi na wapi? Hii ndiyo inayotokea nchini kwetu kama huamini na haujaona mimi sina vidhibiti. Vya nini wakati ambapo hata hiyo lugha inayotumiwa siielewi, japo nikiielewa si vibaya.
Inasikitisha kuona waafrika tumesahau utu wetu na hatutaki kuulinda tena, uzungu umetuingia. Tunataka kujionyesha kwa wazungu kwamba sisi ni watu bora kwa kuiga kile wakifanyacho. Tunaiga hata jinsi wazungu wanavyoongea. Tunakwenda wapi sisi waafrika na tunalipeleka wapi bara hili tajiri. Lugha yetu ni budi tuipe heshima tusiivue nguo na kuiaibisha. Kiswahili yafaa kitumike katika shughuli zote za kila siku tuzifanyazo.
Napingana na kauli ya mhadhiri wa lugha za kigeni ya chuo kikuu cha Dar es Salaam aliyoitoa katika gazeti la ‘Sunday Observer’ la tarehe 19/01/2003. Msomi huyu M. Kadeghe anasema kwamba “wazazi wa Tanzania wanajua umuhimu wa Kiingereza katika kipindi hiki…” Kauli ya msomi anayeamini kizungu ndiyo uelewa!
Kutumia Kiswahili katika vyuo vyetu hakutatuweka kando katika kipndi hiki cha kutafuta maendeleo. Hivi nchi kama Japan, Italia, Ujerumani na nyingie zimemudu kupata maendeleo kwa kutumia lugha zao, kwa nini sisi na Kiswahili chetu tushindwe? Nchi hizi zote zinatumia lugha zao na kiwango cha maendeleo zilizonayo zinashinda hata zile nchi ambazo ‘msomi wetu’anazifagilia.
Kauli hii pamoja na ile iliyotolewa na waziri wa elimu ni moja ya kauli zisizofaa kutolewa na watu kama hawa. Watu hawa pamoja na wengine wenye dhamana katika nchi wanatakiwa kutoa kauli zenye busara, walizozifanyia utafiti wa kina na si mjini na kwa watoto wao wanaosoma katika shule za ‘…akademia’. Waende hata kule Mwabayanda, Mpitimbi na sehemu nyingine za vijijini kufanya utafiti na tuone watarudi na ni lugha ipi ifaayo hapa kwetu katika kipindi hiki.
Dk. Kadeghe ni mwalimu wa lugha, alifanya utafiti mwaka 2000 na kuweka wazi kuwa lugha hizi zote mbili zitumike katika ufundishaji lakini mtafiti mwingine Mwinsheikh aliweka wazi kuwa lugha ya kizungu ifundishwe kama somo tu, na masomo mengine yafundishwe kiswahili.
Kwa kutumia taaluma yake ya ualimu toka shule ya msingi mpaka chuo kikuu dk. Kadeghe anaelewa ni jinsi gani mwanafunzi anaelewa somo analofundishwa na kukariri somo analofundishwa. Haiitaji ‘PHD’ kujua kwamba mtanzania anayefundishwa kiswahili anaelewa zaidi kuliko mswahili anayefundishwa kizungu ambaye hakuna anachoelewa zaidi ya kukariri. Usitegemee swali kwa mtu anayekariri.
Lugha ‘ya kizungu’ hawa imefundishwa shuleni na vyuoni kwa karibu miongo minne sasa na hakuna kilichobadilika zaidi ya kuwepo makundi tu. Haijatusaidia kutatua tatizo la kilimo cha kutegemea mvua n.k. Tukipe nafasi Kiswahili na tuone kama hatujawafukuzia Wajapani. Wengi mtaona kama ninaota lakini ni kweli kwamba mtu akifundishwa kwa lugha yake huelewa zaidi na si kukariri.
Wengi mtasema kwamba mbona hata hicho Kiswahili kinachofundishwa wanafunzi wanashindwa kufaulu. Jibu ni rahisi tu kwamba kiswahili hakijapewa nafasi kubwa katika masomo, vijana wanaona ni bora kukariri masomo ambayo karibu yote ukiacha kiswahili yanafundishwa kizungu.
Masomo yakiendeshwa kwa lugha yetu nina uhakika maendeleo yatakuwepo kwani utafiti uliofanywa na Mwinsheikh ulitanabaisha bayana kwamba masomo ya sayansi (yanafundishwa kizungu!) yakifundishwa kiswahili wanafunzi wanaelewa zaidi. Sasa kama mtu anaelewa somo analofundishwa kwanini asivumbue vitu. Ukielewa kitu tabia ya kukariri waliofanya watu wengine itakwisha kwani mtu utavumbua chako.
Kompyuta sasa ni kitu ambacho wengi tunakiona ni kwa ajili ya ‘wateule’wanaojua kizungu. Hii si sawa. Mungu awazidishie nguvu na maarifa wataalamu wanaoweka ‘program’ za kiswahili katika chombo hiki cha kurahisisha kazi. Wote tutaweza kutumia na kupata vitu mbalimbali vitakavyoleta unafuu katika jamii zetu.
Kizungu na lugha zote za kizungu ni bora zikawa kama masomo ya kawaida tu. Ikibidi vyuo vya kufundisha lugh viongezwe ili kurahisisha mawasiliano kwani marafiki zetu wa Ulaya na sehemu nyingine si wote wanajua lugha ya ‘malkia’
Kuiga vitu kunafanya muigaji awe kama mtumwa, mtumwa ni yule mtu anayefanya kitu asichopenda kufanya. Hata kiongozi asiye na msimamo wa kuamua mambo mazuri hatoki ndani ya kundi hili. Kiongozi ni budi aongoze kwa matakwa ya jamii yake.
Hivi hatuna washauri wazalendo ambao ni wataalam wa mambo mbalimbali. Nani ameturoga yaani mpaka mshauri wa kujua nini tunataka atoke ‘uzunguni’ nje.
Kwani kiswahili kutumika mahakamani haki haitatendeka? Hapana
Kutumia lugha yetu shuleni na vyuoni ni dhambi? Hapana
Kiswahili kutumika kwenye makongamano no kosa? Hapana
Je, bila kuongea kizungu mtu anaonyesha kwamba hana akili? Hapana
Tunahitaji washauri wazungu ili watueleze kwama tutumie lugha yetu? Kwa hili jibu zuri laweza kutolewa na viongozi wetu wanaoamini mshauri anayetoa ushauri wake kwa kiswahili si msomi.
HAKUNA HAJA YA KUIGA KILA KITU KUTOKA NG’AMBO
Na: Obe M. Mashauri


