Wednesday, March 28, 2007

KILA MTU NI MPIGADEBE!!

Unapotembelea vituo vya mabasi na ama unapotaka kusafiri si ajabu kufuatwa na vijana wa rika la kati wakijitahidi kukushawishi kupanda magari yao, hawa ndio wapigadebe.

Sitaki ujenge picha ya hawa, lakini katika hali ya sasa hivi kila mtu amekuwa ni mpigadebe, sijui tunakwenda wapi. Kuanzia rais mpaka wenye NGO wote wanapigadebe sema kinachotofautiana ni sehemu, namna na mahali pa kupigia debe. hata wenye blog ni wapigadebe
KANISA LILISHIRIKI UTUMWA!!!

Niliyofundishwa kwamba walipokuja wamisionari hawakuja kufundisha juu ya Mungu, walikuja kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha kwamba wazungu wanapata watumwa kwa namna yoyote ile. Walikuja wakiwa wameshika baibo na wakakiri kabisa kwamba wao ni wema na mungu wao anaruhusu utumwa.

Usishangae! Majuzi kanisa la Angilikana limekubali na kusikitishwa na kitendo chake cha kushiriki katika biashara 'haramu kwa kipindi hiki' halali ya utumwa kwa kipindi kile. Akiongea mjini Landani jumamosi wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka200 tangu bunge la Uingereza lilipopitisha sheria ya kuzuia biashara na utumwa wenyewe, askofu mkuu wa canterbury daktari Rowan Williams alisema kwamba kanisa linasikitishwa na hali ile na linapanga kulipa fidia.

Swali, Watamlipa nani

Wednesday, March 21, 2007

NINI KINAMBEBA 'MTOTO WA MJINI'!!!

Unaikumbuka ile kesi ya wale jamaa waliomuua wakili Kapinga mnamo mwaka2002! Jamaa hawa walikaa rumande kwa muda wa miaka5 na hukumu ya kesi ilitaja kuwa walikuwa wakituhumiwa kumuua wakili huyo maarufu. Hawa hawakuonwa. Dito kaua hadharana na bado kamanda wa polisi anajaribu kutuaminisha kuwa bastola ilivyatuka kwa bahati mbaya! Amefanikiwa kwani mapema tu DPP aliibadili kesi toka mauaji mpaka kukusudia kuua.

Mahabusu wengi wenye kesi za namna ya 'mtoto wa mjini' wamekaa rumande kwa muda mrefu sana kwa kuwa tu 'upelelezi haujakamilika' (hawa si matajiri) jiulize jamaa waliotuhumiwa kumuua Kapinga hawakuona na yeyote lakini mahakama imewahukumu hukumu nzito kabisa. Dito, hadharani kabisa katoka ndani ya shangingi lake kashika bastola na kuifyatua ikimlenga dereva bado tunaambiwa eti hakukusudia kuua! Tunakokwenda siko.

Jiulize waziri mmoja anasimama na kusema kuwa kesi ya kigogo huyo imekuwa hivyo kwa sababu ana mawakili wazuri! mawakili wazuri ama kuna kitu kingine kilichoanzia kwa Tibaigana, mkurugenzi wa mashtaka na 'serikali'

Tunakokwenda siko na itafikia wakati wenye kutosikia watasikia na mabubu watasema, nimalize kwa kukumegea kipande ambacho mwanamuziki na mwanaharakati Tracy Chapman anasema katika wimbo wake 'Revolution'. Utafute na uusikilize utapata zaidi ya sauti nzuri na milio murua ya magitaa (mara nyingi hutumia gitaa tu)

Saturday, March 17, 2007

YA DITO, NDUGU ZAKE, DHAMANA NA MAHAKIMU!!!

Juma hili linamalizika huku mawaziri wanaohusika na usalama na haki za raia wakishindwa kuwashawishi mahabusu amabo wamekuwa wakigoma sasa mpaka nao kesi zinazowakabili mahakama zitasikilizwa kwa haraka kama ilivyotokea kwa mtuhumiwa wa kesi ya kukusudia kuua ndugu Ditto amabye kesi yake imechukua miezi mitatu tu na sasa yupo nje kwa dhamana kwani kosa lake lina dhaminika ilhali mahabusu wengi wakiwa gerezani kwa takribani miaka10 mpaka 15 kesi zao zikitajwa tu bila chochote kuendelea.

Wamegoma!

