Monday, November 20, 2006

Kutodhibiti fedha hizi, kauli ya Kikwete itakuwa ndoto

MIONGONI mwa falsafa ambazo zinanigusa mno nafsi yangu ni msimamo wa Rais Jakaya Kikwete kuhusu suala zima la ukuaji wa uchumi.

Rais Kikwete amekuwa akisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unaoelezwa kwa wananchi na ama wataalamu wa uchumi au viongozi wa siasa, kwamba uchumi umekua huku hali za wananchi zikiwa duni haiwezi kuwasaidia.

Kiongozi huyo wa nchi ambaye nyota yake ya kukubalika inazidi kung’ara kwa rika zote na kwa watu wa kada mbalimbali, ana maana kuwa takwimu zilizoko katika karatasi zikionyesha kukua kwa uchumi ni ‘hesabu’ ambazo hazieleweki kamwe kwa mwenye njaa.

Idadi kubwa ya Watanzania ni watu masikini ambao hawawezi hata kuhimili idadi ya kawaida ya mlo wao kwa siku moja.

Ukweli ni kwamba Watanzania wengi hawana njia za kuwahakikishia wanapata chakula cha kutosha na chenye ukamili wake kwa ajili ya mahitaji ya mwili. Mwili huhitaji vyakula vya kujenga, kulinda na ‘kuunakshi’ ili uvutie.

Kutokuwepo kwa ‘msosi’ wao wa uhakika kunasababishwa na mambo mengi, makubwa yakiwa ni rushwa, kutotendewa haki, ubadhirifu wa baadhi ya watendaji wa umma na hujuma za kila aina zinazofanywa ili kuwanufaisha wachache katika jamii.

Juhudi za Rais Kikwete kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anafaidi keki ya rasilimali zetu na uhuru uliopatikana kwa ‘mbinde’ zinaonekana na dhamira yake iko wazi.

Ni dhamira hiyo inayowapa moyo zaidi wa kuwepo kwa neema kwa kila mmoja wetu, ingawa bado ipo kazi ambayo inahitaji pia ushirikishwaji wa wananchi wenyewe katika kuupiga vita umasikini, ambao ulionekana kuwa chanda na pete miaka mingi iliyopita baada ya 1986.

Hata hivyo, upo mwanya ambao hakuna anauyeuzungumzia kuwa ni kikwazo katika kuwakomboa Watanzania na ‘njaa’ inayowakabili.

Njaa ninayoizungumzia hapa ni pamoja ukosefu wa makazi bora, kuzungukwa na magonjwa kibao ya kuambukiza na zaidi sana njaa ya tumbo, ambayo kimsingi ndiyo ufunguo unaozungumzwa na Rais Kikwete.

Mwanya huo ni kuwepo kwa ‘njia nyeupe’ kwa baadhi ya wafanyabiashara kupeleka fedha za kigeni nje ya mipaka ya nchi yetu bila kuulizwa na yeyote.

Hivi sasa kila mfanyabiashara wa fedha; awe Mtanzania wa kuzaliwa, kuomba au hata kudanganya, anao uwezo wa kusafirisha kiasi chochote cha fedha bila kupitia Benki Kuu au katika taasisi zinazoshughulika na masuala ya uchumi.

Haihitaji kuwa na karatasi kutoka chuo chochote kutambua kuwepo hilo na kuthibitishwa na jinsi dola ya Marekani, paundi ya Uingereza inavyopanda kila uchao dhidi ya fedha yetu, ambayo baadhi ya watu wasiokuwa na utaifa wanaziita za madafu. Sina uhakika wanayaangua wapi hayo madafu!

Kuondoka kwa kiasi kikubwa cha fedha ndiko kunasababisha mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa huku wahusika wakifaidi na ‘walalahoi’ ambao ndiyo wanunuzi wakubwa wakikamuliwa hadi tone la mwisho.

Hivi sasa dola moja ya Marekani ni sawa na sh. 1,335 na kwamba kesho au Jumamosi kiasi hicho kitakuwa kimeongezeka kwa asilimia 10 au zaidi. Inatisha sana hali hii.

Nguvu ya soko la dunia mara zote imekuwa ikipimwa kwa kuzingatia fedha ya Marekani, hivyo shilingi yetu zinapokuwa nyingi zaidi kwa dola moja, uchumi wetu unashuka kwa njia moja hata kama itaelezwa kinyume chake.

Zipo nchi ambapo kupata dola moja ya Marekani lazima muhusika atembee kweli kweli kutoka Benki Kuu hadi taasisi zinazohusika, ambako atapatiwa karatasi lukuki kumuhalalisha kuwa anapaswa kupata na kutumia fedha hizo.

Lakini hapa kwetu kila kitu ni bwerere…na ruksa. Ukitaka dola za Marekani nenda tu mtaa wowote, hata kama ni dampo kule Tabata, utapata tu. Hakuna haja ya kuuliza benki ziko wapi. Kwa nini ujisumbue bwana! Ya nini! Ndivyo tulivyo.

Inaweza kabisa kuelezwa kwamba KONA YANGU inahitaji kuwepo kwa urasimu uliokuwepo miaka mingi iliyopita. Hapana hiyo siyo nia yangu.

Lakini ieleweke kuwa bila udhibiti wa fedha hizo za kigeni tutakuwa tukitwanga maji kwenye kinu, na kwamba kauli za viongozi wetu zinaweza kuwa zile zile zilizozoeleka masikioni mwetu.

Hakuna maendeleo bila udhibiti wa mambo kadha wa kadha ikiwemo rushwa na dhambi nyingine, ambazo nimekuwa nikizipigia kelele kila ninapopata nafasi ndogo katika ukurasa huu kueleza.

Ni vyema sasa serikali yetu ikabuni mbinu za kudhibiti usafirishwaji wa fedha za kigeni zinazopatikana hapa nchini, ili kulinda nguvu ya shilingi yetu, hivyo kuimarisha uchumi ambao utatuhakikishia maisha bora kwa kila Mtanzania.

Inawezekana.

Monday, November 06, 2006

WANAOMILIKI SILAHA WAKO TIMAMU!!!

Imetokea majuzi kwa mkuu wa mkoa wa tabora, mtoto wa mjini Dito amemuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala kwa kuwa tu jamaa aligonga gari la mhe. huyu lililokuwa likiendeshwa upande wa watembea kwa miguu. Hii ya kutembea kwenye service road si ishu yangu bali ninauliza hivi kweli kuna uhalali wa kiongozi wa serikali kama Dito kutumia bastola yake kumtaka dereva ashuke garini! na polisi wanatuambia eti ililipuka kwa bahati mbaya!

Naogopa sheria isije ikafumba macho. Tusubiri