Kuiga kitu ni ile hali ya kufanya kitu kwa kuona vile mwenzako alivyofanya. Ni kitendo ambacho huwa kinafanyika kwa siri lakini baadaye mgezaji huonekana na mwanzilishi hujulikana na kuheshimiwa.
Si vibaya kugeza kitu ambacho kitaweza kuleta unafuu fulani katika jamii. Mfano, kuiga ufundi wa kutengeneza trekta ni kuzuri kwani kutaleta unafuu kwa jamii ambayo muigaji anaishi. Kuiga teknolojia nako hakuepukiki kwani wote wanajamii wanahitaji teknolojia kwa maendeleo yao.
Kuna mambo mengine ambayo mtu ukiiga wenye busara zao watakuona punguani, chizi. Uigaji huu wa kishenzi mara zote hushusha utu wa muigaji, japo yeye hujiona ameendelea kwa kuiga hata vile vinavyopingana na utamaduni wake.
Utamaduni ni yale mazoea ya kale yasiyobadilika wala kugeuzwageuzwa. Kila mtu ana utamaduni wake ambao ameurithi toka kwa waliomtangulia kuona jua. Taifa nalo lina utamaduni wake. Wazungu wanao wao, waarabu pia, nasi waafrika tuna utamaduni wetu ambao tumekuwa nao kwa miaka mingi tu.
Inashangaza sana kuona waafrika tumekuwa ni mabingwa wa kuiga tamaduni za ng’ambo. Utamaduni wa mwafrika unapotea na sasa kinachonekana ni ule ustaarabu wa ng’ambo. Fahari yetu tunaizika na kukumbatia vitu tusivyovielewa mwanzo na wapi vinakwenda, sisi tunachojua ni kuiga tu.
Hapa sina lengo la kuongelea uigaji wa sayansi na teknolojia au vitu vya namna hiyo. Naongelea kuhusu utamaduni na ustaarabu wetu katika mavazi, maongezi na lugha, kula, mapenzi, dini na kuabudu. Vitu hivi waafrika tunavipoteza na kutokujali kwetu kunatufanya tuone vitu vyetu ni vya kishenzi.
Vijana watanzania wa karne hii tumekuwa ni mabingwa wa kuiga karibu kila kitu kinachofanywa na wazungu hasa wa Ulaya na Amerika ya kaskazini. Mitindo ya uvaaji, kuongea, kutembea na mingine tunaiga toka pande hizi.
Vijana ambao wengi tumebahatika kupata elimu japo kidogo tumekuwa ni mabingwa wa kuiga karibu kila kitu kutoka ‘majuu’ kwa mabepari hawa waliondelea. Haishangazi kukuta siku hizi vijana wanashindwa kuongea lugha zao za kuzaliwa au lugha yao ya taifa kuibolongabolonga.
Kijana anataka na anapenda kuongea lugha ile mzungu aongeayo si kwamba kijana huyu hana lugha yake, ni kule kutaka kujionyesha kwamba amesoma na kuongea lugha yake anaona ni kujishushia hadhi!
Ukitazama mahojiano yanayofanywa katika luninga na redio zetu utakuwa shahidi wa kuona vijana wanavyoikologa lugha yetu. Wanaongea ‘kiswa-nglishi’lugha isiyoeleweka kwa urahisi kwa jamii kubwa. Sasa sijui huku ndiko kutafuta maendeleo.
Kwa suala hili sitaki niamini kwamba kuelimika kwa mtu mweusi ni kuacha kuongea lugha yake. Kuelimika kwa mtu ni safari ya mtu huyu kuleta mabadiliko katika jamii yake na si kuharibu ustaarabu wa jamii yake.
Lugha yetu (ukiacha lugha zetu za kwanza)ya taifa ni muhimu sana kwa kila mtu wa nchi hii kuiongea kwani ni kitambulisho cha utaifa wetu. Inashangaza sana tunapong’ang’a na lugha tusizozijua vizuri kana kwamba hatuna lugha inayotuunganisha.
Tunaonekana ni watumwa kwani hapa mataifa yenye lugha tunazozing’ang’ania yajiona kama ndio yametusitaarabisha. Wakoloni walitukuta na lugha zetu na nyingine kubwa tu zilizotuunganisha. Swali hapa je, wasingekuja wakoloni na wafanyabiashara ya watumwa sisi tusingeweza kuwasiliana?
Ni jukumu la kizazi hiki cha vijana kujitoa muhanga kuhakikisha kwamba ustaarabu wa mwafrika hauharibiwi na vitu vya kishenzi kutoka ng’ambo. Kuongea lugha yako hakumfanyi msomi mswahili apoteze usomi wake ila kutamfanya aiboresha lugha hii iendane na wakati bila kuiharibu.
Majina yetu ya kiafrika sasa tunayakataa, tunayaona kama mkosi fulani. Tunatamani na tunataka tuitwe kwa majina ya kizungu ili tuonekane wastaarabu na hata tusio na dhambi. Nilihudhuria misa katika kanisa moja la Tabata college, mchungaji aliyehubiri alisema kwa watu kuitwa majina ya babu na bibi zetu waliofariki basi tunarithi hata dhambi zao! Huyu ni mtu anayechunga kondoo wa Bwana anayeamini majina ya koo zetu ni laana!
Majina tunayoyatamani ni yale ya wapelelezi na maharamia wa kizungu au wa kiarabu waliokuja kunyanyasa na kutuharibia nidhamu yetu. Mtu akiitwa kwa jina la ukoo wake si ajabu kuulizwa kama hana jina jingine la kikristo au kiislam! Majina ya kizungu au kiarabu tunayaona kama ni majina ya kistaarabu, yasiyo na dhambi kama anavyoamini mchungaji huyu. Tunatamani kuitwa majina ya watu wauaji, waasherati na mengine ya waovu kisa tu yameandikwa kwenye vitabu vya dini.
Suala jingine ambalo tumekuwa tukiiga sana ni dini na ustaarabu wa kuabudu. Itabidi ikumbukwe kwamba kabla ya wakoloni kuja, waafrika walikuwa na bado wana dini zao na ustaarabu wao wa kuabudu. Walikuwa wote wakimwabudu Mungu mmoja ambaye alikuwa akijulikana kwa majina mbalimbali lakini ni yule yule. Kuna walomwita Mulungu, Ngai, Katonda na majina mengine kutokana na lugha zao.
Bahati mbaya sana mawazo yetu yamegeuzwa ili kukubali kile mkoloni alichokuja nacho ili kututawala, ametupa dini yake. Tuna meza chochote kile anachotafuna na kutema vitamu vyetu na kuviita vya kishenzi, havifai kwetu sisi!