Nawashangaa sana hawa mahabusu amabo wameamua kugoma ili kushinikiza kesi zao ziharakishwe kama inavyotokea kwa kesi zinazowakabili vigogo ama watoto wao ama watu maarufu. Kesi zinatofautiana na watuhumiwa wanatofautiana sana kwani hata binadamu wote si sawa japo katiba yetu inayoongozwa na mfumo wa ujamaa kutamka kuwa binadamu wote ni sawa.

Kesi inayoendelea ya mheshimiwa inadhihirisha yale G. Orwell aliyosema katika kitabu chake maarufu kinachoitwa 'the animal farm' shamba la wanyama kuwa kuna binadamu wengine ni zaidi ya wengine.

ninakuwa ninajiuliza kuwa inawezekana ni mfumo wetu wa sheria una macho ama watendaji wenye dhamana ndio wanaoangalia na kuifanya sheria kuwa na macho na kuipotezea imani yake kuwa sheria ni msumeno!

Nimemshangaa jaji mkuu amabye ameshangazwa na kitendo cha wasalama kumpitisha kigogo katika mlango unaotumiwa na mahakimu, hivi hajui kuwa watuhumiwa wengine ni mahakimu tayari, kwenda mahakamani kwao ni kama kuwazuga tu na ndiyo maana wakati wanaogoma wanarundikwa kwenye makarandinga wao wanaletwa na taksi amabyo inalindwa na polisi wenye silaha ili kutotota nafasi kwa 'washenzi' kutotoa habari kwa umma.

Najiuliza wale ndugu wa mtuhumiwa waliowafanyia uhuni wapigapicha wa habari corparation walikuwa wanajua kuwa ni lazima ndugu yao atapewa dhamana! Hivi kama hakimu angekataza dhamana nani angeshambuliwa na ndugu hawa amabo mahakama waliifanya kama sehemu ambako mwali anatolewa kwa kwenda na kanga huku walinzi wa usalama wakiwaangalia kana kwamba wanachofanya kinaruhusiwa.

Ingekuwa ni 'kapuku' kweli angeruhusiwa kwenda hata na 'leso' ikiwa tu simu ya kapuku ikiita basi hima askari atakufuata na kukugombeza huku hakimu akitishia kukuadhibu kwa kuleta kelele kortini.

Sheria haina macho lakini waliodhaminiwa na wanachi kuitunza na kuiimarisha wamekuwa wabaguzi huku vigogo wakikrimiwa na walalahoi wakinyanyaswa hata kwa kufanya mepesi dhidi ya mazito yanayofanywa na vigogo
ETI TIMU YA MNMA KAMA 'ASENO'

Ni jana tu ambapo wanachuo walishuhudia timu yao ya mpira wa miguu ikicheza na timu ya vijana wa mtaani wanaojulikana kama 'nantes' timu ambayo mfadhili wake mkuu inaaminiwa ni mhasibu wa chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere ndugu Magulumengi.

Ikicheza kitimu timu ya chuo ilikukuwa ya kwanza kuliona lango la wapinzani wao kupitia kwa mfungaji wake makini Magesa aliyefunga bao tamu baada ya kupata pasi safi toka kwa kiungo mfungaji Marijani.

Bao hilo liliwafanya wageni wachanganyikiwe huku kiungo wa nantes Dinno akihangaika kuipita ngome ya chuo iliyokuwa chini ya ulinzi wa dogo Allan. Hadi kipindi cha kwanza kinakwisha chuo walikuwa wakiongoza kwa goli moja.

Kipindi cha pili timu ya wageni ilifanya mabadiliko yaliyosaidia kupatikana kwa goli la kusawazisha lililofungwa dakika 20 baada ya kipindi cha pili. Bao hili liliwaduwaza chuo na kujikuta wakicheza bila mpangilio na mabeki wakicheza faulo zilizosababisha chuo kufungwa goli la pili. faulo iliyopigwa dakika za majeruhi pembeni mwa lango la timu ya chuo ilizaa goli lililowaduwaza wachezaji na mashabiki wa chuo kwani licha ya kuwa timu yao ilifungwa bali lilimaanisha uteja wa kudumu kwani tangu 2005 timu ya chuo haijawahi kuwafunga vijana wa nantes ambao huongozwa na kapteni mwenye maneno mengi Ben Shoo.