Wakoloni(mzungu na mwarabu) walikuja na kudai kwamba Mungu wao ndiye wa kweli. Mungu wetu waafrika, wakoloni wamemlinganisha na shetani na roho wake wameitwa mapepo! Kwa kutojua malengo ya wakoloni tumeacha dini zetu na kukumbatia dini mpya. Zinazotukana asili yetu.
Ni uongo wenye kutu kwamba waafrika hatukuwa na dini wala hatukumjua Mungu kabla ya wazungu na waarabu kuja kutupora utu wetu na kumtangaza ‘mungu’ wao! Kwa kulishwa ujinga na wakoloni hawa waafrika hatujui kuhusu Osiris mtu aliyeishi Misri (KK)aliyekufa na kufufuka. Huyu alikuwa akiabudiwa sana huko Misri
Ukristo ulipoletwa na wamisionari ulikuwa na jukumu la kuwa fundisha wenyeji imani chovu ili watawale bila maswali. Uislamu nao uliletwa ili tu kutimiza matakwa ya wachache waliokuwa na uchu wa kutaka kutawala. Wanadini wote hawa hawakufundisha theolojia ila tu walifundisha imani haba ya kutokuhoji. Tumebaki kuwa mabingwa wa kutetea dini hizi bila kuzijua malengo yake.
Dini hizi ngeni watu wanaziona ni bora sana na kuwapa majina ya kishenzi wasiozifuata. ‘Wapagani’ na ‘makafiri’ ni matokeo ya dini hizi zinazoonekana kama za wasomi wasiohoji. Dini hizi mara nyingi zina shawishi na kupenda vita, na kubaguana hizi ndizo tunazozikumbatia tukibusiana sisi kwa sisi!
Fujo nyingi zinatokea barani kwetu, sababu kubwa ikiwa ni dini hizi kutaka aidha kujitanua au kujionyesha kwamba ni bora. Mbaya zaidi maafa haya yanawakumba hata wasiozifuata. Mambo haya hayakuwahi kutokea na wala kuletwa na dini za mababu zetu zilizohimiza kujituma, nidhamu na upendo kwa watu wote. Sasa hapa tujiulize dini ipi ni bora
Kwa kutambua ukweli wa mambo kuhusu uafrika sasa baadhi ya wanateolojia akiwemo ‘fadha’ Mwanampepo wana kitu kinachojulikana kama ‘Kuitamadunisha Injili’ na kadri siku zinavyokwenda basi ni dhahiri kabisa waafrika watarudi kwenye dini zao zisizoshawishi mauaji na zisizotaka matabaka na kubaguana
Msomi Russell aliwahi kusema mwanzoni mwa miaka ya 1940 kwamba “mavazi na mitindo inayoonekana Ulaya mwafrika huiga bila kujiuliza na kwa imani yote”. Ukitazama kwa umakini utaona kwamba mavazi yetu waafrika yanaendana sana na hali ya hewa ya bara letu. Mavazi yetu ni mazuri kwa hali yetu.
Tunaiga uvaaji ambao si tu kwamba unatutesa kwa joto lililopo kwetu bali unatufanya tusionekane wastaarabu kwa jamii yetu. Sehemu nyigi za bara la Afika ni za kitropiki, joto haliepukiki. Kutokana na kuiga mavazi na uvaaji kutoka ng’ambo utashangaa kukutana na ‘msomi’ mchana wa jua kali akiwa amevaa suti kali na nzito. Joto na suti kweli jamani au ni kuiga tu. Jasho mwili mzima!
Mavazi ya vijana ndiyo yanayochosha zaidi. Kijana mzuri wa kiume unakuta amevaa sarawili ambayo ameivalia chini ya kiuno eti wanaita ‘kata K’ na anapita barabarani akitembea kwa madaha. Watoto wa kike nao suruali zinazobana na vijinguo vinavyoonyesha kitovu na ‘upindo wa kufuri’ ndiyo vimekuwa fasheni. Mavazi haya si tu kwamba yanadhalilisha bali yanashawishi na kuongeza hamu ya ngono ambayo madhara yake tunayajua kwa maendeleo ya taifa na bara letu.
Mavazi haya tunayoyaiga hasa sisi vijana hayafai na yanashusha hadhi ya kijana katika jamii yake. Kijana wa kiafrika ni mtu muhimu katika kuleta maendeleo ya jamii yake. Ni budi akajiheshimu kwa kuvaa nguo zinazomsetiri na kumwonyesha kwamba ni mstaarabu.
Kwa kutovaa mavazi mazuri yenye staha vijana wengi wamejikuta wanagharimika aidha kwa kuhisiwa ni wezi au malaya. Mavazi mazuri na uvaaji ulio sawa humjengea mtu hata kama ni mgeni kupata mapokezi mazuri ya kirafiki. Ni mara chache sana kwa mtu aliyevaa vizuri kuhisiwa kwa wizi au uchangudoa barabarani (japo wapo wanaovaa vizuri na wanatabia hizi.
Mwaka 2002 tumeshuhudia kuzaliwa kwa Umoja wa Afrika. Karibu viongozi wote wake kwa waume walihudhuria wakiwa wamependeza sana kwa mavazi yao mazuri. Wanawake walipendeza zaidi kwa nguo zao zilizowaonyesha kwamba hakika ni Waafrika. Hii ni tofauti kabisa kwa viongozi wanaume ambao (si wote) walikuwa ndani ya mavazi ya kimagharibi, suti nzito za gharama. Hivi kweli hatupenda kuvaa nguo zetu zenye kuonyesha fahari yetu!
Wengi wataona kama ni kukurupuka endapo mtu atasema ustaarabu wa binadamu ulianzia Afrika! Kuna ushahidi unaoonyesha kabisa kwamba kabla ya maharamia kuja kwetu( Afrika)maeneo mengi yalikuwa yamestaarabika kiasi kwamba majahili hawa waliiga ustaarabu wetu. Mwanahistoria Walter Rodney anathibitisha hili katika klitabu chake kinachoitwa ‘How Europe Underdeveloped Africa’
Suala jingine ambalo ni muhimu katika maisha ni urafiki na mapenzi kwa vijana. Tamaduni zetu waafrika ni tofauti na tamaduni za wazungu au waarabu, tunachopenda sisi si lazima wao wafuate na wakipendacho wao hawatulazimishi kufuata.
Ni ukweli usiofichika kwamba taifa bila vijana waadilifu si lolote. Vijana wakipotoka basi jamii itegemee kilio kwani hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana ikiwa nguvu kazi ni butu. Wazee ni muhimu kwa kuelekeza na kutoa ushauri na vijana ni watekelezaji wa shughuli zote za jamii.
Vijana wengi sasa wanakazana kuangalia tamthilia za kigeni zilizojaa maudhui mabovu kwa vijana wetu. Mara nyingi michezo hii huonyesha maudhui ya mapenzi kwa wahusika wenye umri mdogo. Nasi twataka kuiga kila sehemu ya tamthilia hii. Hadithi za mababu zetu hazina nafasi tena, sasa mambo yote ni luninga na video.
Mapenzi si kitu kibaya, kwani yalikuwako tokea mwanzo. Muhimu hapa ni jinsi mapenzi haya ya kuiga kwenye luninga yanavyolighalimu bara hili. Vijana wamejiingiza kwenye ngono(si mapenzi)wakiwa na umri mdogo kwa vile tu wameona mhusika kwenye tamthilia anafanya mapenzi ilhali ana umri mdogo.
Vijana tumekuwa si wakweli na mpaka mtu anapofikia umri wa kuoa tayari huwa na namba kubwa ya wapenzi aliokwisha fanya nao ngono. Hiki kitu hakikuwepo kabla na yeyote anayetaka kubishi aweza bishi kwa kuwa ubisha yaweza kuwa hulka yake. Kijana ana miaka 19 na tayari ana ‘wapenzi’saba. Hii inatisha!
Hapo juu nimesema kwamba kila mtu ana utamaduni wake, tamthilia, sinema na michezo ya kuigiza toka nje ya bara hili huonyesha utamaduni wa sehemu hizo. Kuiga kile kinachoonekana ni juu ya mtazamaji na akili yake.
Jamii zetu nyingi haziruhusu mapenzi kwa vijana waliona na umri mdogo. Ili kijana awe na mchumba alitakiwa kuwa na uwezo wa kujitegemea yeye mwenyewe, hii ina maana kwamba kijana anaanza kumjua binti wakiwa na umri ufaao kwa mapenzi na si ngono.
Ngono zisizo salama zinazofanyika kabla ya wakati zina madhara makubwa ambayo kila mwanajamii anayaona. Mimba zisizopangiliwa ni nyingi tu magonjwa ya zinaa sasa yanawakumba zaidi vijana wasiooa. Haya yote ni madhara ya kuiga.
Zamani vijana wote kwa jinsia zao walikuwa wakikaa na wakubwa zao na kupata nasaha mbalimbali kuhusu maisha. Kutokana na mwingiliano wa kijamii na mabadiliko ya kiuchumi kila mtu anahangaika kupata chochote, muda wa kuongea na vijana haupo na kama upo hautumiki ipasavyo. Ndivyo tunavyopotezana.
Kazi huonyesha utu wa mtu, yeyote asiye na kazi katika jamii huonekana mvivu na mnyonyaji wa nguvu ya jamii. Ni ukweli kwamba kwa sasa kuna tatizo kubwa la ajira na ukosefu wa mitaji. Hili ni jambo ambalo liko chini ya serikali na wananchi wake. Watu kukosa kazi ni tatizo ambalo linaangukia mikononi mwa watawala. Kukosa kazi kunafanya watu kuiga yale yanayoonekana kwenye sinema.
Wimbi la ukabaji na uporaji linaloonekana sasa katika mitaa yetu ni matokeo ya kukosa kazi na hivyo kuiga yale yote yanayoonekana kwenye senema za kimagharibi. Jambo hili ikiwa halitapatiwa ufumbuzi mapema basi kitakachokuja kutokea wakumlaumu atakuwa ni kiongozi aliye madarakani na watendaji wake walioshindwa kuona tatizo hili kwa kuwa wao wameshiba.
Ni vizuri tukiwa na watu tunaojitegemea na kujitawala! Tukawa ni watu wenye maamuzi ya kulinda na kuhifadhi historia na utu wetu. Ustaarabu na utu wetu tusiukane na kuuita wa kishenzi. Taifa au mtu asiye na utamaduni ni kama mti usio na mizizi (kama upo!).
Tamaduni, jadi, mila na utu wetu waafrika hauhitaji ‘rafiki’ mgeni aje kutoka nje atuambie sasa na tuache kuiga tamaduni mbovu kutoka kwa rafiki zetu.
Kulinda na kutunza kumbukumbu zetu hakuhitaji ushauri toka sehemu yoyote. Ni jukumu letu kulinda kilicho chetu na kuiga kile kinachotufanya tuonekane wapumbavu mbele za watu walioamua kuhifadhi vilivyo vyao.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi yasiwe chanzo cha sisi kupotoka na kutaka kudandia gari kwa mbele. Madhara yampatayo mtu anayedandia gari lililo kwenye mwendo nadhani kila mtu anayajua. Je, na sisi waafrika tupate madhara haya?
Jibu la maswali haya tunalo nalo ni rahisi sana, halihitaji kutazamia kwa ‘rafiki’ jirani. Uwezo wa kulinda utu kama waafrika umo mikononi mwetu na ni sisi kuamua tu kwamba HAKUNA KUIGA UPUMBAVU.
Kiongozi wa mapinduzi wa Libya amewahi kusema kwamba “mzalendo anayekula chakula kisichozalishwa nchini mwake huyo anaukana uhuru wa taifa lake”. Hii ilikuwa mwaka1984 katika kuadhimisha miaka 15 ya mapinduzi.
Kauli hii ina mashiko ikitafakaliwa kwa umakini ni kauli inayohitaji kila mtu atumie kile alichonacho bila kukidharau. Wote tukae chini na kukubaliana kwa kauli moja ya kwamba kuiga mambo yasiyoendana na sisi ni upuuzi.
Tuige vitu vitakavyoipatia jamii nafuu. Tuige teknolojia ambayo itatuondolea tatizo la kilimo cha kutegemea mvua. Viongozi wahakikishe pato la wanaye muongoza angalau lina eleweka. Ufisadi utokomezwe na watu/ wananchi waishi kwa raha na uhakika wa kupata mlo kamili.
Tuondokane na uigaji ambao huwafanya viongozi wajali matumbo yao tu. Tusiige ufisadi wa kuuza rasilimali zetu muhimu kwa wajukuu wetu. Tuwajengee wajukuu wetu uchumi imara ili wasije tuona kama hatukuwa na akili timamu. Tutunze vyetu ili watoto wetu wasiyachape makaburi yetu viboko kisa hatujawaachia msimamo thabiti.
KASS INAITWA THE MWALIMU NYERERE SASA