Pamoja na mabdiliko makubwa yaliyofanywa na chuo ya kuwaingizi Chidi, Munga na seki timu ya chuo ililala na kumwacha mshabiki ambaye hujifanya kocha hanzuruni akiapa kutoshangilia tena timu ambayo haina dhamana.

Mashabiki walioongea na mwandishi wa blog hii walionekana kukerwa na kufungwa huku na wakaifananisha timu yao kama timu ya aseno ambayo mbali na kucheza mpira na kuumiliki kwa muda mrefu alkini wamejikuta hawana chao msimu huu.

Wednesday, March 14, 2007

NIPO NDANI YA MCHEZO!

Msomaji wangu tegemea kitu adimu toka katika blog hii, kinakuja

Thursday, March 08, 2007

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI!
JAMII IWAANGALIE WANAWAKE WAJAWAZITO!!!

Nimeamua kuandika waraka huu nia kubwa ikiwa ni kutaka kukuonesha wewe msomaji adha wanayoipata wanawake wengi wa Kitanzania hasa wanapokuwa wajawazito. Wanawake wajawazito hasa wale wa vijijini wanapata wakati mgumu sana na unaoogopesha pindi wanapokuwa wakifuata huduma ya 'kujifungua' katika hospitali za serikali.

Hospitali nyingi za serikali zimekuwa si rafiki wa wajawazito hasa wale wanaotoka vijijini ambako umaskini humsabahi kila mtu katika nchi hii inayohubiri maisha bora kwa kila mtanzania. Wanapofika hospitali wanalazimika kununua mahitaji ya kupatiwa huduma ilhali serikali imetangaza kuwa 'vifaa' hivi hupatikana bure kwa wote, hii si kweli.

Wanahitajika kujinunulia vifaa hivi ambavyo kwao ni ghali sana na wengine huamua kabisa kuacha kwenda hospitali kwani masaibu watakayokutana nayo huko yanatisha.

Kuna baadhi ya hospitali, tena nyingine zipo mijini kabisa kina mama wajawazito wamekuwa wakirundikwa wodini kama magunia ya viazi, huku kitanda kimoja kikilaliwa na wajawazito wawili 'wenye bahati' na wasiona bahati basi wasubiri saa katika sakafu.
Ni serikali yenye jukumu la kuhakikisha kuwa hospitali zake zina si huduma bora na vifaa tu bali wahudumu wapo wa kutosha na wanaowezestoa huduma kwa kila mmoja bila kujali hali ya kipato chake.

Leo tunapoungana na wanawake kushehereke siku yao duniani ni jukumu la kila mwanajamii na serikali kujiuliza wanawake wajawazito wanasaidiwa vipi
PONGEZI ZANGU KWA MAMA KATIKA SIKUKUU YA WANAWAKE DUNIANI!!!

Mama, mwanao nakuandikia waraka huu mfupi kwa ajili ya kukupongeza na kukushukuru kwa yote uliyofanya na unaendelea kuyafanya nia kubwa ikiwa ni kuhakikisha kuwa mwanao ninakuwa 'huru'. Mama, leo unaungana na wanawake wengi duniani kusheherekea siku hii nzuri na inayoheshimiwa na kila mwanadamu. Nakupongeza mama yangu kwa kuwa makini katika kuhakikisha ninakuwa na ustawi ulio mzuri na wenye maisha mazuri.

Nina mengi ya kukuandikia kuonyesha furaha yangu wakati unaungana na wenzako katika siku hii muhimu, sitaki nikuchoshe ila tu tambua ya kuwa u mwanamke bora zaidi na unastahili yote jamii inayoweza kutoa kwa ajili ya ustawi wako ambao unamaanisha ustawi wa jamii nzima.
Hongera mama
LEO NI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI!!!!

Wanawake duniani kote leo tarehe 8mwezi wa 3 wanaungana wote duniani kutambua siku yao. Jamii nyingi duniani zinawachukulia wanawake kama binadamu wa 'pili' huku wanaume wakiwa ni wa kwanza bila kujali mchango mkubwa unaoletwa na wanawake katika suala zima la kuleta maendeleo kwa taifa na familia kwa ujumla.

wanawake ni muhimu sana kwa taifa kwani ukiachana na jukumu lao kubwa la kuongeza 'wanachama' katika taifa, wamekuwa ni mstari wa mbela katika kujenga jamii bora kabisa kwa kujenga misingi imara ya tabia za watoto na hivyo kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya jamii.