Ukiwa mgeni sasa na unategemea kuongozwa na bango utapotea kwani sasa vibao vya kukuelekeza kuwa uende na uingie vipi chuo cha sayansi ya jamii kivukoni maarufu kama KASS yamefutwa na hakuna maelezo yaliyotolewa si kwa umma wa wanachuo tu bali hata umma wote wa watanzania.
Lakini nikiwa kama mwanajumuia nadhani labda ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yanayotarajiwa hivi karibuni mara baada ya tangazola serikali. Tusubiri na nitakuwa nikikupatia habari zote juu ya chuo hiki adhimu kilichowahi kuwa chuo cha propaganda cha CCM kabla ya kuchukuliwa na serikali na kuwekwa chini ya wizara ya sayansi na elimu ya juu kinatarajiwa kuanza kutoa shahada

Monday, January 23, 2006

KAULI ZA VIONGOZI NA TAALUMA YA POLISI

Hakuna asiyejua kinachoendelea sasa baada ya kauli mbovu kabisa ya waziri wa usalama wa raia.
usalama wa raia si siasa ya kutamka tu kila unachojifikiria.
Vijana wanne wa kitanzania wanafungwa pingu na kupigwa risasi vichogoni mara tunatangaziwa kwamba majambazi hayo yalirushiana risasi na polisi, hivi inaingia akilini kweli!
Tutegemee vifo vingi vya 'majambazi' yaani sasa ukigombania demu tu na askari kosa waweza kuwa jambazi linalotafutwa kwa siku nyingi
UMEISIKIA MIPANGO YA WAAFRIKA

Mara zote vyombo vya habari vya mataifa ya Ulaya na marikani huwa haviripoti mazuri ya Afrika, hulionyesha bara hili kama bara linalokabiliwa na lililogubikwa na kila aina ya matatizoikiwemo umaskini na magonjwa.
Hii yaweza kuwa kweli lakini si kwamba hakuna mazuri yaliyo huku yanayopaswa kuripotiwa.
Sasa hivi karibuni huku Landani kumefanyika mipango ya kuanzisha tV itakayokuwa ikiripoti habari za Afrika kwa urari sawa kabisa.
Naomba wazo hili lifanikiwe na kuonyesha upande wa pili wa Afrika

Sunday, January 15, 2006

MWAPACHU v/s MAJAMBAZI


Kauli ya waziri wa Usalama wa raia wa Tanzania imesikiwa na kila mwananchi. kauli hii kutoka kwa waziri huyu ya kuwa Polisi wauwe jambazi ambalo linaonyesha dalili za kufanya uhalifu si ya kupita hivi hivi bila watanzania na raia wema wa nchi hii kuihoji, hivi kweli haki iatatendeka kwa jinsi tunavyowajua baadhi ya askari wetu wanavyotubambikizia kesi! na sasa wana rungu la kuuwa
Nadhani kuna wakati viongozi kama hawa wakawa na mtu wa kuedit kauli zao kabla hazijatufikia wananchi.
Tuikatae hii kauli kwani haifai na kama kauli ya mtu huyu haitufai basi naye tumwangalie kama anafaa kukaa mahli alipo

Thursday, January 12, 2006

SHIRIKI


Kuna mjadala sasa uko katika blog na unahusu ni neno gani la kiswahili linafaa kwa ajili yablog unaweza kushiriki kwa kutoa maoni yako

Wednesday, January 11, 2006

NANI KAWALOGA WAANDISHI WA HABARI!

Kichwa cha habari hata kisikuchanganye, mara nyingi siku hizi nimekuwa nishangazwa na waandishi wetu wa habari na hasa namna wanavyoripoti habari za mafanikio ya kiuchumi kwa watawala wa tanzania
Kinachonisumbua ni kuona kwamba utawala wa Mzee Mwinyi hauongelewi kabisa na kinachotukuzwa ni mafankio ya Nyeere na Mkapa kwisha.

Hivi ninyi waandishi mnajua namna maisha ya Watanzania yalivybadilika wakati wa mzee Ruksa au mnasukumwa na mapenzi binafsi kwa viongzi hawa, Hebu tizama hata daraja la Ndndu linaitwa daraja la Mkapa hii ni haki kweli?
Hivi ni nani anastahili pongezi kwa kuwepo kwa daraja hilo ni Mwinyi au Mkapa?
Hivi bila Mwinyi kumuibua rais wa sasa Kikwete kuna mtu angemjua kweli hebu tuache chuki binafsi kama ni suala a kukusanya kodi kidogo wakati wa ruksa mbona sasa kodi inakusanywa kubwa lakini hakuna kilichobadilika zaidi ya vitu kuwa juu na maisha kupanda kwa kila sehemu.
Sipendi niukubali msemo wa kwamba watanzania hatuna utamaduni wa kusoma si magazeti tu na vitabu lakini kama mwandishi hana falsafa kuna umuhimu wa kusoma kazi yake na hata kama anaiandika kwa mapenzi binafsi bla kujali nini jamii inafikiria
BADO NAIKARABATI


Najua kla mtu ana hamu ya kuisoma blogu hii, vuta subira kwani bado naikarabati
JE, DINI NA MUNGU WA WAAFRIKA NI MSHENZI?