Jamii zetu kwa sasa zimebadilika sana katika suala la kumtambua na kumthamini mwanamke, hapo zamani mwanamke alikuwa anabaguliwa na familia katika suala zima la elimu lakini kwa sasa hali ni tofauti kwa uwezo wao mkubwa darasani na mawazo yao endelevu vimechangia kujenga misingi madhubuti katika nyanja ya elimu. Kwa nchi kama tanzania, wasichana miaka miwili mfululizo wamekuwa wakiongoza katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na sita. Hii imeongeza changamoto kwa jamii kuona kuwa mtoto wa kike anafaa sana kusomeshwa na kama ule usemi wa msomi maarufu unaosema 'kumwelimisha mwanamke ni kuelimisha jamii' unatimia

Wednesday, March 07, 2007

ETI KIKWETE ANASAFIRI SANA!!!!!!!

Ni majuzi tu rais wetu mpendwa na ambaye pia ni mwenyekiti wa chama chetu kinachodumu amerejea kutoka safari ambazo sasa zimekuwa ni za kawaida kwake. Inawezekana watu wanaolaum safari hizi hawajui kuwa huyu aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje! Wewe unaonaje, unadhani hajasahau kuwa cheo sasa ni kipya?
HATA BLOG HII INABADILIKA!!!!

Msomaji wa machweo, nimekuwa nikikuandikia kuhusu mabadiliko makubwa yanayoendelea hapa chuoni ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya jina la chuo cha kumbukumbu ya nyerere mpaka kuteuliwa kwa viongozi wa kuongoza chuo na kubwa zaidi maktaba ya kompyuta kuanza kutumika.

Kwa mabadiliko haya, nami pamoja na waandaaji wa blog hii tunajipanga ili kuiboresha blog hii ivutie na pia kuongeza 'utamu' kwako msomaji.

Kwa sasa unapofungua blog pembeni utaona viunganishi ambapo utaweza kutembelea blog nyingine za kiswahili ikiwemo ya Ndesanjo, Mkina, Ngurumo na ile ya katuni za Kipanya.

Mengi yanakuja nami nawaahidi kuwapa kile mnachoona kinafaa, tafadhari msisite kutuma maoni yenu katika blog hii

Friday, March 02, 2007

NI MABADILIKO TU KILA KONA, UMEYAONA MASHANGINGI...

Leo imekuwa ni siku njema na ya furaha sana kwa walioteuliwa kushika nyadhifa hapa chuoni, kama huna habari ya uteuzi huu ngoja nikupashe kidogo. Juma lililopita bodi ya chuo chini ya m/kiti dr Salim A. Salim iliwateua ndugu Mushi na ndugu Luambano kushika nyadhifa za juu kabisa hapa chuoni, Mushi aliteuliwa kuwa naibu wa mkuu wa chuo na Luambano kuwa msajiri wa chuo, hii imekuwa ni habari njema kwao.

Licha ya uteuzi kumaanisha 'posho' kuongezeka na majukumu tele lakini uteuzi huo umeendana na kuletwa kwa 'mashangingi' magari mazuri ya kifahari (sema ya anasa) ili kurahisisha utendaji kazi wa vionngozi hawa.

Jumuia tumeombwa kutoa ushirikiano kwao lakini hatujaona sehemu wao walipoombwa kutoa ushirikiano kwetu, labda tutapata lifti! Tusubiri tuone
WAMESIKIA KILIO CHETU, SASA TUPO MTANDAONI!!!!!

Niliwahi kukuandikeni kuhusu kutokuwapo kwa huduma ya kisasa ya intanet hapa katika chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere, kwa sasa hii leo inaweza kuwa ni historia kwani kwa muda huu ninapokuandikia nimo ndani ya chumba ambacho zamani kilikuwa kimefungwa kwa makufuri makubwa ya solex na milango ya vyuma yakihifadhi kompyuta, ninakuandikia habari hii huku mwalimu wa somo akiwa pembeni.

Wanachuo sasa hatuna haja kwenda 'ferry' ili kupata huduma hii muhimu ambayo baadhi ya 'watu' wanaiona kama ni ya anasa.

lakini kikubwa kinachoonekana hapa ni ratiba ya kuingia madarasani kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanaamua kushinda 'lab' wakiamini mtandao ndo kila kitu, labda ni 'ugeni'.
Tusubiri tuone mabadiliko ambayo yameendana kabisa na uongozi mpya wa chuo