Na: Obe Mashauri
Ni falsafa ya uongo kwa mtu kuamini kwamba waafrika hawakuwa na dini kabla ya kuja kwa wageni waliokuja kwa nia ya kupora utajiri wa bara hili.
Dini ni njia ya kuhusiana na Mungu. Kwa tafsiri hii ni uongo wenye kutu kusema kwamba kabla ya wazungu na waarabu kutuvamia tulikuwa watu wasio na diniau kwa lugha nzuri kwao nakwa wafuasi wao wa sasa, wapagani au makafiri.
Wengi wetu tumekuwa tukiamini kwa kuaminishwa kwamba dini zilizoletwa na wageni ndiyo dini za asili.ukoloni na utumwa wa maharamia hawa ulitufanya tuamini kwamba Mungu wa majangiri hawa ni wa kweli. Mungu aliyeabudiwa na wenyeji aliitwa mshenzi na mitume wake wakaitwa mapepo. Huu ndio ustaarabu wa wageni.
Baada ya kuwa zimejikita afrika kwa mabavu na propaganda, zimewajaza wafuasi wake falsafa mpya ya kujibagua na kujiona bora zaidi ya wengine
Tanzania na afrika kwa ujumla katika miaka ya hivi karibuni imeshuhudia vujo na migogoro mikubwa ya kidini inayoletwa na dini hizi za ukristo na uislam katika ama kujitanua au kujiona bora zaidi ya nyingine.
Mbaya zaidi migogoro baini ya dini hizi inawaathiri hata wasiozifuata. Mambo haya hayakuwahi kutokea kutoea kabla ya kuja kwa dini hizi za kigeni.
Historia ni shahidi wa mengi. Historia ya mwafrika haioneshi machafuko au vita vilivyosababishwa na dini za asili. Dini ambazo ‘wakoloni na mabwana’ waliziita za kishenzi huku waumini wake wakibatizwa majina kama wapagani,kaffir na majina mengine mengi ya kipuuzi.
Ukristo na uislamu ni dini za kibiashara zenye historia ya vita katika kujitanua. Itkadi ya dini hizi ilisambazwa kwa heri au shari kwao waliozikataa. Walikuwa wakimtangaza Mungu wao kwamba ndiye wa kweli na hapana mwingine ila yeye.
Ukristo na uislam uliokumbatiwa na waafrika uliletwa afrika si kwa minajili ya kumtangaza mungu wa kweli bali dini hizi zilikuwa ni mbinu za wazungu na waarabu kujitanua kiuchumi na kisisasa katika bara hili tukufu. Biashara ya utumwa na ukoloni vinadhihirisha haya.
Kwa mantiki hii utaona kwamba mungu anayehubiriwa katika dini hizi ni yule anayehalalisha uporaji na uuwaji wa watu wasiomtaka.
Uislamu ulisambazwa kwa upanga mkali uliokata shingo na viungo kwa wote walioukataa. Jitihada zilizofanywa na uthman dan fodio zinadhihirisha jambo hili.
Mabomu,mishale, risasi na uongo nazo zilitumika kuusimika ukristo na yule aliyeukataa aliitwa msaliti, kifo ni zawai yake.
Mtu aliyepingana na dini hizi aliuawa.
Falsafa iliyopandikizwa na wakristo na waislam vichwani mwa waafrika bado inatutawala mpaka sasa. Ukweli ni kwamba kila mtu ana Mungu wake anayeujua utamaduni wake na kila hali yake ya maisha ya kila siku.
Kwa waafrika Mungu huyu alijulikana kwa majina anuai, wapo waliomwita Ngai, Mulungu, Lyoka na majina mengine mengi yanayoonyesha utukufu wake.
Dini za kiafrika ziliabudu Mungu mmoja tu na si kwamba wageni ndio waliowaletea waafrika dini na kuwatambulisha kwa Mungu. Ustaarabu ulikuwapo afrika na wazungu na waarabu ndio waliokopi ustaarabu huu.
Dini za kigeni ziliudharau utamaduni wa mwafrika na kumtambulisha kwa utamaduni mpya wa kujidharau na kudharau kila kilicho chake, akiiponda dini yake na kukumbatia ukisasa eti huo ndio ustaarabu.
Kwa kuudharau utamaduni wake mwaafrika amekuwa kama kasuku, kazi yake ni kuimba kila anachopewa na bwana wake. Lugha za kiafrika karibuni zitatoweka kwa kuwa tu hazina nafasi katika dunia ya wastaarabu. Lugha muhimu ni kizungu na kiarabu tu.
Ukitaka kumtawala mtu basi mporeulimi wake. Majangiri hawa wamefanikiwa kwa hilo. Kwani kila mtu hata kuamini ukisema umetokewa na Mungu anayeongea lugha yako. Wao Mungu ni yule anayeongea kwa lugha zao,Mungu asyeongea lugha zao basi watamwita shetani kama ilivyotokea Joan of the Arc huko London. Kitabu cha the African civilization kinalieleza hili.
Mwanzoni mwa muongo huu watanzania tumekuwa tukishuhudia migogoro na fujo nyingi za kidini zikitokea na ukijaribu kuchunguza kwa umakini migongano hii imekalia katika maslahi binafsi ya dini hizi na si kumtangaza mungu wao.
Machafuko haya yanayotokea ndiyo yanayonifanya nijiulize kama kweli dini zetu zilikuwa za kishenzi?
Hivi matusi, vita, migongano na machafuko yanayotokea katika nyumba za ibadandio ustaarabu tulioletewa?
Hivi wageni hawa walituletea Mungu tuliyemjua sisi au mungu wao mpenda vita, mwenye wivuna mbaguzi? Je, ni kweli kwamba sisis hatukuwa na Mungu? Swali hili nisingependa waljibu wasomi waliokaririshwa kwamba cha mzungu na mwarabu ndio bora
Kama tusingekuwa na Mungu ‘wastaarabu’ hawa wangetukuta kweli? Moyo wa ukarimu tuliowaonyesha japo walitutemea mate, ulitoka kwa Mungu wa kishenzi kweli? Hivi Mungu wetu aliyetulinda na kutupa akili ya kumjua alikuwa ni Mungu aliyevaa ngozi ya kondoo.
Je, mungu aliyeruhusu wengine kupora,kutawala kwa mabavu na kuuza binaadamu kama bidhaa ndiye mungu wa kweli?
Maswali haya pamoja na hili linalosema kwamba ukristo na uislam ni dini za ulimwengu (universal) yananifanya nijiulize na kuchoshwa na hadithi za vitabuni.
Ukweli usiolazimishwa kuukubali ni kwamba dini hizi mbili si dini za ulimwengu kama tunavyopotoshwa. Kwa afrika dini hizi ni ngeni kabisa na hatukuwa na migogoro ya kidini kama tunayoishuhudia sasa katika dini hizi ngeni.
Ni wakati wa waafrika sasa kurejea katika imani ya asili tuliyokuwa nayo, imani inayotutambua sisi na utamaduni wetu. Turudi katika dini zetu ili tutunze ustaarabu wetu, utamaduni wetukila fahari yetu.
Dini zetu za jadi ndizo zitakazotuepusha na migogoro tunayoishuhudia sasa na kwa bahati mbaya sana tunaishiriki tu eti kwa kuwa tumebatizwa na kusilimishwa katika majina mapya tusiyojua maana yake.
Vilevile tujue dini hizi mwanzo wake na wafuasi wake wa mwanzo. Ukristo ulianzishwa na kikundi cha waalimu (rabbi) Yesu akiwa mwanzilisha wakati Uislamu ulianzishwa na mfanyabiashara aliyeitwa Muhamad aliyejiita mtume huko mashariki ya mbali na kuusambaza kwa vita akianzia huko Makka.
Kuzifuata na kuzikubali dini hizi ni kukubaliana na waanzilishi wa dini hiziz na misemo yao kama…ya kaisari mpe kaisari…., na bakora ndizo zitakazoleta usuluhishi kati yetu!
Kukataa kurudia dini zetu ni kukumbatia laana tulizopata kwa kuaminishwa kwamba waafrika hatuna Mungu
Ufumbuzi wa migogoro tunayoishuhudia katika dini za kigeni ni kurudi katika dini zetu za asili zinazotutambua kwamba sisi ni nani na ni kwa ajili ya nani.
Tumekuwa na tunakuwa wanyonge kwa kukumbatia dini hizi zinazotunyima uhuru wa kuhoji kwani mafundisho yake yanatumia lugha tusizozielewa na zinatokana na mawazo ya watu wenye utamaduni tofauti na wetu.
Tujiuliza kama zingekuwa ni dini za kweli mbona zinabaguana na viongozi wa dini hizi wanajiona wao ni bora kuliko waumini wake.
Ukweli hata ukipingwa haubadiliki kuwa uongo. Ukweli ukishindwa ni kama umesakafiwa tu na siku moja utaibuka na waliopinga wataficha nyuso zao kwa aibu
MAWIO
Na: Obe Mashauri
Ndani ya jela, siku huisha kama jana, funguo ikifunga malango,nafungiwa usiku. Tunahesabiwa kama bidhaa dukani, kitambo kidogo taa zinazimwa na tunalazimishwa kulala kama watoto wa shule.
Usiku unakuja polepole tena kimya kimya. Macho yanatazama dari refu mikono kufikia. Kila mfungwa yupo macho akisubiri saa ili afurahie amani kwa usingizi.
Huu ni wakati mgumu zaidi gerezani. Ni wakati mabao kuta za gereza zinakuliwaza.
Asubuhi unaamshwa mapema sana, unahesabiwa kama ng’ombe wanaopelekwa malishoni, unapangiwa kazi,unachapwa ukitegea hata kama umechoka. Hakuna kupumzika bwana afande anataka akuone unajishughulisha sio unakaa kama uko kwa bibi yako. Kichwani mawazo yamejaa, unasubiri usiku. Hakuna kitu zaidi ya ukimya na mawazo yako kichwani.
Navuta kirago changu, ni kitanda hiki. Baridi ni kali,blanketi lenyewe fupi. Anophelesi wanahimizana kutafuta chakula kwani vyandarua hakuna, sherehe kwao.nawasha sigara natabasamu nikifikiria nilivyoipata,moshi unawafukuza mbu. Siko peke yangu niliye macho, wanautazama moshi wa sgara ukutafuta uhuru darini.
Chumba kimetawalwa na furaha ya upweke, kila mtu yupo kimya. Uso wang’aa,moyo umegubikwa na majonzi,sauti haitoki kijana analia. Kuwezi kuisikia mnyapara anafanya mapenzi na kiherehere,wote wanaume. Kila mtu anataka aishi kikawaida apasipo ukawaida.
Natizama moshi wa sigara unavyopaa,nadhani sasa ni saa 8 usiku. Moshi unazidi kufata dari ukielekea kusikojulikana. Ni kama maisha yangu. Swali liko kichwani mwangu,najaribu kulifukuza kwa bangi, linarejea stimu zikiisha na msokoto umeisha. Swali kuhusu maisha, malengo yangu maishani, wapi mafanikio?
Shuka imechoka, ni fupi, miguu imekataa kukunjwa,baridi linanifariji, kichwa kimechanganyikiwa, maumivu, bahati mbaya, kuta nene ajabu na askari waliokumbatia mianzi ya kizungu.
Nalia ka mbogo, kimya kimya, machozi mishipani yanaondoa nguvu za nafsi. Najisikia hatia, je, nimezaliwa bila bahati? Mbona wengine wanafanikiwa hata kama kichwa changu ni bora kuliko wao. Wengine mwenyewe nachangia mafanikio yao, mbona mimi sibahatiki! Tajiri wa mikosi, natabasamu. Jana imepotea moja kwa moja, kesho ni mbali sana, kuijua ni kama ndoto ya mchana.
Najaribu kurejea ndoto zangu baada ya kukabidhiwa cheti cha kumaliza shule,chuo, nafikiria ofisi nilizopita kutafuta kazi. Namfikiria mke wangu anayependa mambo makubwa nisiyoweza kuyakidhi. Nachoka nikifikiria familia yangu,mama na jamaa zangu. Nachoka kama mtoto anayetambaa, nina kiu, Israel anatabasamu na kunionyeshea kamba iliyo pembeni mwa kirago changu. Nimefungwa muda mrefu kazi bila malipo na nimesoma.
Siko peke yangu, tuko wengi lakini najisikia mchovu, kuzeeka sio kuwa na umri mkubwa tu. Nimezeeka nikiwa kijana tena kijana mbichi. Mzee wangu amekuwa mlevi eti pombezinamfariji baada ya kukosa mafao yake ya iliyokuwa EAC. Kama wameutendea mti mkavu namna hii vipi kwa mti mbichi.
Nimechoka, nitaondokanaje na chaka hili, nitapataje kazi, wacha nisome nani atanilipia karo na serikali ina wenyewe!
Viongozi wajifunze maisha yetu wasione watoto wao wanatabasamu wakafikiri nasisi tuko kama wao.wengine tumefungwa na msamaha hauonekani, upendo hakuna bila pesa.ajira zisitoke kwa upendeleo
Nahitaji mabadiliko, nataka kuishi maisha bora, nahitaji kufanya mapinduzi. Naichukia serikali yangu. Mko wapi mliotoswa?
Nini nifanye nikomeshe upuuzi huu wa kujipendelea. Nafikiria kuua, nafsi inakataa kwani chuki na utengano vikikutawala maisha yako,kutegemea urafiki na msamaha ni upuuzi mtupu.
Nani anamfikiria mwenzake,namtazama mayu ameinama. Nakosa jibu, nakunja shuka naamka kwenda kutafuta kibarua. Siku mpya.
Mara baada ya mwanguko mkubwa wa uchumi huko Marekani mwaka1930, Marekani chini ya rais wake Roosevelt, ilianzisha mpango kamambe wa kufufua uchumi wake uliojulikana kama Marshall Plan.
Moja ya mipango mingi ya kufufua uchumi nchini humo ulikuwa ni mpango wa uliopewa jina la mabadiliko katika sekta ya kilimo chini ya sheria za nchi. Katika mpango wa ufufuaji na uboreshaji wa sekta ya kilimo mkazo ulitiliwa katika utoaji wa mikopo na ruzuku kwa wakulima.
Mpango huu ulipofanikiwa mara baada ya miaka mitano mafanikio yake ni haya tunayoyaona leo. Soko lote la bidhaa za kilimo marekani amelishikilia.
Tanzania na mamlaka yake imekuwa ikiimba kila siku tangu tupate uhuru kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa. Kauli mbiu na maazimio mbalimbali ya serikali yanasisitiza kuwa kilimo ndiyo kitaondoa umaskini katika nchi yetu.
Kwa ukweli hakika ni kuwa asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo na kiasi hicho cha watu ni maskini wanaoishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku. Idadi kubwa ya watu hawa wote wanalima mashamba madogo vijijini.
Ukiiangalia Tanzania na ardhi yake bora ambayo kwa kiasi kikubwa haijatumiwa kwa ukamilifu,ukaangalia na idadi ya watu waliomo utaona kwamba endapo kilimo kitapewa kipaumbele basi kilimo ndiyo silaha kubwa ya kukabiliana na adui, umaskini.
Mpaka sasa wakulima wadogo wa Tanzania hawajawezeshwa ili kuondokana na shuka kubwa walilofunikwa lililogeuka kuwa tunu kwao,umaskini. Kuwezeshwa huku kwa mkulima mdogo hakuwezekani kwa hotuba tamu za kwenye majukwaa ya siasa na semina kwa warasimu kilimo bila ushirikishwaji wa wakulima na utekelezwaji wa maamuzi.
Mkulima wa Tanzania anahitaji misaada mingi ili kumwezesha ambayo wenye mamlaka wakiacha u-mimi, mkulima mdogo wa nchi hii atainuka na hata kuweza kushindani katika soko na wakulima wa nchi nyingine ambako mkulima anathaminiwa na kupewa kila aina ya msaada.
Ili kumwezesha mkulima wa Tanzania haina maana ya kwamba mkulima huyu apewe fedha za bure. Hapa ninamaanisha kwamba mkulima wetu apewe mikopo atakayopaswa kulipa pindi uuzaji wa mazao unapoanza. Ni mikopo tu ndiyo iliyotumika na inatumika katika kuondoa umaskini kwa wananchi katika nchi kama Mali na nyingine.
Jitihada nyingi za kuleta maendeleo zinazoonyeshwa na serikali yetu zinafaa sana. Lakini kwa upande wangu pamoja na kujenga madaraja na barabara nzuri

NIMO NDANI YA NYUMBA

Najua kuna wengi wametangulia wakiwa na nia moja kubwa ya kutoa mawazo yao ili wengine wayaelewe na ikiwezekana wachangia kwa kadri wanavyoweza. Nami nachukua fursa hii ili niweze kushirikiana na wasomaji wengi. Najua mtanikaribisha